Pages

Friday, July 22, 2011

THT yalipuliwa bungeni


MBUNGE wa Meatu, Meshack Opolukwa (Chadema) amelilipua bungeni Kituo cha Kukuza Vipaji (THT) cha Dar es Salaam akisema, kinawafanyisha kazi wasanii kwa ujira mdogo.

Pia amesema baadhi ya wasanii wanaokimbilia kwenye kundi hilo kwa nia ya kupata mafanikio ya sanaa wanaishia kupata mimba na kupangiwa kuishi nyumba za uswahilini.

Akizungumza bungeni jana jioni wakati akichangia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Mwaka 2011/2012 ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto iliyosomwa na Waziri wa Wizara hiyo, Sophia Simba, Mbunge huyo alihoji kama kundi la Tanzania House of Talent (THT) limebadili malengo yake wakati ikisajiliwa.

Alisema, kundi hilo lilianzishwa kwa ajili ya kusaidia wasanii yatima na kwamba hajui kama sasa limebadilishwa na kuwa kampuni inayojiendesha kibiashara.

Alisema, kutokana na hali hiyo wapo vijana wanakimbilia kwenye kundi hilo kwa nia ya kupata mafanikio ya sanaa, lakini badala yake wanaishia kufanyishwa kazi kubwa kwa ujira mdogo.

“Na wengine mabinti wanaishia kupata mimba na kupangiwa nyumba za uswahilini…., Serikali iseme kama kundi limebadilisha malengo yake ya awali au la. Vinginevyo tutakuwa tunapoteza mapato mengi,” alisema Mbunge huyo.

Hata hivyo wakati akifanya majumuisho ya hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge, Waziri Simba hakulizungumzia jambo hilo kutokana na muda kuwa finyu na kuwa mengine angeyafanyia kazi na kuwajibu wabunge.

Opulukwa alisimama tena wakati Bunge likiwa limekaa kama Kamati ya Matumizi na kutoa hoja kwamba, aliulizia suala la THT kama imebadili usajili au vipi, hivyo kuomba ufafanuzi kwa Waziri.

Akizungumzia hoja hiyo Waziri Simba, alisema kwa jana ingekuwa vigumu kwake kuweza kujibu jambo hilo na kuomba apewe muda alishughulikie ili kufahamu ukweli.

Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), alisimama wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Matumizi na kutoa hoja kuwa wasanii mpaka wanafikia hatua ya kujulikana wanapitia hatua mbalimbali za kunyanyaswa.

Alisema wasanii hao wa muziki na filamu hasa wa kike wananyanyasika kwa kiasi kikubwa lakini hawasemi, hivyo kuhoji kama Serikali ina taarifa hizo ili kuhakikisha wanalindwa na kuwa na hadhi.

Akizungumzia hilo, Waziri Simba alisema suala la manyanyaso si kwa wasanii tu hata sehemu nyingine halikubaliki na kushauri kwamba wanaofanyiwa unyanyasaji hawana budi kutoa taarifa.

Hata hivyo alimuomba Mbilinyi ambaye pia amepata kuwa msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya akijulikana kwa jina la Mr II au Sugu, kama ana ushahidi kuhusiana na manyanyaso hayo ampatie Waziri na pia naye aweze kuwasaidia wasanii hao ambako ndiko alikotokea.

Wizara hiyo iliidhinishiwa Sh bilioni 16.2 kwa mwaka 2011/2012.

No comments:

Post a Comment