Pages

Friday, July 22, 2011

FAMILIA YATAABIKA


MKAZI wa kitongoji cha Mkocheni, kijijini Makuyu, wilayani Mvomero, Lenati Abdallah (74) analazimika kutumia zaidi ya lita 200 za maji kila siku kwa ajili ya usafi wa miili na mavazi ya watoto wake watano wenye ulemavu.

Watoto hao wenye umri tofauti, miongoni mwao wa kike ni mmoja, na wamekuwa wakitambaa na kujisaidia haja ndogo na kubwa sehemu wakaapo usiku na mchana.

Mwandishi wa habari hizi, aliyetembelea kijijini hapo hivi karibuni, alipata fursa ya kuzungumza na mzee huyo, ambaye alisema watoto hao walikumbwa na ugonjwa huo baada ya kuzaliwa wakitanguliwa na Charles Lenati (21).

Watoto wake wengine ni Severine (18), Vailet (15), Emmanuel (11) na mjukuu Joseph Harman (14).

Kwa mujibu wa Abdallah, watoto wake hao wanne na mjukuu pia hawawezi kuzungumza, na hivyo analazimika kutumia muda wake mwingi akiwa nyumbani kwa ajili ya kuwahudumia kwa kila jambo.

“Nina mzigo mkubwa wa kulea watoto hawa … ni kipimo cha Mungu mwenyewe ambaye ameniambia ‘hebu jaribu kuubeba mzigo huu’, siwezi kumlaumu mtu yeyote,” alisema Abdallah. Hata hivyo, aliongeza kuwa madaktari wameainisha kwamba,”watoto hawa wana mtindio wa ubongo, licha ya kuwa na ufahamu wa kusikia jambo,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, yeye na mkewe, Maria Lucas, hulazimika kutumia lita zaidi ya 200 za maji kwa usafi wa watoto hao kwa kuwaogesha na kuwafulia nguo.


“Hapa mtihani mkubwa ni maji, nikikosa maji, hali inakuwa mbaya, hakuna mtu anayeweza kuwasogelea, magorodo nayo yameharibika kwa mkojo hasa ukizingatia hawa ni wakubwa,” alisema. Hata hivyo, alisema watoto hao kila walipokuwa wakikaribia umri wa mwaka mmoja walipatwa homa kali – degedege - na walipokuwa wakifikishwa hospitali ya Turiani walitibiwa, lakini hata baada ya kukua kwa miaka miwili hawakutambaa, kusimama wala kutembea kama watoto wengine wakuavyo.


“Madaktari walitaka kujua historia iwapo huko nyuma babu zetu miongoni mwao walikuwa kama hawa, lakini haikuwa hivyo … ni majaribu ya Mungu,” alisema Abdallah. Hata hivyo, aliushukuru uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Mvomero, kwa kuwapa msaada wa baiskeli nne za magurudumu manne, mahindi magunia matatu, mafuta ya kula ndoo moja, sabuni katoni moja, sukari kilo 25 na chumvi pakiti 10 sambamba na wadau wengine.

Uongozi wa Serikali ya Kijiji hicho, kwa kushirikiana na taasisi isiyo ya Serikali, wanakusudia kujenga kisima cha maji karibu na makazi ya familia hiyo, ili kuiwezesha kuondokana na adha ya maji.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Hamza Kitegile, alisema kutokana na familia hiyo kukabiliwa na adha ya maji, Serikali ya Kijiji imeomba msaada kwa taasisi hiyo inayosambaza maji ya visima iwachimbie kisima karibu na makazi hayo.

“Hii taasisi imekubali na imetenga bajeti ya kuchimba kisima na kujenga choo kitakachofaa kwa matumizi ya familia hiyo,” alisema Mwenyekiti huyo.
habari leo.

No comments:

Post a Comment