Thursday, August 28, 2014

OKWI : SEASON 2

STAILI ile ile waliyotumia Yanga SC kumpata mshambuliaji Emmanuel Arnold Okwi ndiyo ambayo klabu yake ya zamani, Simba SC inaitumia kumrejesha kundini Mganda huyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jioni hii mjini Dar es Salaam, Okwi amesema kwamba amesaini Simba SC mkataba huru wa muda, baada ya Yanga SC kumpa barua ya kusitisha mkataba naye jana pamoja na kumshitaki Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Okwi amesema ameamua kuomba kuichezea Simba SC kipindi hiki ambacho ana matatizo na Yanga SC ili kulinda kipaji chake, kwa kuwa hata FIFA haitaki mchezaji akae bila kucheza.


Msimbazi ni nyumbani; Okwi akiwa na jezi ya Simba SC baada ya kurejea timu yake ya zamani leo

“Sasa wakati Yanga wanaendelea na kesi yao, mimi ninaomba nichezee Simba SC ili kulinda kipaji changu. Nimewaandikia barua TFF na FIFA pia na nina matumaini usajili wangu utaidhinishwa, kwa sababu mimi si tatizo katika hili,”amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba wamemsaini mchezaji huyo baada ya kupitia kwa kina suala lake na Yanga SC na kugundua haki ipo upande wa mchezaji.
“Baada ya kulipitia suala lake na Yanga kwa undani kabisa na vielelezo ambavyo mchezaji mwenyewe ametupatia, tumejiridhisha tuko sahihi kumsaini ili acheze mpira kunusuru kipaji chake kipindi hiki ambacho ana matatizo na Yanga SC,”amesema Poppe.

Yanga mtanikoma; Okwi akiwa ameshika jezi yake nbamba 25 kwa pamoja na Hans Poppe

Tayari Simba SC imetuma jina la mchezaji huyo katika usajili wake TFF na ataungana na Mganda mwenzake, Joseph Owino, Warundi Pierre Kwizera na Amisi Tambwe na Mkenya, Paul Kiongera katika wachezaji watano wa kigeni.
“Tumewaandikia barua TFF kuomba kumtumia mchezaji huyu kwa muda wakati kesi yake na Yanga inaendelea, tumeambatanisha na barua yake ambayo yeye anatuomba kucheza kwetu kulinda kipaji chake,”amesema Poppe.
Okwi aliichezea Simba SC tangu mwaka 2009 kabla ya Januari mwaka jana kuuzwa kwa dola za Kimarekani 300,000 Etoile du Sahel ya Tunisia.
Etoile haikulipa fedha hizo Simba SC na baadaye ikaingia kwenye mgogoro na Okwi, aliyedai hakulipwa pia mishahara yake kwa miezi mitatu.
Okwi akawafungulia Etoile kesi FIFA na akaomba wakati mgogoro wao unaendelea, aruhusiwe kuchezea timu yoyote kulinda kipaji chake, ndipo akajiunga na SC Villa ya kwao.
Akiwa SC Villa ndipo aliposaini Yanga SC Desemba mwaka jana na pamoja na mapingamizi yaliyoanzia ndani, na baadaye klabu yake, Etoile- lakini Okwi aliidhinishwa kuichezea timu hiyo ya Jangwani.
Okwi aliichezea Yanga SC mechi 11 na kuifungia mabao matano- lakini kuelekea mechi tano za mwisho za Ligi Kuu msimu uliopita akaingia kwenye mgogoro na klabu hiyo.
Okwi alisusa kushinikiza amaliziwe fedha zake za usajili na mgogoro wao umeendelea huku mchezaji huyo akiwa amesusa tangu Machi, miezi minne tu baadaye tangu asajiliwe.
Vikao kadhaa vimekwishafanyika baina ya Okwi na Yanga SC tangu hapo kutafuta suluhu ya suala hilo na kikao cha mwisho leo baina ya mchezo huyo na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji matokeo yake ni nyota huyo kurejea Msimbazi.
Kuhusu deni lao la dola 300,000 kumuuza mchezaji huyo Etoile, Poppe amesema haihusiani kabisa na usajili wake huu wa sasa. “Ile kesi yetu ya madai ya fedha zetu kule FIFA ilikwishamalizika na vielelezo vyote vilipelekwa, bado kutolewa hukumu tu,” amesema.
 
Msaada Bin Zubery

MWANAO MLETE HUKU

Hii ni shule ya awali maarufu chekechea huko Mbarali

Friday, August 15, 2014

Kikwete: Uraia pacha kwa sasa ni ndotoDar/Dodoma. Rais Jakaya Kikwete amesema suala la uraia wa nchi mbili linaonekana kutokuwa na nguvu kwa sasa kutokana na kutojitokeza katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hivyo kutoingia katika Rasimu ya Katiba inayojadiliwa sasa bungeni.
Kauli ya Rais Kikwete imekuja wakati suala hilo likionekana kuwagawa wajumbe katika Kamati za Bunge Maalumu, kutokana na kuwapo kwa mapendekezo kwamba suala uraia pacha liingizwe kwenye rasimu hata kama halikuwekwa na Tume.
Juzi, suala hilo liliwagawa wajumbe wa Kamati Namba mbili inayoongozwa na Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na kusababisha ibara hiyo kukosa theluthi mbili ya kura kutoka pande zote za muungano.
Akizungumza katika kongamano maalumu linalowakutanisha Watanzania waishio nje ya nchi Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema suala hilo limekosa wasemaji wanaoguswa moja kwa moja ambao wangeweza kulitetea, hivyo kutokuwa miongoni mwa vipaumbele katika rasimu hiyo.
“Msijipe matumaini kwa sababu kwa namna ilivyoandikwa kwenye Rasimu ya Katiba, haiwezi kuzaa uraia wa nchi mbili, bali inaweza kutoa stahiki ya fursa wanazoweza kupata Watanzania waishio nje ya nchi, kupitia sheria,” alisema.
Kongamano hilo la kwanza la siku mbili

linawakutanisha Watanzania waishio katika nchi 17 duniani, lililoandaliwa na Asasi ya Tanzania Diaspora Initiative (TDI).
Rais Kikwete alisema Serikali yake inafahamu umuhimu wa kupatikana kwa uraia pacha kwa watu wake lakini suala la uraia ni la kikatiba na siyo la Rais kwa kuwa Katiba ndiyo inayoamua.
Alisema hata chama chake (CCM), kilipojaribu kuliingiza lilionekana kutokuwa na nguvu ya kutosha kwa kuwa hakuna ambaye lilikuwa likimgusa moja kwa moja.
Aliwashauri kuwatumia wajumbe katika Bunge linaloendelea mjini Dodoma ili wapaze sauti zao na ikiwezekana watumie fursa zote za mawasiliano kufikisha ujumbe wao.
“Sisi upande wa Serikali tunaliona ni suala jema, ila halina nguvu kwa sababu wabunge wengi haliwagusi moja kwa moja, hivyo si rahisi kulipigania. Mbona nchi nyingine watu wao wananufaika na hili! Kwa nini hapa kwetu lishindikane?” alihoji.
Ndani ya kamati
Habari kutoka ndani ya kamati zinasema wajumbe wamegawanyika kuhusu suala hilo na wengine wameshindwa kufikia mwafaka kama ilivyotokea katika Kamati namba 11 inayoongozwa na Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela.

Mwandishi wetu alidokezwa kuwa kulikuwa na mvutano mkali kuhusu pendekezo la kuanzishwa kwa uraia pacha na hadi sasa uamuzi wa kura bado haujafanyika kuhusu suala hilo na wajumbe wa Kamati namba tano inayoongozwa na Hamad Rashid Mohamed walikubaliana kwa kauli moja kuongeza ibara inayoruhusu kuanzishwa kwa uraia pacha.
Itakumbukwa kuwa suala hilo ndilo lilizua mvutano mkali baina ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi na Watoto, Sophia Simba kiasi cha kutoleana maneno makali wakati wakilijadili kwenye Kamati namba 6 inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira.
Taarifa ya nyongeza na Mwandishi Wetu, Dodoma

Hofu ya ebola Dar, mgeni kutoka Benin alazwa Temeke


Watu wakikatiza kwenye lango la kuingilia katika Hospital ya Temeke, sehemu ambayo anayedaiwa kuwa mgonjwa wa Ebola amelazwa

Dar es Salaam. Hofu ya ugonjwa wa ebola imeingia jijini Dar es Salam baada ya msichana anayedhaniwa kuwa na ugonjwa huo kutua nchini akitokea Benin, Afrika Magharibi na kulazwa katika Hospitali ya Temeke.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Amani Malima alithibitisha kuwapo msichana huyo mwenye umri wa miaka 14 aliyeingia nchini jana kuonekana akiwa na dalili hizo.
“Huko alikotoka alihisiwa kuwa na dalili hizo, alipofika hapa madaktari walipomhoji alisema ana maumivu makali ya viungo, miguu na mikono,” alisema.
Dk Malima alisema baada ya kupata maelezo hayo, walichukua vipimo vyote vya damu na majibu yake yatatoka leo kujua kama ana ugonjwa huo au la.
“Tumegundua kwamba ana malaria lakini vipimo vya ebola majibu ni kesho (leo), hivyo tunaangalia namna ya kumtibu na kama atakuwa hana ugonjwa huo tutamruhusu,” alisema Dk Malima.

Chanzo: Mwananchi

Sunday, August 10, 2014

KILICHOMUONDOA LOGA SIMBA HIKI HAPA


MBUNGE ZUNGU AKUMBUKA MIFEREJI YAKE

Mbunge wa Ilala Mh.Mussa Zungu leo akiwa katika operesheni maalum ya kuondoa kero ya mifereji iliyoziba maeneo ya kariakoo na gerezani


baadhi ya eneo ambalo mifereji yake imeziba na kusababisha harufu mbaya

Wednesday, August 6, 2014

UGAWAJI WA VITAMBULISHO VYA URAIA-TEMEKE

 Baadhi ya Wananchi wakisubiri vitambulisho vya uraia katika ofisi za Nida wilaya ya Temeke
baadhi ya wafanyakazi wakiendelea kugawa vitambulisho vya Taifa