Pages

Friday, June 10, 2011

Wanafunzi DUCE waivaa Bodi ya Mikopo


Baadhi ya wanafunzi wa Chuo kikuu kishiriki cha ualimu Chang'ombe(DUCE) wakiwa katika Ofisi za Bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu, Dar es salaam jana wakishinikiza kulipwa madai mbalimbali kuhusiana na mikopo.

Na Salim Nyomolelo

WANAFUNZI wa Chuo Kishirikishi cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE) wameandamana kwenda Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kulalamikia kudaiwa fedha za ada
wakati wamekwishalipa.

Wamesema madai hayo ya ada yanategemeana na daraja ambalo wanafunzi hao walipangiwa baada ya kujaza fomu za mkopo, ambapo wenye daraja A wanalipiwa fedha zote, daraja B wanalipiwa asilimia 80, daraja C asilimia 60, daraja D asilimia 40 na daraja E wanalipiwa asilimia 20.

Fedha za masomo kwa mwaka ni sh. milioni 1.2 ambapo wanafunzi wenye daraja A wanalipiwa zote na bodi, lakini bodi imetoa majina ya baadhi ya wanafunzi wa daraja hilo wanaodaiwa.

Mmoja wa wanafunzi hao, Bw. Jumanne Nyakirang'ani alisema chuo kinawadai walipe fedha hizo na walipohoji kwa Bodi ya Mikopo walijibiwa kuwa bajeti yao imekwisha, jambo ambalo lilizua maswali kwa jinsi gani bajeti imeisha bila ya fedha kutumika.

Bi. Sophia Bakari, mwanafunzi wa mwaka wa tatu alisema alipata mkopo wa daraja C ambapo Bodi ya Mikopo ilitakiwa kumlipia sh 720,000 kwa mwaka na yeye kulipa sh 480,000.

Alisema ameshamaliza kulipa fedha zote kwa miaka yote mitatu, lakini chuo kimemwandikia deni la sh. 800,000 wakati mwisho wa masomo ni Julai 22, mwaka huu.

Wanafunzi Uliza Jape, Wakuru Manini, Eliza Mole ni miongoni mwa walipata mkopo wa daraja A ambao hawakutakiwa kulipa kiasi chochote lakini wanadaiwa shilingi milioni 1.

"Mimi nimeandikiwa deni la sh. 320,000 ambayo ni ada niliyotakiwa kulipa mwaka wa pili, na bodi tukiwauliza wanasema bajeti imeisha wakati fedha hazikutumika, na mimi ni mtoto wa mkulima," alilalama Hapiness Swai.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo aliyesikiliza malalamiko yao, Bw. Asange Bangu aliwaleza kuwa bodi hiyo itawasiliana na uongozi wa chuo hicho ili wanafunzi hao wasidaiwa fedha hizo.

Wanafunzi hao pia walipewa barua ya kupeleka chuoni inayoelezea kuwa uongozi wa chuo usiwadai fedha hizo na umewahakikishia kuwa ifikapo Jumatatu watakuwa wamemaliza mchanganuo wa kubaini makosa yaliyofanyika.`

No comments:

Post a Comment