Pages

Thursday, September 29, 2011

BUNDI HUANZA KURUKA JUA LINAPOZAMA

 
Ndugu zangu,


Bundi  ana kawaida ya kuanza kuruka  jua linapozama. Bundi haoni kwenye mwanga, ndio maana ya kulisubiri giza.

Nchi yetu imeingiwa na giza nene na bundi ameanza kuruka.  Ngoja nikutafunie msomaji, giza hilo ni ufisadi uliotamalaki na hali ya kukosa maarifa.  Ufisadi  chanzo chake ni maradhi ya kuendekeza ubinafsi. Na kibaya zaidi, ubinafsi huo unapofanywa na viongozi.

Ndio,   aliye gizani anamwona aliye kwenye mwanga, lakini aliye kwenye mwanga hamwoni aliye gizani. Na ajionaye yuko kwenye mwanga aweza kabisa kuwa yu gizani na asimwone kabisa aliye kwenye giza jingine. Haiyumkini aliye topeni akajaribu kumwinua mwingine aliye topeni, wote watadidimia topeni!

Waongozwa wengi wako gizani, lakini hata wale viongozi waliodhaniwa kuwa wako kwenye mwanga na wana uwezo wa  kuwasaidia kuwatoa wananchi gizani, nao yaonekana ndio walio  gizani na wanaochangia kutubakisha gizani . 

Hakika, mambo mengine wayafanyao wanayafanya kama vile hawakusoma hata madarasa matano ya Shule ya Msingi, ni ya ajabu, ni mambo yanayofanywa  au kusemwa na watu wajinga. Watu walio gizani.

Ndio,  tatizo kubwa  kwa baadhi ya hao viongozi ni kuendekeza ubinafsi na kupenda sana U-bwana Mkubwa. Ni ushamba fulani hivi.  Na kwa hali ilivyo sasa, wananchi wameanza kuonyesha kuchoshwa na hali iliyopo inayosababishwa na baadhi ya viongozi wao. Wananchi hawa hawawezi kukaa kimya daima, ni mjinga tu atakayeamini kuwa jambo hilo linawezekana. Umma umeanza sasa  kuamka na kusema, ‘ basi, inatosha’. 

Maggid,
Iringa, 
 Septemba, 2011

No comments:

Post a Comment