Pages

Friday, September 16, 2011

‘Uwezo wa wanafunzi kusoma Kiswahili ni mdogo’

WANAFUNZI watatu tu kati ya 10 wa darasa la tatu ndiyo wanaweza kusoma hadithi ya Kiswahili huku mwanafunzi mmoja kati ya 10 akiweza kusoma hadithi ya Kiingereza kwa darasa hilo.

Aidha, wanafunzi watatu kati ya 10 wa darasa hilo wakiweza kujumlisha, kutoa na kuzidisha ambapo uwezo wao ukitofautiana kutokana na mazingira.

Hayo yamo katika ripoti ya utafiti uliofanywa Mei mwaka huu na Taasisi ya Uwezo katika wilaya 132 nchini na kuwahusisha wanafunzi 128,000 ili kutambua uwezo wao wa kusoma Kiswahili, Kiingereza na kufanya Hisabati.

Mratibu wa Utafiti huo, Dk. Grace Soko alisema tathmini hiyo ililenga kupima uwezo kwenye kiwango cha wanafunzi wa darasa la pili katika kila somo ikimaanisha kuwa wanafunzi wa darasa la tatu na madarasa ya juu wanapaswa kufaulu majaribio hayo.

Soko alisema katika kusoma hadithi rahisi ya Kiingereza, yalionesha chini ya nusu ya wanafunzi wa darasa la saba waliopimwa, walisoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili huku wengi wakifanya vizuri katika Hisabati kuliko kusoma kwa tofauti ndogo.

Alisema katika darasa la saba matokeo ya kila wilaya yanatofautiana kulingana na mazingira ambapo Iringa mjini ufaulu ni asilimia 84 huku Kibondo ikiwa kwa asilimia 14 huku kati ya walimu watano mmoja hakuwepo shuleni wakati wa tathmini hiyo.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba alisema imefika wakati wa Tanzania kujenga utamaduni wa kutumia ushahidi wa utafiti katika kutunga sera.

Aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuchukua ripoti hiyo kama changamoto na kuacha kubeza kuwa ni za uongo kwani wadau hao wametoa hadi kwa jinsi gani wamepata matokeo hayo.
Habari leo

No comments:

Post a Comment