Pages

Tuesday, May 31, 2011

YA BABU WA LOLIONDO NA USHAURI WA WAMAREKANI


Na Maggid Mjengwa,

INAYODAIWA kuwa tiba ya Babu wa Loliondo, badala ya kuwa msaada kwa taifa, imeanza kuonyesha madhara zaidi ya kiafya, kijamii na kiuchumi. Tuliandika kutahadharisha na kushauri. Tumepuuzwa; maana, kwa wengine, tiba ya Babu sasa ni mradi, na kwa kweli umeanza kugeuzwa kuwa mradi wa kitaifa.

Na kilichojikita katika kuwaacha watu wetu wakitaabika ni unafiki wetu. Tuna maradhi mabaya, na ni sugu. Ndio, miongoni mwetu kuna wenye kusumbuliwa na maradhi ya unafiki. Nitatoa mfano wa juzi tu; nilikaa na wasomi wawili, tena wana digrii zao. Tukazungumzia ya Babu wa Loliondo.

Mimi na wasomi wale tulikuwa na misimamo ya kufanana, tulipinga upotoshaji unaoendelea katika jamii kuwa Babu wa Loliondo, Ambilikile Mwasapile , anatibu ukimwi, kansa, kisukari na mengineyo. Na kwa vile wote tumekwenda shule, hoja kuu ilikuwa hii; kuwa hadi sasa hakuna hata wagonjwa watatu wa ukimwi waliothibitishwa kitaalamu kuwa wamepona ukimwi kwa dawa ya Babu. Badala yake, kuna wengi wamekufa baada ya kuacha kutumia madawa waliyoelekezwa na madaktari watalaamu waliosomea tiba.

Wakati tukiendelea kuzungumza, mara akatokea mheshimiwa fulani, naye akaingia moja kwa moja kwenye mjadala. Alimtetea Babu na kusisitiza kuwa Babu ni lulu ya taifa, lazima aenziwe. Wasomi wale afadhali wangekaa kimya, hapana, walianza kumuunga mkono mheshimiwa kwa hoja nyepesi.
Hawakuwa wapumbavu, walijifanya tu wapumbavu wakiniacha mimi nikipambana peke yangu kuziponda hoja za mheshimiwa yule. Kwa kiasi fulani, niliogopa kuona hulka hii ya wasomi wetu. Wasomi ambao, kwa unafiki, wanashindwa kutetea na kusimamia katika hoja zao za msingi. Na hii, bila shaka, ni moja ya majibu ya swali la kwa nini Tanzania ni masikini?

Hakika, ya Babu wa Loliondo ni aibu yetu kitaifa. Katika karne hii ya 21 nchi yetu inatumia raslimali zake kufanya promosheni ya ndoto ya Mtanzania mmoja kati ya Watanzania milioni 42! Ndio, tunafanya promosheni ya jambo lisilo na uthibitisho wa kisayansi. Si tunaona, haipiti siku bila kusikia habari za Babu wa Loliondo?

Kwa sasa, tunaweza kabisa kusema, kuwa habari za huduma za Babu wa Loliondo zinatangazwa na kuufikia umma kuliko habari za Wizara yeyote ile katika Serikali ya Awamu ya Nne. Babu wa Loliondo si mchezo bwana, ana ‘maafisa habari wake’ wanaowafunika hata maafisa habari wa Wizara za Serikali.

Na katika mzaha huu wa mambo ya msingi kitaifa, tuna maelfu kwa maelfu ya Watanzania wanaotaabika na hata baadhi kufa kwa kuamini kuwa Loliondo kuna tiba, na iko Loliondo tu! Leo, kuna Watanzania walioweka rehani mavuno yao ya mwaka mzima ili wapate nauli ya kwenda kwa Babu. Si wameambiwa, kuwa hata mawaziri wanapanga foleni ya kwenda kupata kikombe cha Babu!
Na wakishapata kikombe wanapiga picha ya ukumbusho, au labda ya kisiasa. Asubuhi yake ’maafisa habari’ wa Babu wameshatundika picha ya waziri ukurasa wa kwanza gazetini! Jimboni kwa mheshimiwa wapiga kura wake watamwona au kusikia kuwa Mheshimiwa naye anaumwa kama sisi, na amepata kikombe cha Babu!

Kikombe cha Babu ni abrakadabra, nilipata kuandika hilo. Na Watanzania, baadhi, kwa hiyari yetu, tumekubali kujifanya, wajinga na hivyo kuwapumbaza wengi wengine. Kwanini? Tulitafute jibu kwa kufikiri kwa bidii.

Hebu jiulize; wakati Shirika la Afya Duniani (WHO), ifikapo Juni mwaka huu, litaadhimisha miaka 30 ya mapambano dhidi ya ukimwi, je, Tanzania, kama nchi, tutakuwa na banda la maonyesho likielezea ugunduzi wa tiba ya ukimwi iliyotokana na ndoto ya Babu?!

Labda ndio maana, magazeti yetu ya lugha ya Kiingereza hayafanyi sana promosheni ya tiba ya Babu. Maana, kama habari za Babu zingepewa uzito kama ilivyo kwenye magazeti yetu ya lugha ya Kiswahili, basi, wana jumuiya ya Kimataifa, wakiwamo wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, huenda wangeshindwa kuamini wanachokisoma.

Maana, wawakilishi wa mashirika kama PSI na FHI yenye miradi ya kupambana na ukimwi nchini na mengineyo wangejiuliza; nini hasa wanachokifanya katika nchi yetu. Na pengine wameshatafsiriwa tunachooandika juu ya Babu kwa Kiswahili chetu!

Si ajabu basi, Ubalozi wa Marekani umekuja na tamko lake Mei 5 mwaka huu. Wamarekani hawa, kwa kuwaonea huruma Watanzania, wameshauri watu wanaotumia tiba mbadala wasiache kutumia dawa walizopewa na madakatri na vile vile waendelee kujikinga na maambukizi.

Na wakaweka msisitizo kuwa, kuacha kutumia dawa hizo za madaktari watalaamu kunafanya dawa hizo zinapotumiwa tena kushindwa kufanya kazi ipasavyo (drug resistance). Na ajabu ya habari ya tamko lile la Wamarekani ilichapishwa katika gazeti moja tu kwa lugha ya Kiingereza - The Citizen, jina la gazeti hilo lina maana ya Mwananchi; ingawa wananchi wengi hawakupata habari hiyo kwa lugha yao!

Kwa hakika, hatuhitaji kuambiwa na Wamarekani juu ya ukweli huu na wajibu wetu. Huu ni wakati kwa wizara inayohusika kufanya jitihada za dhati kutoa tamko litakaloweka bayana kuwa tiba inayodaiwa kutolewa na Babu bado haijathibitika kitalaamu kama inaponya maradhi sugu kama vile ukimwi, kansa na kisukari.

Wakati utafiti huo ukiendelea, umma ukumbushwe kuwa, dawa zinazotambulika kitalaamu kwa sasa ni zile zinazotolewa na madaktari wetu watalaamu. Kwamba wanaokwenda kwa Babu wana ruhusa ya kufanya hivyo, lakini, kikombe cha Babu kinaweza kunywewa pamoja na dawa za hospitalini.
Tufanye hivyo sasa, na ujumbe huo usambazwe kwa nguvu zote na maafisa wa habari wa wizara husika. Ndio, maofisa habari wa Wizara ya Afya nao washindane na ‘maafisa habari’ wa kujitolea wa Babu wa Loliondo!

Watanzania tunapita kwenye kipindi kigumu sana. Na huu ni wakati wa kutafakari kwa kina. Na nimepata kumwuliza jamaa yangu swali hili; mwanadamu unafanyaje unapoamka na kukuta dunia unayoishi ardhi yake imeanza kumegeka na kuchotwa na bahari? Naye akanijibu; ” Huo ndio utakuwa mwisho wa dunia!” Aliyenijibu alikuwa amechoka kufikiri. Nilidhani angetamka kuwa, angeanza kujifunza kuogelea. Maana, kwa kuogelea majini angeweza kukutana na kisiwa, au nchi kavu.

Wanadamu tumejaliwa akili ili tuweze kufikiri. Na kufikiri ndio njia mojawapo ya kuiteka kweli. Kufikiri kunahamisha milima na hata kuiweka kando kuruhusu mwanga upite. Inakuwaje basi mwanadamu anapoacha kufikiri?

Haya ya kwa ‘Babu wa Loliondo’ ni kielelezo cha Watanzania kuamua kuacha kufikiri. Kuna umma uliojifunika vilemba vya ujinga. Umma uko gizani, unahitaji mwanga.

Yumkini wakatokea Watanzania wenzetu wakaoteshwa na Mungu juu ya dawa za tiba kwa mwanadamu. Na hapo wakaingiza suala la imani. Lakini, jambo hilo halituzuii wanadamu kuhoji na kudadisi. Ndio, kuuliza maswali. Na kwa Serikali, jambo hilo haliizuii kufuata taratibu zake za kawaida ikiwamo kufanyia utafiti jambo hilo na kutoa msimamo wa kiserikali.

Hata kama Watanzania watakuwa na uhuru wa kwenda kwenye tiba za imani, lakini msimamo wa Serikali uwepo. Na kwa wengi utabaki kuwa ndio mwongozo; maana, watakuwa wameufanyia utafiti. Nahitimisha.

No comments:

Post a Comment