Pages

Monday, May 23, 2011

Kiama Hakijatokea, Mchungaji Aingia Mitini

Kiama kilitakiwa kiwe jana saa 12jioni lakini hakikutokea kama kilivyotabiriwa na mchungaji wa nchini Marekani ambaye alitumia pesa nyingi sana kuwaonya watu kwa miezi kadhaa kuwa kiama kingetokea jana mei 21 kwenye majira ya saa12jioni.

Wafuasi na waumini wa Mchungaji Harold Camping wamebaki hawajui la kufanya baada ya kuhubiriwa kwa miezi mingi kuwa kiama kingetokea jana jumamosi saa 12 jioni.
Mwanaume mmoja na familia yake walisafiri kilomita 4830 toka Maryland hadi California mbele ya ofisi ya radio ya mchungaji Camping na kusubiri kupaishwa mbinguni kwenda kuonana na Yesu kama walivyohubiriwa na mchungaji huyo.

Kiama hakikutokea kama walivyotarajia, walibaki kwenye gari lao masaa yakikatika na sasa wakiwa na kazi nyingine ya kusafiri kilomita zingine 4830 kurudi nyumbani kwao.

Mwanaume mwingine mwenye umri wa miaka 60, Robert Fitzpatrick kwa kuamini kuwa mwisho wa dunia umefika na kwa kuamini mafundisho ya mchungaji Camping, alitumia dola $140,000 toka kwenye akiba yake ili kuchapisha mabango na vipeperushi vya kuwaonya watu kuwa mwisho wa dunia ni mei 21.

Akiwa amesimama kwenye viwanja vya Times Square jijini New York akiwa amezungukwa na wapita njia, Fitzpatrick, alikuwa akisoma mistari ya biblia huku akigawa vipeperushi akiwataka watu wajiandae kwa kiama ambacho kingeanza saa 12 jioni ya mei 21.

Masaa yalikatika na kiama hakikutokea, Fitzpatrick kwa mshangao alisema "Siwezi kukwambia ninavyojihisi hivi sasa, saa 12 imekuja na kuondoka haraka haraka, sielewi kwanini hakuna kitu chochote kilichotokea".

Mchungaji Camping mwenyewe hajaonekana tena na amekaa kimya na hadi sasa hajasema chochote kwanini kiama hakikutokea kama alivyotabiri na kuwahabarisha watu kwa miezi kadhaa kabla.

Hata hivyo bado waumini wengine wa mchungaji Camping wanaendelea kumuamini mchungaji huyo wakisema kuwa kuchelewa kutokea kwa kiama ni mtihani mwingine toka kwa Mungu juu ya imani zao.

Wakati huo huo watu wasioamini kuwepo kwa Mungu wameendelea kujirusha wakihoji hicho kiama kiko wapi?.

2 comments:

  1. Dah jamaa kanialibia sana mambo yangu kwani ile siku ya jumamosi aliosema itakua kiama nikatumia pesa zangu zoooooote nashanga hakuna kiama wala nini.

    ReplyDelete
  2. pole mwana ucjali tafuta tena

    ReplyDelete