Pages

Wednesday, May 11, 2011

CHADEMA, CCM SASA NI KULIPUANA

Gasper Andrew, Singida na Boniface Meena, Nkasi
VITA ya maneno baina ya vyama vikubwa vya siasa nchini CCM na Chadema, imezidi kushika kasi kwa vyama hivyo kurushiana tuhuma katika mikutano ya hadhara inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.CCM kinawaita Chadema wanafiki na Chadema kinaendelea kudai kuwa chama hicho tawala ndicho kinachoisababishia nchi umasikini.

Jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alidai kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ni mnafiki kwa kula matapishi yake anapodai kuwa chama tawala kinafuja mali ya umma huku naye (Dk Slaa) akiwa katika mwelekeo huohuo.

Alidai kuwa Dk Slaa ameingia mikataba ya kukishinikiza chama chake kimlipe Sh7.5 milioni kila mwezi wakati alipokuwa mbunge alikuwa akiilalamikia serikali kwamba inawabebesha wananchi mzigo mkubwa kwa kuwalipa wabunge kila mmoja Sh milioni sita. Nape alisema hayo jana alipokuwa akizungumza kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katikia Kituo Kikuu cha mabasi cha zamani mjini Singida.

Alisema anazo nyaraka halali za chama hicho zinazoonyesha kwamba baada ya Dk Slaa kuukosa urais, sasa amekigeukia chama chake na kuanza kukishinikiza kimlipe mshahara mkubwa kuliko aliokuwa akiupata alipokuwa mbunge.Nape alisema madai kwamba Dk Slaa haombi alipwe si ya kweli akidai kwamba ndiye anayeshiniza kulipwa kiasi hicho kwa vile ameachishwa ubunge na ameukosa urais.

"Anashangaza sana bungeni alikuwa akipanua mdomo hadi mwisho kupotosha jamii kuwa wabunge pamoja na posho, mishahara na marupurupu mengine, wanalipwa shilingi milioni sita kiasi ambacho alidai kuwa kinawaumiza wananchi. Kwa hiyo ndiyo tuseme Sh7.5 milioni ni kiwango ambacho hakitawaumiza wanachama wa Chadema na walipa kodi wengine," alihoji Nape huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria.

 Katibu huyo alisema kwa kitendo chake hicho cha kushinikiza alipwe kila mwezi mamilioni hayo, anapaswa kuwaomba radhi Watanzania kwa kuwadanganya alipokuwa bungeni kuwa Sh milioni sita ni mshahara mkubwa mno.
 Aidha, alisema kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe naye aliwahi kutoa msaada wa Fuso (malori aina ya Mitsubishi Fuso) tatu ili zikisaidie chama hicho katika shughuli mbalimbali za ustawi wake lakini sasa anakidai Sh500 milioni za ununuzi.

Madai ya Nape kuhusu mshahara wa Dk Slaa yaliwahi kutolewa maelezo na Chadema ambacho kilisema kilifikia uamuzi wa kumlipa, Dk Slaa mshahara na maslahi yanayolingana na anayopata mbunge kwa sababu ndicho kilichomshawishi aache kugombea ubunge katika Jimbo la Karatu mkoani Arusha, ambako alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda na kumtaka agombee nafasi ya urais ambayo mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alishinda.

Kilisema uamuzi huo ulifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na vikao vikuu vya chama hicho, kama vile Kamati Kuu, kuidhinisha malipo hayo.Kuhusu malori Chaadema kilisema kiliamua kufanya mkakakti wa kununua magari matatu ambayo Mbowe aliyanunua na kuyatoa kwa muda ili yakisaidie kwenye kampeni.

Mbowe: CCM wanajipa mamlaka ya uungu mtu
Wakati Nape akisema hayo Mbowe amesema viongozi wa Serikali ya CCM wamelewa madaraka na kujivika mamlaka ya uungu watu na kusahau kuwatumikia Watanzania: "viongozi wa nchi hii, wanajipa mamlaka ya umungu-mtu na wananchi wanawaogopa."
Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa mji mdogo wa Namanyere, Wilaya ya Nkasi, Rukwa, ikiwa ni sehemu ya operesheni ya Chadema ya kuishinikiza serikali kusikiliza kilio cha wananchi.

Alitoa mfano akisema, iwapo wananchi wa Wilaya ya Nkasi watajengewa barabara, wajue kuwa hiyo ni haki yao na pia wana haki ya kuiuliza serikali sababu za kuchelewa kujengewa kwa miaka 50 ya uhuru.
Alisema katika mkoa kama wa Kilimanjaro, wamekuwa wakijengewa barabara za lami kwa kadri inavyohitajika, tofauti na Mikoa kama ya Rukwa, Iringa, Mbeya na Ruvuma ambayo imeachwa nyuma kimaendeleo, licha ya kuzalisha chakula kinachohifadhiwa katika Hifadhi ya Chakula ya Taifa.

Kutokana na hali hiyo, alisema iwapo wananchi wa Mkoa wa Rukwa hawatapiga kelele kudai maendeleo, kamwe hawezi kushuka Malaika Gabriel kuwapigia kelele."Kwa hiyo ndugu zangu, si kila kitu ni cha kupongeza, muwatume wabunge wenu wakapige kelele," alisema Mbowe.Alisema tangu Chadema ianze kupiga kelele Rukwa, imefanikiwa kutoa Mbunge mmoja tu, Said Arfi na barabara zikianza kutengenezwa.

Mbowe alisema serikali imeshindwa kusimamia reli ya kati kiasi ambacho wananchi wanaotaka kusafiri kulazimika kutumia gharama kubwa kupata usafiri wa ndege.Alisema kuwa baadhi ya wabunge kutumia muda mwingi bungeni kuishukuru serikali katika mambo ambayo ni wajibu wake kuwatekelezea wananchi.Alisema wabunge hao wamekuwa wakifanya hivyo, huku wakijua wazi kuwa ni kinyume na jukumu la mbunge, ambalo ni kuisimamia serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.
"Kitendo cha kuishukuru serikali, ndicho kinatuchelewesha kupata maendeleo. Wananchi wanaiomba serikali, wabunge wanaishukuru..." alisema.Alisema vitendo hivyo vimechangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya viongozi wa serikali nchini kujiona kuwa ni miungu kwa sababu wanatukuzwa.

Waliopewa siku 90 CCM wataaibika karibuni
Katika hatua nyingine, Nape alisema kuwa viongozi walioombwa na chama wajipime wenyewe na kuchukua uamuzi wa kuachia nyadhifa zao mapema kutokana na kutuhumiwa na wananchi juu ya tabia zao za kifisadi, kwamba sasa siku zao za kuja kuaibishwa, zinahesabika.

"Watu sasa wameanza kusema kuwa Nape hana nguvu tena za kupambana na ufisadi nchini, nawaambia kuwa si kweli. Sijalala wala sijaishiwa nguvu za kutokomeza ufisadi. Hawa wanaotuhumiwa kwa ufisadi wanakipa chama machungu na kuanza kukikosesha imani kwa wananchi, wanapaswa kujiondoa wenyewe na wasisubiri kuja kuapishwa kwa kufukuzwa kwa nguvu," alisema.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Chilingati aliwataka viongozi na wanachama wa chama hicho ngazi ya wilaya na mikoa kusaidia kukirudisha kwenye misingi yake ya awali ili wananchi waendelee kukiamini.
Chiligati ambaye pia ni Mbunge wa Manyoni Mashariki, alitoa wito huo juzi alipozungumza na wananchi wa Kata ya Ikungi, Singida.
Alisema vikao vya Halmashauri Kuu vilivyofanyika hivi karibuni mjini Dodoma, vilibaini kuwa CCM imefika mahali pabaya kwa kuanza kuacha misingi yake na kusababisha baadhi ya wanachama wake na wananchi kwa ujumla, kuanza kukosa imani nacho.

No comments:

Post a Comment