Pages

Monday, January 9, 2012

Nigeria yazizima kwa mgomo wa mafuta

Mgomo wa nchi nzima umeitishwa nchini Nigeria kupinga kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta ambayo imesababisha shughuli za nchi hiyo kusimama.
Maduka mengi, ofisi, shule na vituo vya mafuta nchini humo vimefungwa katika siku ya kwanza na mgomo ulioitishwa na vyama vya wafanyakazi.
Maelfu ya watu wamekusanyika mjini Lagos na miji mingine kupinga kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta ambayo imesababisha kupanda mara dufu kwa bei ya mafuta na gharama za usafiri.
Rais Goodluck Jonathan alisema ruzuku hiyo ina athari za kiuchumi.

Risasi

Mitaa ya Lagos ambayo kawaida huwa imejaa watu imekuwa kimya, isipokuwa kwa doria za polisi na watu wanaoelekea kwenye mikutano ya hadhara.
Maelfu kadhaa ya watu wamekusanyika katika eneo la wazi la Gani Fewehinmi mjini humo na wengine wengi wanaendelea kuwasili, anasema mwandishi wa BBC Mark Lobel aliyepo nchini Nigeria.
Nigeria
Wananchi wa Nigeria wamekasirishwa na kuondolewa kwa ruzuku
Kumekuwa na taarifa kuwa mwandamanaji mmoja amepigwa risasi na kufa mjini Lagos.
Katika mji wa Kano kaskazini mwa nchi hiyo, polisi wamefyatua mabomu ya kutoa machozi na kupiga risasi hewani kutawanya maelfu ya waandamanaji waliokuwa wakikusanyika katika ofisi ya gavana. Watu 12 walijeruhiwa, alisema mwandishi wa BBC Idhaa ya Kihausa Yusuf Ibrahim mjini humo.
Mjini Abuja, vizuizi vimewekwa na kusababisha uwanja wa ndege kufungwa, na hivyo kuzuia ndege kupaa na kutua, anasema Ibrahim Shehu Adamu wa BBC akiwa katika mji huo mkuu.
"Lazima tutazame manufaa ya taifa, hata iwe ngumu kiasi gani, kwani maumivu ya sasa hayawezi kufananishwa na manufaa ya kesho"
Rais Goodluck Jonathan
Pia mjini Abuja, kuna taarifa kuwa vijana waliokuwa wamepiga kambi katika eneo la wazi la Eagle waliondolewa usiku na polisi kwa kutumia mabomu ya machozi.
Katika mji wa kaskazini wa Kaduna, kuna polisi wengi na mitaa iko kimya, huku maduka yote yakiwa yamefungwa, amesema mwandishi wa BBC Abdullahi Kaura Abubakar.
Shughuli pia zimesimama katika mji mkubwa wa Ilorin uliopo kusini magharibi mwa Nigeria, mtu mmoja anayefanya biashara sokoni ameiambia BBC. Alisema aliwataka wafanyakazi wake kusalia nyumbani baada ya kuona magari mawili yakifanyiwa uhalifu.

Ongezeko

Kumekuwa na maandamano yenye hamaki tangu kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta tarehe mosi ya Januari na gharama za mafuta, usafiri na nyinginezo kupanda pia.
Kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta kumewakasirisha wananchi wengi wa Nigeria, ambao waliona ndio faida pekee wanayopata kutokana na utajiri mkubwa wa mafuta wa nchi hiyo.
Maandamano
Mitaa haina watu
Wananchi wengi wa Nigeria ambayo idadi yao ni milioni 160 wanaishi chini ya dola mbili kwa siku, kwa hivyo ongezeko la bei limewaathiri sana.
"Kwa ongezeko hili, gharama za usafiri zimepanda na hii imeathiri gharama za chakula na mahitaji muhimu, kama vile kodi ya nyumba, ada za shule na gharama za hospitali," alisema Chris Uyot, msemaji wa chama cha Labour, moja ya waandaaji wa maandamano hayo.
Maandamano kama hayo mwaka 2003 nusura yasimamishe kabisa shughuli nchini Nigeria. Hali hiyo ilipungua baada ya serikali kukubali kupunguza kiasi cha ruzuku, badala ya kuondoa kabisa.
Wakati mgomo huo ukitarajiwa kuathiri wafanyakazi wa mafuta pia, vyanzo kutoka idara ya viwanda vinasema mgomo huo hautarajiwi kuathiri mauzo ya mafuta yasiyosafishwa nje ya nchi, limeripoti shirika la habari la Reuters.
Mafuta
Ukosefu wa miundombinu ya usafishaji unasababisha gharama kupanda
Licha yakuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta, Nigeria haijawekeza katika kusafisha mafuta, kwa hiyo ni lazima iagize mafuta ya petroli kutoka nje.
Kwa ruzuku kutolewa, mafuta huuzwa kwa bei rahisi nchini Nigeria kuliko nchi majirani, kwa hiyo mafuta mengi yalikuwa yakiuza nje ya nchi kwa njia za ulanguzi.
Wabunge wamemtaka Rais Goodluck Jonathan kufikiria upya jambo hilo, lakini alisema ruzuku hiyo ina athari za kisiasa.
Rais alitoa hotuba kupitia televisheni siku ya Jumamosi kutetea kuondolewa kwa ruzuku na hatua nyingine za serikali za kubana matumizi.
"Lazima tutazame manufaa ya taifa, hata iwe ngumu kiasi gani, kwani maumivu ya sasa hayawezi kufananishwa na manufaa ya kesho."
Jonathan
Rais Jonathan ametetea kuondoa ruzuku
Mabadiliko katika sekta ya petroli, alisisitiza, ndio njia nzuri ya kupambana na ufisadi na kuhakikisha uchumi unakua.
"Ukweli ni kwamba, sote tunakabiliwa na mambo mawili... ama tuendelee na hili na uchumi wetu uendelee au tuendelee kutoa ruzuku ambayo itateteresha uchumi wetu na tukabiliane na matatizo makubwa."
Alisema maafisa wa ngazi za juu, kuanzia mwaka huu, watakatwa mishahara yao kwa asilimia 25, na safari za nje ya nchi pia zitapunguzwa.
Serikali imesema itatumia dola bilioni 8 ambazo zitatokana na kubana matumizi, katika kuweka hali bora katika sekta ya afya, elimu na tatizo sugu la umeme nchini humo.
Hata hivyo, wananchi wengi wa Nigeria wanahofu kuwa huenda fedha hizo zikaishia katika mifuko ya mafisadi.
Mwezi uliopita, mkuu wa shirika la fedha duniani IMF Christine Lagarde alisifu jitihada za Rais Jonathan za kufanyia mabadiliko uchumi, lakini alionya kuwa nchi hiyo haina budi kutotegemea mapato ya mauzo ya mafuta nje.
 BBC

No comments:

Post a Comment