Pages

Saturday, January 14, 2012

Gogo Mzome; nimeona mengi chumba cha maiti kwa miaka 20

 Gogo Mzome akiwa kazini
Na Florence Majani
WASWAHILI husema kazi ni kazi, bora mkono uende kinywani. Lakini, zipo kazi ambazo wengi katika jamii huzikimbia na wakati mwingine kuzipa majina mengi.hili si jina geni kwa wakazi wa Temeke,maeneo ya chan`gombe Usalama, evereth, Mwembeyanga, Mtaa Yombo nk
Lakini, kuna dhana imejengeka katika jamii kuwa kufanya kazi katika chumba cha kuhifadhia maiti, lazima uwe kichaa au pengine mtu ambaye umejitoa mhanga kweli.
Ni nini ukweli kuhusu maisha katika chumba cha maiti na nini majukumu ya mhudumu wa chumba kile?
Safari ya Mwananchi katika chumba hicho katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)  jijini Dar es Salaam inaanza!
Jokofu  la kwanza linapofunguliwa inaonekana miili mitatu. Ule  wa kwanza ni wa mfungwa, alitambulika kutokana na sare zake. Huyu  alikuwa na jeraha kubwa usoni …  huku ngozi yake ya  kichwa ikining’inia.
Mwingine wa pili ulikuwa umefunikwa kwa shuka gubigubi, lakini shuka hilo lilikuwa limejaa damu usoni na wa tatu ulikuwa kawaida.
Kulia kwangu kilikuwapo chumba kingine kikubwa. Hicho kilikuwa na wanaume wanne walioonekana kutingwa na kazi zao za kila siku. Kila mmoja alikuwa  mbele ya meza ya chuma akiushughulikia mwili wa marehemu.  Miili  yote ilikuwa  ni  ya wanaume. Walikuwa wakisafishwa tayari kwa maziko.
Mtu anayenitembeza katika milki hii ya kutisha si mwingine bali amejitambulisha kuwa  Gogo Mzome Abdallah. Yeye ni mhudumu mkuu katika chumba cha kuhifadhi maiti (mortuary) cha MNH.
Kama wewe ni mfiwa na umekwenda kuchukua mwili wa nduguyo na kuwakuta wahudumu hawa wakipiga soga- huku wakicheka - wakiwa ndani ya sare zao za suti zenye rangi ya bluu bahari, utadhani hawana huruma, wala hawayajui machungu ya kufiwa. Lakini, yakupasa ukumbuke kuwa … wapo kazini!
Novemba 1991 ndicho kipindi ambacho Mzome aliajiriwa katika kitengo hiki cha uhifadhi miili ya marehemu hapo MNH.
Wakati huo, Mzome anasema alikuwa na  umri wa miaka 34. Anasema, hakulazimishwa, wala hakwenda kwa kubahatisha bali alifika mwenyewe mahali pale (Muhimbili) na kuomba kazi.
Hawezi kusahau siku yake ya kwanza kazini:  “Nilipoanza kuonyeshwa maeneo yangu ya kufanya kazi, ikiwamo kazi nitakazokuwa nafanya, nilinyong’onyea. Miguu yangu iliishiwa nguvu,” anaanza Mzome katika simulizi yake.
Anasema alijisikia  hali ya ukiwa kwa saa tano baada ya kuanza kazi, lakini baada ya hapo aliyaelewa majukumu yaliyompeleka mahali pale na alianza kuchapa kazi.
Kazi  kubwa  ya wahudumu wa maiti ni nini?
Mzome anajibu  kuwa, kazi kubwa ni kuipokea miili ya marehemu na kisha kuihifadhi. Miili hiyo inapohifadhiwa katika majokofu huwekwa jina na namba kwa ajili ya kuitambua.
Huduma nyingine tunazozifanya ni pamoja na kuosha miili  hiyo endapo wafiwa watataka huduma hiyo, ambayo hulipiwa Sh25, 000, kuwachoma dawa ili wasiharibike na kuwasitiri
Huduma nyingine ni kuweka rekodi ya kila mwili wa marehemu unaofika hapo.
Anaongeza  kuwa, wafanyakazi wote wa kitengo hicho hupewa mafunzo na madakatari wa pathologia ambapo  pamoja na mambo mengine huelekezwa jinsi ya kumdunga marehemu dawa maalum(formaline) ya kuzuia mwili usiharibike.
Wakati mwingine tunapasua maiti ili kuweka dawa kwenye miili inayosafirishwa nje ya nchi ili isiharibike.
Hali kadhalika sisi husaidiana na madaktari kufanyia uchunguzi mwili wa marehemu (post mortem), anasema.
Mauza uza ndani ya chumba cha maiti
Wengi wetu tumekuwa tukisikia dhana au hadithi mbalimbali kuwa, yapo matukio ya ajabu  katika vyumba vya kuhifadhi maiti.   Kwa mfano, maiti kufufuka, kusikia maiti zikisemezana katika majokofu na mengine mengi.
Mzome anakanusha uvumi huo na kusema: Katika miaka 20 niliyofanya kazi  humu sijawahi kuona  vitu kama hivyo. Huo ni uvumi na woga tu, hata ukiwa nyumbani ukiwa mwoga utahisi mauzauza,
Anakanusha dhana nyingine kuwa,  wahudumu wa chumba cha maiti hawawezi kufanya kazi mpaka walewe pombe au wavute sigara au bangi , na kusema kuwa, yeye hafanyi kazi akiwa amelewa hata siku moja
Hata hivyo, Mzome anakiri kuwa, wakati mwingine hukumbwa na hofu  na simanzi kwani baadhi ya miili huletwa ikiwa  imeharibika vibaya au imeoza.
Hii kazi wakati mwingine haina raha bwana! Hakuna picha ya kutisha kama maiti iliyooza, au iliyoungua. Lakini, kwa sababu tupo kazini, sisi huzihudumia maiti hizo vile inavyotakiwa, anasisitiza Mzome.

Changamoto kuu
Gogo Mzome anasema kuwa, changamoto kubwa ambayo amekutana nayo katika miaka yake 20 ya kufanya kazi katika chumba cha kuhifadhi maiti ni kuwahudumia wafiwa.
Mara nyingi wafiwa huwa katika hali ya  kuchanganyikiwa. Hawa wanataka uhuzunike nao, lakini utalia mara ngapi kwa siku?  Yakupasa kuwahudumia kwa  hekima ili wasijisikie vibaya, anasema.
Mzome anaikumbuka siku alipokuja mwanamume mmoja kutafuta mwili wa marehemu, lakini hakuwa akitoa taarifa kamili.
Alipoambiwa akahakikishe majina ya marehemu  ndipo arudi kuutafuta mwili wa nduguye, alilipuka kwa hasira na kumwambia Mzome Ndiyo maana kazi yenu ni  kucheza na maiti tu.Mzome anaizungumzia kazi yake na kusema, hakuna kazi inayohitaji umakini kama ya kuhudumia maiti.
Ukifanya kazi hii unatakiwa uwe makini mno! Maiti hasemi, kama ndugu wasipotoa taarifa kamili za marehemu wao au wakawa waoga kumtambua, unaweza ukafanyika uzembe wa hali ya juu, anasema.
Analikumbuka tukio moja ambapo wafiwa walikuwa waoga kuutambua vyema mwili wa ndugu yao na mhudumu hakuwa makini,  hivyo wakachukua mwili  wa marehemu mwingine.
Lakini tuliwawahi kabla hawajaaga. Tulipowaeleza ilibidi waahirishe kila kitu na kuanza upya kumhudumia marehemu wao halisi, anasema.

Mzome: Ninawapenda maiti
Katika kazi yake Mzome anasema amejifunza kitu kimoja. Nacho ni upendo. Anasema, binadamu wote ni marehemu watarajiwa hivyo yatupasa tuishi kwa upendo.
Mimi ninajifunza mengi hapa, leo unazungumza na mtu, anacheka, pengine ana mipango  ya kufunga ndoa, lakini kesho analetwa hapa tayari ni marehemu.
Kwa hiyo, nawapenda  na kuwahudumia maiti  kwa upendo, kwani hata mimi kesho nitakuwa marehemu na sijui atakayenihudumia,aAnasema Mzome akionyesha kuwa na hisia kali.
Anasema, kwa kuwa maiti hazungumzi basi isiwe kigezo cha kumhudumia vibaya.
Siku asiyoweza kusahau
Mzome ambaye ni baba wa watoto wanne na mke anasema, hataweza kuyasahau matukio mawili katika kipindi chake chote cha ajira hapo Muhimbili.  La kwanza ni siku kilipoletwa kichwa cha mtoto Salome.
Sitalisahau tukio la kijana Ramadhan ambaye alikutwa maeneo ya Muhimbili akitafuna kichwa cha mtoto Salome.
Basi, tuliletewa hapa kichwa, na baadaye kiwiliwili. Kichwa cha mtoto yule kilikuwa kimesukwa vizuri maskini! Liliniuma mno tukio hilo, anaeleza.
Anaongeza na kusema, tukio la pili ni la ajali ya  basi huko Yombo Dovya. Marehemu walikuwa wanakuja vipandevipande, wengine ubongo katika mfuko wa rambo, yaani vilikuja viungo na si miili.
 Hali kadhalika anakumbuka siku ya kwanza kuingia zamu usiku ambapo alihisi analala na maiti na hakufumba jicho, mpaka kulipopambazuka.

Alificha siri kwa mwaka mzima.
Alipoajriwa katika kitengo hiki cha kuhudumia maiti, hakutaka watu wafahamu wapi anapofanyia kazi. Awali, aliona ni kazi ya aibu. Hakuwaficha marafiki tu, bali  hata mkewe.
Kila mara mke wangu aliponiuliza  nafanya kazi wapi nilimwambia kwa kifupi: Muhimbili. Lakini, baada ya kupita mwaka mmoja nikasema potelea mbali, na nikampasulia jipu, Anasema huku akiangua kicheko kikubwa.
Gogo Mzome  ni baba mtu mzima mwenye umri wa miaka 55 sasa, ana uzoefu wa hali ya juu katika kitengo cha kuhifadhi miili ya marehemu. Anatoa wito kwa Watanzania kuachana na dhana kuwa kazi hii ni ya fedheha.
Hii ni kazi kama kazi nyingine. Nisipofanya mimi atafanya nani?” anauliza Mzome.
Naye  Mkuu wa Kitengo cha Kuhifadhi Maiti MNH, Dk Innocent Mosha anasema pamoja na  moyo wa ujasiri, kazi hiyo inahitaji uzoefu na umakini wa hali ya juu.
Ukifanya uzembe kidogo tu unajitia matatani. Kwa mfano, maiti za watoto wachanga mara nyingi huchanganya watu, utakuta wote wawili wana majina kwa mfano, Mwajuma Saleh, halafu wanafanana, basi hapo utata mzito hutokea, anasema Dk Mosha.
Dk Mosha anaongeza na kusema, wahudumu wa chumba cha maiti hutumika pia kufanya uchunguzi katika miili ya marehemu wakishirikiana na madaktari.
Hali kadhalika anatoa wito kwa Watanzania kujenga tabia ya kuifanyia miili ya marehemu uchunguzi (postmortem)kabla ya kuzika.  Nia ni kujifunza na kupata ukweli wa chanzo cha kifo badala ya kuhisi.

No comments:

Post a Comment