Pages

Monday, January 2, 2012

NAULI-MAGUFULI FUTA KAULI YAKO WAOMBE RADHI WATANZANIA



Ndugu zangu,
Waziri wa Ujenzi amenukuliwa na Watangazaji wa habari akitamka;  "Na atakayeshindwa kulipa nauli mpya Dar- Kigamboni na apige mbizi au azunguke Kongowe"- John Magufuli.

Ndugu zangu,
Siamini kama maneno haya yanatoka kwenye kinywa cha Waziri Mwandamizi mwenye dhamana ya kuwatumika WaTanzania. Na kwa vile ni kweli yametamkwa hayo na Magufuli, tena hadharani, basi, nionavyo, John Magufuli ana mawili ya kufanya; ama afute kauli yake hiyo sambamba na kuwaomba radhi WaTanzania hadharani, au apime mwenyewe kama bado anastahili kuongoza Wizara akiwa na dhamana ya kuwatumikia WaTanzania na huku akitegemea atandelea kuheshimiwa na Watanzania ambao kimsingi wamekerwa sana na kauli hiyo yenye dharau na kebehi kwa WaTanzania.

Magufuli huenda amekaa muda mrefu Serikalini kiasi cha kupoteza mguso na hali halisi za Watanzania. Kauli aliyotumia ni kelelezo cha kupoteza mguso huo na hali halis inayowakabili Watanzania walio wengi miongoni mwao ni wakazi wa Kigamboni.

Hivi, Magufuli huyu anaposema atakayeshindwa kulipa nauli mpya apige mbizi au azunguke Kongowe  hajui kwamba kuna WaTanzania ambao shilingi mia tatu ni kubwa sana kwao. Kwamba wangekuwa tayari kulipa hiyo nauli lakini ukweli wengi wana hali ngumu kimaisha.

Na je, unafanyaje na Mtanzania anayempeleka mgonjwa wake kwa kutumia kivuko na hana hiyo mia tatu? Naye apige mbizi majini au azunguke kupitia Kongowe kwa miguu, maana hata nauli ya mia tatu ya Daladala hana?  Ndio, wazee na wagonjwa nao wapige mbizi majini kwa kukosa nauli ya mia tatu? Na wasiojua kuogelea?

Hapana, inasikitisha. John Magufuli hawezi kujitetea kwa kauli yake hiyo. Aifute na atuombe radhi WaTanzania, basi. Na kimsingi suala hili la nauli za kivuko liangaliwe upya. Tujifunze kutoka kwa jirani zetu wa Kenya. Pale kivuko cha Likoni, Mombasa, ambacho ni sawa na cha Kigamboni, abiria wanavuka bure. Kinachotozwa kodi ya kuvuka ni vyombo vya motot u ikiwamo magari na pikipiki. Hivyo basi, gharama za kuendeshea kivuko zinatokana na kodi za vyombo vya moto.

Na Magufuli atambue kuwa kuna waliomtangulia katika kutoa kauli za ‘ kuchemsha’ na zilizowagharimu kisiasa.
John Malecela ni mmoja wa watu hao. Kuna wakati,  akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi.  Katikati ya kilio cha watumiaji wa njia ya reli ya kati (TRC)  juu ya huduma mbaya za Shirika hilo la Reli miaka ile ya 80,  Bw. John Malecela alipata kukaririwa akitamka kuwa hakukuwa na tatizo la huduma mbaya na kwamba wenye kufikiri hivyo, “ They can go to hell!”- kwamba wanaweza kwenda kuzimu.

Katika sanaa ya mawasiliano, tunaamini, kuwa sentesi moja inayotamkwa na mwanasiasa, yaweza kumjenga au kumbomoa kabisa kisiasa. Kwa John Malecela, kauli yake ile ataishi asiiahau, maana, pamoja na kuwa tulikuwa katika mfumo wa chama kimoja, redio moja ya taifa na magazeti matatu, bado wananchi waliweza kufikisha shutuma zao kwa Malecela juu ya kauli yake ile.

Na kilichotokea katika uchaguzi mkuu uliofuata wa mwaka 1985 ilikuwa ni kwa wapiga kura wa Dodoma mjini kushindilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la kisiasa la John Malecela. Walifanya hivyo  kwa niaba ya Watanzania wengine na hususan watumiaji wa reli ya kati. Malecela aliangushwa vibaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Hakupata ubunge na hivyo hakuweza kuwa Waziri.

Tukirudi Kigamboni, hivi, ni kwanini umtoze nauli mkazi wa Kigamboni wakati kila Mtanzania ana haki ya kuishi mahali popote katika nchi hii.
Sasa basi, kama  mtu na familia yake wameamua kuishi Kigamboni kwanini watozwe nauli kwa kuvuka kwenda na kurudi katikati ya Jiji kwa shughuli zao za kila siku na kama hawatumii vyombo vya moto? Mbona wanaoishi Oysterbay na Masaki akiwamo John Magufuli hawatozwi kodi ya kuvuka daraja la Sarenda?

Tunadhani  ni jukumu la Serikali na Wizara ya Magufuli kuhakikisha kunajengwa daraja la Kigamboni kuwasaidia wakazi wa eneo hilo. Kama daraja hakuna ni jukumu la Serikali na wizara ya Magufuli kuhakikisha kunakuwepo na huduma, ikiwezekana ya saa 24 ya kuwavusha watu wa Kigamboni.

Na mpango mpya wa Magufuli wa  kuwa na Ferry ya hadi Bagamoyo na Mtoni Kijichi ili kupunguza msongamano wa magari nao haueleweki. Kwenda Bagamoyo na Mtoni Kijichi kwa njia ya maji hakuwezi tena kuwa Ferry kwa maana ya kivuko bali ni usafiri wa majini. Ndicho tunachohitaji kwa sasa wakati kitaalam usafiri huo utakuwa wa gharama kubwa zaidi na vyombo hivyo vya majini itabidi visafiri kwenye kina kirefu cha maji.

Tulidhani kwenda Bagamoyo na Mtoni Kijichi kunahitaji miundo mbinu ya barabara iliyo bora.
Na kuvuka kwenda Kigamboni kwa harakan a ufanisi kunahitaji daraja. Na je, mapato ya kivuko ya kila siku yanatumika vipi? Na tangu yaanze kukusanywa kwanini tumeshindwa kujenga daraja? Au kivuko nacho ni mradi wa wakubwa wa kuzidi kuwanyonya WaTanzania wanyonge?

Hapana, inatosha sasa. Naungana na wakazi wa Kigamboni wakiongozwa na Mbunge wao wa Kigamboni Dr. Faustine Ndungulile wanaopambana sasa kuhakikisha nyongeza hii ya nauli inasitishwa.
Ndio, waacheni Watanzania  wa Kigamboni wavuke bure kama hawavuki na vyombo vya moto. Na wana haki pia ya kujengewa daraja. Wakivuka kwa miguu au baiskeli darajani wasitozwe  hata senti tano, kama wanaovuka daraja la Sarenda, akina Magufuli na wengine.

Nawasilisha.
Maggid Mjengwa,
Bagamoyo
Januari , 2012.
http://mjengwablog.com

No comments:

Post a Comment