Pages

Saturday, July 20, 2013

UBIZE WETU UNAWALA WANETU

Na: Albert Sanga, Iringa.
Leo ngoja niweke kando kidogo masuala ya biashara na uajsiriamali; nigeukie moja ya jambo ambalo limekuwa likinigusa na kuniumiza sana kichwa-malezi ya watoto wetu kuanzia wakiwa wadogo mpaka wanapofikisha umri wa kujitegemea. Gazeti la The African linalotolewa na New Habari (2006) Limited; la jumatano ya tarehe 5, Agosti, 2009 limewahi kuripoti habari ya watoto wawili wa kiume;( mmoja miaka 7 mwingine miaka 9 ) walioshirikiana kumlawiti mtoto mwenzao wa kiume (wa umri wao) na kusababisha majeraha na maumivu sehemu zake za siri. Tukio hilo lilitokea Mbezi Temboni Kwa Msuguli jijini Dar es Salaam. Wazazi wa watoto waliotuhumiwa walipohojiwa walikiri kuwa hawakuwa na habari ikiwa watoto wao wanaweza kuwa na tabia za kifirauni namna hiyo! Habari hiyo imenipa tafakari ya kina nikiiunganisha na tukio la hivi karibuni nililolishuhudia; ambapo mama mmoja alikuwa akimuadhibu vikali mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka saba. Sababu ya adhabu hiyo ni baada ya mama huyo kumsikia binti yake huyo mdogo akiigiza sauti za watu wanaofanya mapenzi. Mtoto huyu mdogo alieleza kuwa sauti hizo ameziiga kutoka kwenye mkanda wa ngono wa video, ambao huwa wanaangalia wakiwa na dada yake (house girl) mama na baba wakiwa
kazini!
Kadiri dunia inavyozidi kubadilika katika mifumo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa npyo ambavyo watu wanazidi kusongwa na mambo mengi mno ili kukabiliana na mabadiliko hayo. Na kwa kadiri "ubize" unavyozidi kupanda npyo na athari mbalimbali zikiwemo za kijamii zinavyozidi kuongezeka. Moja wapo ya eneo hili la kijamii ni malezi ya watoto wetu wadogo.
Kuna maeneo matatu ambayo kutokana na yalivyo yanaua kabisa baadae njema za kizazi cha watoto wetu (future). Eneo la kwanza ni malezi ya watoto mikononi mwa wafanyakazi wa ndani, "house girls"; la pili ni shule za bweni ambazo zinachukua watoto wadogo na la tatu ni vituo vya watoto yatima. Katika makala haya nitaeleza maeneo mawili ya kwanza nikiliacha hili la tatu la vituo vya watoto yatima, ambalo linahitaji mjadala wa makala inayojitegemea.
Umekuwa ni mtindo maarufu sana nyakati za sasa kwa wazazi wengi miezi michache baada ya kujifungua kuwaacha watoto wao mikononi mwa "ma-house girls" ili wawalee. Na tena ni kawaida sana kuona mtoto hadi anafikisha miaka mitano akawa amelelewa na wafanyakazi wa ndani hata watano, ambao wote wameshafukuzwa kutokana na tabia mbalimbali. Hebu tutazame mfano huu.
Unaweza kuona mama mwenye nyumba anamfukuza binti wa kazi kutokana na tabia yake ya uvivu na kisha anamtafuta mwingine bila kujua kuwa ana tabia ya uzinzi. Wengi wa akina mama huwa wanakuja kushtukia kuwa wakati mwingine mabinti hawa hutembea hata na waume zao! Huyu akifukuzwa anampata mwingine ambaye nae unaweza kuona ana tabia ya uchafu, umbea, uvivu na mengine mabaya.
Saikolojia ya malezi ya watoto inabainisha kuwa ubongo wa mtoto mdogo huwa mwepesi sana kunakiri vitu na tabia mbalimbali kwa haraka sana. Anayemlea akiwa na hulka za uzinzi, udokozi, uvivu ama matusi mtoto ataiga na kuwa hivyo. Watoto wengi siki hizi wanakua wakiwa tayari ni makahaba, wezi, wakatili, wasio na nidhamu na wenye kila tabia zinazokatisha tamaa.
Mtaalamu na mwandishi wa mausuala ya saikolojia na ukuaji wa kiroho, M. Scott ameandika katika kitabu chake cha "The Road less traveled" kuwa wazazi wanafanya kosa kubwa sana la kutotumia muda wa kutosha kimalezi kwa watoto wao wakiwa wadogo. Kosa hili analiita "sins of the father".
Mtaalamu huyu anasema dhambi hii ya baba husababisha mtoto awapo mkubwa kuandamwa na upweke, kutojikubali, kukosa ulinzi wa kiroho (insecurity) hali ambayo hupelekea watu kuhamishia hali hiyo katika utafutaji usio halali wa mali, ukatili, kuheshimiwa na kulazimisha mapenzi. Inadaiwa watoto waliokosa malezi mazuri kutoka kwa baba zao huwa wakatili sana kwa wake zao pindi wakioa na kama wakishika nafasi za kisiasa mara nyingi huwa madikteta.
Makala haya hayakatai uwepo wa wafanyakazi wa ndani ambao wananidhamu na maadili mema kufanikisha makuzi mazuri kwa wanetu. Lakini yanajaribu kuangalia kundi la wale ambao wana tabia za kufisha na kuwa hatarisho kwa ustawi wa watoto wetu wadogo.
Kama walivyo wafanyakazi wengine, wafanyakazi wa ndani wametofautiana kwa hulka na misukumo ya wao kufanya kazi hizo. Tunao ambao wanafanya kazi hizo kwa sababu ya kukosa nafasi ya kuendelea na masomo, kufeli masomo, tamaa ya kutajirika wakiwa mijini na ugumu wa maisha.
Katikati yao hawa wapo ambao wamekata tamaa kabisa kiroho na kimwili. Ndio hawa ambao walalapo vyumbani na watoto wetu wa kiume huwafundisha ngono, wawapo na mabinti wetu wadogo huwafundisha usagaji! Ni hawa ambao kwa sehemu kubwa huwa ni wakatili sana, wakiwanyima chakula watoto, wakiwapiga na kuwatesa pamoja na kuwatukana na kuwanenea laana pindi wazazi wakiwa hawapo.
Nae mtaalamu wa masuala ya saikolojia, Freud Sigmund anaeleza katika tafiti zake kuwa mtoto anapozaliwa huwa na viambata vingi vizuri ambavyo husubiri muongozo sahihi ili kufikia katika utendaji wake mzuri. Viambata hivyo vinajumuisha matarajio ya kuishi na kufa, ujenzi wa kufikia kipaji kamili pamoja na furaha. Inasemwa kwamba wazazi ndio wanaobeba miongozo ya kijenetiki "genetics stimulations behaviours" kufanikisha muonekano bora wa viambata kwa mtoto.
Ni vigumu kupata kizazi bora kwa kutumia rasilimali duni. Hatuwezi kuwa na watoto waliojengeka vema kimaono, kifikra na kinidhamu kwa kuwatumia, "ma-housegirls" waliokata tamaa, wadokozi, wambea na wenye kila namna ya kutojitambua. Lakini pia tusitegemee "ma-house girls" wawatendee mema watoto wetu pindi tuwapo "bize" wakati sisi waajiri tunawadharau, tunawatesa, tunawadhulumu kwa mishahara midogo na kwa kuwarundikia kazi nyingi bila mapumziko. Tataendelea kuvuna tunachokipanda!
Eneo la pili ni mtindo unaozidi kushika umaarufu siku hizi wa kuwapeleka watoto wadogo katika shule za bweni. Mtoto hadi wa miaka mitatu anapokelewa bwenini bila wasiwasi. Hapa kuna kitu cha kujiuliza, Je, watoto hawa wadogo tunaowapeleka shule za bweni wanakuwepo katika mikono na malezi ya watu sahihi? Je, malezi yanayotolewa ndiyo ambayo mzazi angependa mtoto wake ayapate?
Mwanamuziki nguli wa rege hayati Lucky Dube amewahi kuimba wimbo wa, "Born To Suffer" akielezea athari za watoto wadogo kukua bila uangalizi wa wazazi. Katika wimbo huo Dube anasema maneno haya, "The parents are the people we are depending on, for the growth of the children. If they treat them right we are going to have brighten future.If they grow up without their parents who is going to tell them this is wrong/right"
Watoto wakiwa katika shule za bweni wanakuwa mbali na wazazi wao. Huko kwa bahati mbaya ama nzuri wanakutana na watoto wenzao ambao nao wamekusanyika na tabia mbalimbali nyingi zikiwa kutoka kwa "ma-house girls" ambao wamewalea wazazi wao wakiwa bize kazini. Kinachofuatia hapa ni kuigana.
Kama mitaani tunashuhudia watoto wakifanyiana ulawiti, wakifanya ngono na usagaji nini kituzuie kuamini kuwa huenda tabia hizi zikasambaa hata kwa hawa watoto wetu tunaowapeleka shule za bweni wakingali bado wachanga? Bila kujua ama kukusudia watoto wanaanza kuwa mashoga, wasagaji, makahaba na majambazi wakingali wadogo wa miaka saba!
Wazazi hawawezi kulazimika kukaa na watoto wao muda wote, kutokana na mishughuliko na mihangaiko ya kimaisha. Lakini ninachokiamini ni kuwa hakuna mzazi hata mmoja ambaye yupo tayari kushuhudia mtoto wake akiharibikiwa. Kutoka hapa tunapata changamoto ya kutafakari namna ya kuwaandaa watu tunaowakabidhi jukumu la kuwalea watoto wetu.
Ndio, "ma-house girls", "matrons" na "patrons" katika nyumba zetu na katika shule tunakowapeleka wanetu wanatakiwa kuwa na elimu sahihi kuhusu malezi ya watoto, (professional in children care). Wazazi waepuke kukusanya, "bora mfanyakazi wa kazi" na shule ziepuke kuteua bora mtu kuwa, "patron" ama "matron"; vinginevyo tutakuwa tunawaweka rehani watoto wetu kwa ustawi wao wa baadae.
Kuna ushindi katika malezi bora ya watoto!