Pages

Sunday, October 2, 2011

KILA LA KHERI KIDATO CHA NNE

LEO nchini kote watahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne wanaanza mtihani wao ili kuhitimisha ngazi ya pili ya safari yao ya elimu.

Hawa ni wanafunzi ambao walihitimu darasa la saba na baadaye wakajiunga na masomo ya sekondari ambayo kwa muda wa miaka minne wanafunzi hao walitumia muda wao kwa ajili ya kupata maarifa yaliyoko katika ngazi hiyo.

Lakini pia watahiniwa wengine ni wale ambao hawakufanya vizuri mtihani wa kidato cha nne wa miaka ya nyuma ambao wanafanya mtihani huo kama watahiniwa wa kujitegemea.

Watahiniwa wote wanatamani wafaulu mtihani wao ili waendelee katika ngazi ya tatu ya kidato cha tano au ya kwenda katika vyuo mbalimbali vya ualimu na ufundi kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kimasomo.

Katika ngazi hiyo tunatambua kuwa wanafunzi hao katika elimu yao wapo waliojikita katika fani ya biashara, sanaa, kilimo na sayansi. Masomo yote hayo yamewekwa na mamlaka ya elimu kwa ajili ya kumwandaa mwanafunzi huyo kujitegemea baada ya kupata ngazi hiyo ya elimu.

Ndiyo maana tunasema kila mtahiniwa ambaye leo anaanza mtihani wake anatamani afaulu vizuri ili kudhihirisha umma kuwa miaka yake minne haikuwa bure.

Lakini pia inakuwa faraja kwa mzazi, mlezi na walimu ambao wamekuwa wanahangaika naye ili kumwezesha mtoto huyo kupata elimu yake vizuri.

Tunatambua kuwa walimu wao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanafunzi wao wanaandaliwa vizuri ili kukabiliana na mtihani huo ambao utafanywa kwa zaidi ya wiki mbili.

Pia kwa upande wa wazazi na walezi tunatambua kuwa walitimiza majukumu yao ya kuwalipia ada na kuwapa mahitaji mengine ya shule ili kumwezesha mwanafunzi aweze kusoma katika mazingira mazuri.

Wanafunzi hao wanafanya mtihani huo huku kukiwa bado na kumbukumbu mbaya ya watahiniwa waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana walivyofanya vibaya katika mtihani wao wa mwisho.

Tunaamini kuwa matokeo hayo mabaya ambayo yalitokana na changamoto mbalimbali tayari walimu na wanafunzi wameyatafutia ufumbuzi na hivyo kwa wale ambao watafanya mtihani huo safari hii watakuwa wamejiandaa vizuri.

Watahiniwa wa shule ambao ni mara yao ya kwanza kufanya mtihani huo tunaamini pia kuwa matokeo ya mwaka jana yalikuwa ni funzo kubwa ili watambue kuwa hakuna lelemama katika kukabiliana na mtihani huo.

Hivyo tunaamini kuwa watahiniwa hao kwa kutambua hilo watakuwa wamejiandaa vizuri zaidi ili wasije wakaadhirika kama wenzao wa mwaka jana ambao nusu ya wanafunzi walifanya mtihani kama huo walifeli vibaya.

Kwa wale ambao ni watahiniwa wa kujitegemea ambao wanarudia mtihani huo, sisi tunawatakia kila la kheri na tunawasihi wasirudie makosa waliyoyafanya katika mtihani wa miaka ya nyuma.

Tunasema hivyo kwa vile tunaelewa kuwa hawa tayari walishang’atwa na nyoka hivyo kwao tunaamini kuwa maandalizi yao ni mazuri zaidi kwani hawataki tena kurudia makosa yaliyowafanya wakashindwa mtihani huo.

Lakini pia tunawasihi watahiniwa wote wajihadhari na vitendo vya udanganyifu ambavyo vinaweza kuwafanya wafutiwe matokeo yao. Vitendo hivyo ni vile ambavyo vinakiuka sheria na taratibu za mtihani huo.

Pia tunawasihi wanafunzi hao kuepukana na udanganyifu wa kupatiwa mtihani ya bandia. Maandalizi waliyofanya kwa miaka minne sisi tunaamini kuwa inawapa fursa nzuri ya kufanya vizuri mtihani huo.

Kwa hali hiyo tunawatakia kila la kheri watahiniwa wote ambao leo hii wanaanza mtihani wao. Tunaomba watambue kuwa matokeo ya mtihani huo ndio ambayo yatawapa taswira ya maisha yao ya baadaye.

No comments:

Post a Comment