Pages

Sunday, March 6, 2011

SIMBA AZUA TAHARUKI MBAGALA


Na Charles Lucas

ALFAJIRI ya jana haikuanza vizuri kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, eneo la Mbagala Rangitatu na maeneo mengine ya karibu ambao walikumbwa na taharuki kubwa na kuanza kukimbia hovyo huku na huko kuokoa maisha yao, baada ya kusikia ngurumo za kutisha, za simba jike aliyevamia maeneo hayo.

Harakati hizo za wakazi hao, akiwemo mwandishi wa habari hii anayeishi eneo hilo, kuokoa maisha ziliwalazimu baadhi yao kujifungia ndani ya nyumba, huku akiwa tayari ameshamjeruhi mmoja wa wananchi wa eneo hilo.

Taarifa za kuwepo kwa simba huyo jike zilianza kuvuma kutokana na ngurumo hizo lakini pia baada ya kuonekana na mmoja wa wakazi hao aliyefahamika kwa jina moja la Abdallah aliyepishana naye alfajiri alipokuwa akienda kisimani kwenye mtaa wa Kimbangulile, karibu na mto Mzinga eneo ambalo lina nyumba zilizozungukwa na msitu mdogo.

"Awali baadhi ya watu waliomuona hawakubaini kama ni simba kutokana na giza lakini kadri kulipokuwa kunapambazuka na ngurumo zake tulibaini kuwa ni mnyama huyo hatari ameingia mtaani kwetu," alisema Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Bw. Abdul Kessy.

Alisema baada ya kuhakikisha ukweli huo alipiga simu polisi kwa msaada zaidi ambapo askari watano wa Kituo cha Polisi Kizuiani walifika saa 1:30 na kuanza kumsaka kwenye maficho yake na kumpiga risasi bila mafanikio kutokana na bunduki aina ya SMG kuonekana kutomudu kumuua mpaka zilipotumika silaha 'kubwa' zaidi.

Hata hivyo wakati akiwapigia simu polisi tayari simba huyo alikuwa ameshamjeruhi vibaya mkazi mmoja wa eneo hilo aliyefahamika kwa jina la Nassor Ally, baada ya kumrukia shingoni, hivyo akakimbizwa Hospitali ya Temeke kwa matibabu.

Shambulizi hilo la simba lilitokana na Bw. Ally kumfurumusha mafichoni kwenye gofu la nyumba ambayo ujenzi wake haujaisha alipokuwa amejificha.

Upigaji wa risasi kumdhibiti, uliendelea kwa muda mrefu, ambapo takribani risasi 40 zilitumika kutokana na simba huyo kujicha kwenye vichaka na kutoonekana vema, pia zilipigwa kwa tahadhari ili kuepusha madhara mengine katika eneo hilo la makazi ya watu.

Hatimaye Simba huyo aliuawa majira ya saa 2 asubuhi hivyo kulipua shangwe kwa wakazi wa eneo hilo huku wengine wakitaka kumgawana kwa ajili ya kitoweo, ingawa wengine walionekana kuhitaji viungo vyake kwa shughuli ambazo hazikujulikana mara moja, wakidai 'mnyama huyo ana mambo mengi'.

Polisi wakiongozwa na Inspekta Abdallh Omary walilazimika kupiga risasi hewani ili kuwadhibiti wananchi hao, baada ya hali ya kugombea nyama na viungo vya mnyama huyo, kuanza kuashiria fujo, baada ya watu kulizingira gari la polisi lenye namba PT 2068 Landrover Deffender, wakitaka kupora simba huyo.

Baada ya hali hiyo kutulizwa kwa risasi ya hewani, polisi waliondoka kwa kasi hadi Kituo cha Polisi Kizuiani.

Hata hivyo wakazi hao walifika kituoni hapo kwa maandamano huku wakiimba 'tunamtaka simba wetu', wakijaribu kumchukua kwa nguvu simba huyo. Kutokana na hali hiyo, polisi walilazimika kumhamisha kwa haraka, wakimpeleka kusikojulikana.

Mmoja wa wakazi wa siku nyingi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Mzee Mahuta aliliambia gazeti hili kuwa ujio wa mnyama huyo katika eneo hilo ni moja ya mwendelezo wa tabia za wanyama kufika kwenye maeneo waliyopata kuishi zamani.

Alisema kuwa katika sehemu hiyo, hapo zamani walikuwapo wanyama hao kwa wingi, ambao walihama kutokana na mabadiliko ya kimazingira, ikiwemo kujengwa kwa makazi ya watu na kuongeza kuwa pamoja na kuuawa kwa simba huyo, anaweza kutokea mwingine tena, kwa kuwa wana tabia ya kutafutana mmoja anapopotea.

Akizungumza na Majira, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, David Misime, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema kuwa hali ya majeruhi haikuwa nzuri hivyo akahamishiwa Hospitali yaTaifa Mhimbili, kwa matibabu zaidi.

No comments:

Post a Comment