Pages

Thursday, August 18, 2011

WANAFUNZI WAGOMEA MTIHANI

Baada ya kugeuzwa 'zoba' kila mwaka, Wanafunzi wameanza kuamka na kudai "Elimu bora" si "Bora elimu"!

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Vijibweni, Kigamboni, Dar es Salaam wamecharuka, hali iliyowafanya polisi kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi wa kidato cha nne, waliokuwa kwenye mgomo wa kupinga kufanya mtihani wa kujipima (mock) uliodaiwa kuwa ni 'feki'.

Mbali na kupinga kufanya mtihani huo, wanafunzi hao pia wanaulalamikia uongozi wa shule kwa kuwatoza Shilingi 12,000 zikiwa ni malipo ya kufanya mtihani huo, badala ya malipo halisi ya Shilingi 7,000 waliyotozwa wanafunzi wa shule nyingine.

Polisi watano waliovalia sare za askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wawili sare za polisi wa kawaida na kumi kiraia, wakiwa ndani ya magari manne ya polisi, wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Temeke, Thobias Sedoyeka na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Kigamboni, Mrasani Ndewina walifika katika eneo la shule, majira ya saa saba mchana wakiwa wamebeba mabomu ya machozi na silaha za moto baada ya kuarifiwa kulikuwa na vurugu shuleni hapo

Kabla ya polisi kufika, kundi la wanafunzi, walikusanyika katika ofisi za Ofisa Mtendaji wa Kata ya Vijibweni, kufuatilia hatima yao.  Polisi walipofika na kulikaribia eneo hilo, wanafunzi hao walianza kukimbia na kutawanyika sehemu mbalimbali.

Baadaye wanafunzi hao walirejea kufuatia polisi kuwaita ili kuzungumza nao ambapo RCO Sedoyeka aliwalaumu kwa kufanya mgomo, akisema kama walikuwa na malalamiko walitakiwa kuyapeleka kwa wazazi kwa kuwa ndio waliotoa fedha wanazodai.

Wanafunzi hao walipinga kauli hiyo, wakisema hawajagoma, bali wanalalamikia kupelekewa mtihani 'feki' wa Hisabati na Uraia pamoja na kutapeliwa fedha za malipo ya mtihani.
  • Kwa niaba ya wenzake, Ruth Gervas, alidai walipewa mitihani Jumatatu wiki hii na ndipo walipobaini kuwa ni 'feki' walipoilinganisha na ile waliyopewa wenzao katika shule nyingine. Siku iliyofuatia waligoma, baada ya kuona mitihani wanayoendelea kupewa ni ile ile 'feki. 
  • Ruth aliongeza kuwa mitihani hiyo ni feki kwa kuwa tayari imeshajibiwa kwa kalamu ya risasi tangu Mei, 2011, huko mkoani Arusha. 
  • Naye mwanafunzi Zaituni Ally alidai mitihani hiyo walipewa ikiwa imefungwa, kinyume cha kawaida. 
  • Zaituni alidai wanashangaa wenzao katika shule nyingine wamekuwa wakipewa nakala za mitihani hiyo baada ya kufanya, lakini wao hawapewi.
Ruth alidai walijaribu kuwasiliana na uongozi wa shule kuhoji suala hilo, lakini wamekuwa wakipewa vitisho na kejeli na dharau kuwa, “Nendeni, msiende, kwa afisa elimu, nyinyi mmeshaliwa.”

Mkuu wa Shule Msaidizi, aliyefahamika kwa jina moja la Christina, alipofuatwa, aliwazuia waandishi kuingia ndani ya ofisi yake.

Mratibu wa Elimu wa Kata ya Vijibweni, Mohamed Likwembe, alithibitisha kuwa mitihani hiyo ni 'feki' na kwamba, wamepanga na uongozi wa shule kufanya mkutano Jumatatu ijayo pamoja na wazazi, wanafunzi, Ofisa Elimu wa Manispaa.

Polisi waliwaamuru wanafunzi hao kuondoka shuleni hapo hadi siku ya Jumatatu.
wavuti.com

No comments:

Post a Comment