Pages

Thursday, August 18, 2011

KAULI YA SHIBUDA


Mbunge wa Maswa Magharibi (CHADEMA), John Shibuda, amejilipua kwa kusema yeye si msaliti wa Chadema bali anatofautiana na viongozi wa juu wa chama hicho kutokana na kuweka mbele zaidi maslahi yao binafsi kuliko ya wapigakura na Watanzania.

Pia, amesema kuwa yuko tayari kwa uamuzi wowote utakaochukuliwa na chama hicho, kwani watu mbalimbali wamekuwa wakimuuliza ni nini hatma yake ndani ya CHADEMA, kufuatia Kamati Kuu kukutana mara mbili kumjadili kabla ya kumchukulia hatua.

Shibuda, ambaye kila anaposimama wabunge huvunjika mbavu kwa vicheko kutokana na lugha ya msamiati anayotumia, alitoa msimamo huo Bungeni alipokuwa akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2011/2012.

Baadhi ya viongozi wa CHADEMA wamekuwa wakimtuhumu Shibuda kwenda kinyume na msimamo wa chama hicho, ikiwemo kugomea kuchukua malipo ya posho za ubunge, ambapo ameupinga. Mbunge huyo wa zamani wa CCM anachukua malipo hayo, "Nilipokuwa kwenye msiba (mazishi ya Luteni Jenerali Silas Mayunga mkoani Shinyanga), niliulizwa maswali mengi kuhusu hatma yangu CHADEMA, nimeona hili ni muhimu kulizungumza. Mheshimiwa Spika, maliasili katika nchi yetu ni siasa pamoja na utawala bora, viongozi wa dini kazi yao ni kung'arisha binadamu ili waende akhera, viongozi wa kisiasa kazi yao ni madobi wa kung'arisha serikali," aliongeza. Wananchi wa Maswa na Watanzania wengi, hata nyinyi wabunge, kila saa wananiuliza vipi Kamati Kuu ya CHADEMA, wamekuita? Wamekufukuza? Kauli zinazotolewa na kunukuliwa na magazeti ni kauli hatarishi. Ukificha ukweli, unakaribisha mikosi. Maneno yaliyonukulikuwa na vyombo vya habari kwamba mimi ni msaliti si ya kweli, mimi siyo msaliti na sijavunja msimamo wa kikao cha kamati. Nimetofautiana na watu wachache kwa dhamana zao binafsi kwa sababu ya kudai haki, mimi siwezi kugandishwa na kukosa demokrasia ya kikatiba kutoa maoni yangu".

Shibuda alisema yeyote, ambaye anageuza cheo chake kwa maslahi yake, hatokuwa tofauti na wale  wanaopindisha sheria. Alisema kwa kawaida, mazuri huwa ya baba na mabaya huwa ya mama na kuongeza, bahari ikichafuka, nahodha hupimwa ujasiri wake, "Kwa hiyo ninakiri kuchafuka kwa hali ya hewa, lakini napenda kusema Shibuda ni jasiri na Maswa siyo tunda pori, ina wenyewe na wananchi wa Maswa wanasubiri na wamekataa kuporwa kama wanyamapori kuhusu mbunge wao," alisema.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema hekima na busara ndizo zinazoweza kukiongoza chama chochote kufika salama, na kuongeza yeye hana makuzi ya kukuwadia mtu na kuviasa vyombo vya habari visikubali kulishwa maneno.

Alisema wapo wanasiasa wanaotumikia jamii na wengine walioweka mbele zaidi maslahi yao binafsi na kwamba hapa nchini kuna vyama vya siasa zaidi ya 12, vikiwepo vinavyoendeshwa kisiasa, maslahi jamii, maslahi binafsi na saccos, hivyo wananchi wanapaswa kuvichambua ili kupata ukweli, "Yesu alituhumiwa na kusulubiwa na alidhalilishwa. Mimi Shibuda sipo tayari kudharauliwa, na kupuuzwa na mtu, sijali sana kwa sababu tabia zangu ni za peponi na uwazi na ukweli ndio unaoniongoza. Dini yangu inanizuia kusema uongo, kwa hiyo nasikitika kwa mtu ambaye namkwaza, hususan ambaye hapendi ukweli," alisema.

Mbunge huyo alisema wapo viongozi wanaoteuliwa na Mwenyezi Mungu na wengine wanaoteuliwa kutokana na pesa na kuwataka waliopewa nyadhifa hizo kuacha dhambi zao na kutumikia jamii.

1 comment: