Pages

Tuesday, November 15, 2011

Tandika wachanga fedha kuchimba mifereji

WANANCHI wa kaya zipatazo 23 katika Kata ya Tandika eneo la Devis Kona wamechanga Sh150,000 kwa ajili ya kuchimba mitaro ya kupitisha maji yanayokwama na kusababisha mafuriko katika nyumba zao kufuatia mvua zilizonyesha mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Davis Corner, Mfaume Mbonde alisema kwamba aliwahamasisha wakazi hao ili kila kaya kutoa Sh5,000 kwa ajili ya kuchimba mitaro iliyoziba na kusababisha mafuriko ndani ya nyumba za wakazi wa mtaa wake.

Mbonde alisema kwamba walikuwa wakipeleka malalamiko mara kwa mara katika ofisi ya kata, lakini hatua za haraka hazikuchuliwa hali iliyosababisha yeye kuchangisha fedha katika mtaa huo.

 “Tulipeleka malalamiko yetu katika ofisi yetu ya kata mara nyingi tu, lakini hatuoni hatua zikichukuliwa na hivyo nimechangisha hizo fedha” alisema Mbonde na kuongeza

“Mimi nimeongezea  Sh20,000 ili kutatua tatizo la maji ya mvua kukwama katika maeneo haya”, alisema.
Akizungumzia adha wanayoipata kutokana na mafuriko hayo, mkazi wa eneo hilo, aliyejitambulisha kwa jina  la Albert Mwakatumbula alisema kuwa maji yanaingia hadi ndani na kusababisha vitu kuloa ikiwa ni pamoja na magodoro, makochi na vyombo vingine.

Alisema hali hiyo ilijianza baada ujenzi wa barabara iliyokuwa ikitoka Davis corner kwenda Yombo Dovya kuziba miundo mbinu iliyokuwa ikipitisha maji katika mtaa huo.Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tandika, Joseph Kambanga alionyesha wasiwasi kwa wananchi hao kuchangishana fedha hizo.

Alisema kuwa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mwenyekiti ya Serikali ya Mtaa wa Devis Kona, alikwenda eneo hilo pamoja na  mhandisi wa Manispaa ya Temeke kisha wakatoa ombi kwa kampuni husika kuchukua hatua za dharura ili kudhibiti hali hiyo.

Afisa Mtendaji huyo wa kata ya Tandika aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo itokayo Devis Kona kuelekea Yombo Dovya ulianza Septemba mwaka jana lakini hajui ujenzi huo utaisha lini  kwani mkataba wa mkandarasi huyo upo Manispaa ya Temeke.

No comments:

Post a Comment