Pages

Monday, February 14, 2011

UMEME JANGA LA TAIFA

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Nishari na Madini, January Makamba, amesema yeye na wajumbe wenzake wa kamati hiyo wamejizatiti kuchukua hatua za haraka za kuishauri na ikibidi kuishinikiza serikali kuchukua hatua za haraka na sahihi za kukabiliana na tatizo kubwa la mgawo wa umeme linalolikabili taifa.

January aliyasema hayo jana jioni wakati alipozungumza kwa simu na Tanzania Daima muda mfupi baada ya kuwaongoza wajumbe wa kamati yake kutembelea bwawa la Mtera ambalo ni moja ya vyanzo muhimu vya uzalishaji wa umeme.

“Wakati tukitambua kwamba kazi ya utekelezaji ni ya serikali, baada ya kutembelea Mtera tumemweleza Waziri (wa Nishati na Madini) bayana kwamba tutaishauri serikali na wakati mwingine tutalazimika kuishinikiza kuchukua hatua sahihi na za haraka za kulimaliza tatizo la umeme ambalo lina athari kubwa kwa maendeleo ya taifa,” alisema January.

Katika kuonyesha namna hali ilivyo mbaya alisema hivi sasa Mtera imebakiza kina cha maji cha mita 1.32 tu kabla ya mitambo kuzimwa kutokana na kina cha maji kupungua.

Alisema hali hiyo ndiyo ambayo inalifanya bwawa hilo ambalo lina uwezo wa kuzalisha megawati 80 za umeme litoe megawati 52 tu kwa sasa wakati taifa likisubiri kudra za Mungu kuifanya mvua inyeshe ili kina cha maji kiongezeke.

Akieleza kile walichokiona Mtera, January alisema wamejifunza kwamba ni jambo la hatari kuendelea kuweka matumaini ya kudumu katika umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji wakati hali ikijulikana bayana kwamba mvua ni za msimu na zisizo za uhakika.

January ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bumbuli (CCM), alisema ni jambo lisiloingia akilini kwa taifa kuendelea kuweka matumaini makubwa kwa umeme unaozalishwa na maji yayotokana na kudra za Mwenyezi Mungu za kuleta mvua.

“Leo hii tumekuwa tukiwahimiza wakulima kutumia njia mbadala za kilimo badala ya kuendelea kutegemea mvua iwapo wanataka kupiga hatua. Iweje sisi wenyewe tunaosema hivyo ndiyo tuwe wale wale tunaotaka umeme wetu uwe wa uhakika kwa kutegemea mvua?” alihoji January.

Alisema baada ya kuzungumza na wataalam wa TANESCO wakati wakiwa Mtera, wanajipanga kusafiri hadi Dar es Salaam baada ya vikao vya Bunge kwisha na kukutana nao kujadili kwa kina namna ya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme.
Kwa hiyo watu wa Temeke msilalamike hili suala ni la kitaifa zaidi tuombe dua mvua zianze kunyesha huko Mtera.

No comments:

Post a Comment