Pages

Thursday, February 24, 2011

MKOPO WA BIASHARA


Je wewe ni mfanyibiashara ama unanuia kuanzisha biashara hivi karibuni? Ni lazima basi utakuwa umewaza jinsi utakavyo pata fedha za kukuwezsha kuanzisha au kuipanua biashara yako.

Kuna njia mbalimbali za kupata fedha hizi unaweza kuweka akiba kwa muda fulani hadi kitakapotimia kiasi unachohitaji, unaweza pia kukopesha fedha hizo kutoka kwa jamaa na marafiki. Kila mojawapo ya njia hizi ina changamoto yake ambayo utakumbana nayo.

Habari njema sasa ni kuwa kando na njia hizi unaweza kupata mkopo kutoka kwa benki ama vyama vya ushirika lakini haina maana kuwa mikopo ya benki haina changamoto.

Hivi sasa kuna matangazo mengi ya benki na vyama vya ushirika katika magazeti, redio na vyombo vingine vya habari kuhusu namna ya kupata mikopo, kilicho muhimu ni wewe kama unyetaka mkopo kuchunguza kwa kina na uangalifu kuona ni benki ipi ama ni chama kipi cha ushirika kina mkopo ambao utakufaa.

Ni wazi kuwa benki hizi zinatumia lugha ya mvuto, kwa mfano benki ya Barclays nchini Kenya inafanya kampeni iitwayo ‘rarua mkopo’ ambapo ukijisajili kuchukua mkopo unewezeshwa kulipa mkopo ulio nao sasa. Huko Tanzania benki ya CRDB inatoa mkopo wa ‘Bidii’ mahsusi kwa wenye biashara ndogo.
Usipokuwa mwangalifu huenda ukaingia katika mpango ambao hauwezi kukimu ama kutoshelezi mahitaji yako. Lakini swali muhimu zaidi ni je utawezaje kutathmini mpango wa mkopo ambao unapendekezwa na benki fulani?

Kwanza jiulize ujue unahitaji pesa kufanya nini haswa katika biashara lako. Unataka kununua mashine, kukarabati vifaa, kuongeza mali ghafi au kuongeza uzalishaji ? na kufanya hivi utahitaji pesa kiasi gani, na ni muda gani ambao kwa mtazamo wako umetosha kuulipa mkopo huo na pia kulingana na mapato yako unaweza kulipa kiasi gani katika kila awamu ?
Baada ya kuzingatia mambo hayo hatua ya pili ni kusoma kwa kina masharti ambayo yamewekwa na benki ambayo inatoa mkopo ambao unaona unakufaa. Kwa kawaida masharti hayo licha ya kutegemea benki yenyewe huwa kama vile uwe raia wa nchi fulani, stakabadhi za kudhibitisha kuwa biashara yako ni halali na hulipa ushuru.

Kando na hayo utahitajika kuthibitisha una uwezo wa kulipa mkopo huo na hapa tena kulingana na kiasi ambacho unanuia kukopa huenda ukatakiwa kuweka dhamana kama vile gari, nyumba ama mali nyingine.

Hatua hii ndiyo italeta utata kwani inadaiwa kuna benki ambazo huficha taarifa na takwimu zilizo muhimu kama vile ada wanazo toza kando na zile za kulipa mkopo huo. Ni wajibu wako kuhakikisha umeelewa kikamilifu mkopo ambao umekubali kuchukua kabla ya kutia sahihi.

Kumbuka kuwa hatimaye utahitajika kulipa mkopo huo, na hivyo basi ni muhimu kuwa na mpango murwa wa kuulipa mkopo huo na jambo lingine la kutilia maanani ni kuwa na dhamira ya kuchukua mkopo ni kuanza au kuipanua biashara usije ukaingia katika mtego wa kuzifuja pesa hizo holela.

Msaada toka kwa:
Ken Owino

No comments:

Post a Comment