Pages

Saturday, February 19, 2011

Kambota: Tanzania Yetu, Dar Yetu Na Jeshi Letu


……Mjenga nchi ni mwananchi……..

Nimekaa nimetafakari naona iko haja ya kuandika kuhusu tukio la kulipuka kwa mabomu kule kambi ya Gongo la Mboto jijini Dar es salaam.


Ikumbukwe kuwa tukio hili linajitokeza ndani ya miaka mitatu tangu tukio la namna hiyo au linalofanana na hilo litokee kule Mbagala kuu na pia hapa sitaki kufanya assumption ila nalazimika kusema kuwa YAWEZEKANA BAADHI YA NDUGU WA WAATHIRIKA WA MBAGALA PIA WAMEATHIRIKA GONGO LA MBOTO.

Nani asiyejua kuwa ukiacha viongozi wa dini hapa Tanzania ni jeshi ndicho chombao ambacho kinaaminika zaidi hapa nchini? Nani asiyejua kuwa jeshi letu limedumisha nidhamu yake kwa muda mrefu licha ya mapungufu ya hapa na pale ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanajeshi wachache kuhusika kwenye matukio kama ujambazi au kupiga raia lakini bado yatosha kusema jeshi letu tunaliamini sana.

Ingawaje ni ukweli wa kikatiba kama sio sheria kuwa kuandika kuhusu mambo ya jeshi kwa mtu asiye mwanajeshi ni kosa ila nafikiri kulipuka kwa mabomu na watu kuathirika sio jambo la jeshi bali la wananchi yaani watanzania hasa wa Dar es salaam ambao bila shaka ni waathirika wakubwa wa maafa hayo hivyo na kila sababu na haki ya kuliandikia tukio hili.

Kwa kweli tunaamini kuwa kilichotokea ni bahati mbaya sawa lakini kwanini hatukujifunza Mbagala? Kama kweli tulijifunza kwanini tukio hili limejirudia? Haya ni maswali ya msingi ambayo yanapaswa yajibiwe kwa hoja sio kwa kupoozana kwa kulipana fidia pekee au kuombana pole.

Sawa kulipana fidia ni muhimu kweli hata kupeana pole ni swala la ubinadamu lakini hoja sio hii la msingi hapa jeshi letu lirudishe imani ya wananchi ambayo imeanza kupotea kwa jeshi hilo.

Kuna maneno yamezagaa kuwa mara jeshi letu halina wataalamu, mara uzembe tu, mara kutofanyika kwa ukaguzi wa mara kwa mara lakini haya sio mambo mazuri kuzungumzwa kuhusiana na jeshi letu. Mimi nadhani na naamini hata mkuu wa majeshi Jenerali Davis Mwamunyange na mnadhimu mkuu wa jeshi Luteni Jenerali Abdurahman Shimbo na hata wanajeshi naamini hata wao hawapendi kauli hizi hata kidogo , leo wangependa kuona watu wakisema ….aah! jeshi letu lina wataalamu waliobobea bwana…, hakuna uzembe jeshini…., jeshi letu ni la wachapakazi……au jeshi letu safi sana bwana…



Lakini haya hayaji hivihivi hata kidogo, yanajengwa , kama watu sasa walivyojengwa bila kujua sasa wanaiogopa Dar es salaam, wanaogopa jeshi badala ya kulipenda na kuliheshimu kisa jeshi letu limeshindwa kuzuia mabomu yasilipuke tena baada ya kuahidi hivyo kule Mbagala kuu. Hili si jambo la kubeza kabisa watanzania wanalia, wana hofu na wametishika sana. Mabomu, mabomu mabomu! Kila kwenye mdomo wa watanzania! Sio jambo jema ni lazima twende mbele zaidi ya kulipana fidia.



JWTZ wadhamirie kwa dhati hili lisitokee tena, kama ukaguzi wa kambi ulikuwa unafanyika kila mwaka basi sasa uwe kila mwezi, kama ulikuwa kila mwezi sasa uwe kila week, kama kila week sasa uwe kila siku , kama kila siku sasa uwe kila saa NA KAMA UKAGUZI KWENYE MAKAMBI YETU YA JESHI ULIKUWA UNAFANYIKA KILA SAA SASA UFANYIKE KILA DAKIKA AU SEKUNDE.



Watanzania tumefadhaika sana, tumesikitika sana zaidi tumeanza kuliangalia jeshi letu kwa jicho la kuhoji hili si jambo jema hata kidogo ikumbukwe tu kuwa Tanzania ni Yetu, Dar ni Yetu na Hata Jeshi Pia ni Letu.





Nova Kambota mwanaharakati,

Mzumbe University,

Morogoro, Tanzania

0717-709618 au 0766-730256,

novakambota@gmail.com

novadream.blog.com

18 Februaary 2011.

No comments:

Post a Comment