Pages

Wednesday, February 15, 2012

WANAOSEMA LOWASSA NI FISADI KWA SABABU YA RICHMOND SAGA, HAMKUONA HII TAARIFA NILIYOIONA MAHALI? EDWARD LOWASSA ALISAFISHWA NA MWAKYEMBE

Sasa ni wazi kwamba baada ya waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa kujitetea mbele ya kikao kilichopita cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) mjini Dodoma, wajumbe wengi wa kikao hicho, na wachambuzi wa mambo ya kisiasa nchini wanakubaliana kwamba mbunge huyu wa Monduli amekuwa akisakamwa na baadhi ya viongozi ndani ya chama chake na watu wengine, si kwa sababu yeye ni fisadi au kuna tuhuma za ukweli za ufisadi dhidi yake, bali ni kwa sababu ya mbio za urais za mwaka 2015.
Ingawa yeye mwenyewe hajakubali wala kukanusha nia yake ya kugombea urais mwaka 2015 kupitia chama chake, lakini zimejengeka hisia kwamba ana nia hiyo, lakini kinachoumiza wengi si hiyo nia tu, maana na wengine wengi tu ndani ya chama hicho wanaelezwa kuwa na nia hiyo. Kinachowasumbua watu wasiompenda ni kwamba kati ya hao wanaodhaniwa kuwa na nia
Inawezekana kumbukumbu za watu wengi zimechakachuliwa kiasi cha kutokumbuka kwamba Kamati Teule ya Dr. Harrison Mwakyembe iliyokuwa inachunguza sakata la mkataba wa kufua umeme baina ya TANESCO na kampuni ya Richmond ilimsafisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kwamba hakuwajibika na kujiuzulu kutokana na ufisadi wake katika sakata hilo, bali aliwajibika kisiasa kwa makosa ya watu waliokuwa chini yake.
Inashangaza pia kwamba hata wajumbe wa Kamati hiyo, akiwemo mwenyekiti wao, Dr. Mwakyembe, wanashindwa kumtetea Bw. Lowassa anapoendelea sasa hivi kusakamwa na baadhi ya wanasiasa na wanajamii kwamba ni fisadi kutokana na kashfa ya Richmond, na hawajitokezi kumtetea na kurejea hitimisho la ripoti yao ndani ya Bunge. Lakini mbaya zaidi hata baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu kabisa wa chama chake hawakumbuki hitimisho la ripoti hiyo na wameng’ang’ania kwamba kujiuzulu kwa Lowassa uwaziri mkuu hakutoshi na inabidi chama kimtose zaidi kutokana na kashfa ya Richmond.
Kwa kweli suala la tuhuma dhidi ya Edward Lowassa kwamba ni fisadi kutokana na tuhuma za Richmond, mtu unaweza kusema huu ni unafiki na chuki za kisiasa zilizopita kipimo. Suala la Richmond ni moja kati ya kashfa hapa nchini ambazo zilichunguzwa kwa makini sana na Bunge kupitia Kamati Teule na matokeo na hitimisho la uchunguzi huo yakamsafisha Lowassa kwamba alijiuzulu siyo kwa sababu alihusika moja kwa moja na kashfa hiyo bali aliwajibika kwa makosa yaliyotendwa na watu wa chini yake.
Tarehe 15 Februari 2008, kwa mujibu wa taarifa rasmi za majadiliano Bungeni (Hansard), Dr. Harrison Mwakyembe, wakati akihitimisha hoja ya Kamati Teule iliyochunguza suala la Richmond, alisema:
“Mheshimiwa Spika, ninaomba nianze na utangulizi mfupi na rahisi; uwajibikaji kwa viongozi waandamizi katika nchi zinazolinda na kuenzi demokrasia kama vile Tanzania, una sura mbili; sura ya kwanza, kiongozi anawajibika kwa makosa yake mwenyewe ya kiutendaji. Kiongozi anafanya maamuzi mabaya, pengine kwa kishawishi cha pesa, maamuzi yake yakaleta hasara au kiongozi ameshindwa kutoa ushauri mzuri kama kiongozi, kwa kukiuka kanuni, kukiuka taratibu na kadhalika, matatizo yakatokea, anawajibika. Sasa sura hii ya uwajibikaji, inahusisha uvunjwaji wa maadili, kanuni, sheria, miiko ya uongozi na kadhalika. Chini ya uwajibikaji wa aina hii, kiongozi anaweza akashitakiwa, akaadhibiwa mbali na kuachia ngazi. Nitarejea kwenye sura hii hivi punde. Suala la msingi hapa ni kuwa, kuna element ya adhabu katika sura hii ya kwanza.
“Sura ya pili; kiongozi anawajibika kwa makosa ambayo si yake moja kwa moja ila yaliyofanywa na watendaji chini yake. Kitendo cha kuwajibika kwa aina hii, kunaijengea Serikali au taasisi heshima na imani ya pekee katika jamii, kunatoa picha ya kwamba, uongozi unajali, unalielewa tatizo kwa kubeba lawama wao wenyewe. (Makofi)
“Mheshimiwa Spika, katika suala hili la Richmond, viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini na Waziri Mkuu, walikuwa wanakabiliwa na uwajibikaji wa aina hizo mbili. Kwanza, uwajibikaji unaotokana na makosa ya viongozi wenyewe katika maamuzi yao, maelekezo yao, maagizo yao na kadhalika. Mawaziri wote wawili wa Nishati na Madini; aliyetangulia na aliyefuatia baadaye, Katibu Mkuu na Kamishina wa Nishati, wote tukawaona wana makosa ya moja kwa moja, waliyoyafanya wao kwa njia moja au nyingine. Kwa kuwa uwajibikaji wa aina hii, unatokana na ukuikwaji wa kanuni, taratibu, maadili, sheria na kadhalika, Kamati Teule ikahakikisha inawahoji wote ili kusikia their side of the story kabla ya kutoa pendekezo la kuwawajibisha kwa makosa waliyofanya. Ndiyo maana baada ya kuwahoji, tumependekeza hatua za kuchukuliwa dhidi yao.
“Hali haikuwa hivyo kwa Waziri Mkuu; Kamati teule ilikuwa na ushahidi wa mawasiliano ya karibu kati ya Waziri Mkuu na Uongozi wa Wizara. Ushahidi huo haukutosha kwa uwajibikaji wa sura ile ya kwanza wa kiongozi kukutwa na makosa ya moja kwa moja, aliyoyafanya yeye mwenyewe kwa njia moja au nyingine, lakini ushahidi huo ulitosha kwa uwajibikaji wa sura ya pili, ambao hauhitaji mahojiano, kusikilizwa wala utetezi. Unawajibika kwa makosa ya watendaji walio chini yako. Hiyo ndiyo demokrasia. Wabunge wengi wametoa mifano mingi hapa, ukiwemo wa Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi, alipokuwa waziri wa Mambo ya Ndani; aliwajibika kwa makosa ya askari huko Shinyanga wakati yeye alikuwa Dar es Salaam; hatukumsikia akidai apewe nafasi ya kusikilizwa na hata kama angepewa, bado angewajibika yeye mwenyewe. (Makofi)
“Mheshimiwa Spika, Kamati Teule inatamka ukurasa wa 37 wa taarifa yake kuwa, ninanukuu ‘Ushiriki huu wa karibu wa Waziri Mkuu katika kila hatua ya zabuni ya umeme wa dharura si lazima uwe ushahidi wa kwamba, kiongozi huyo wa Kitaifa alihusika katika kuibeba Richmond. Unaweza pia ukawa ushahidi wa style yake ya kawaida kabisa ya Waziri Mkuu katika kufuatilia masuala yote ya Kitaifa kwa karibu sana, tukizingatia kwamba, nchi wakati huo ilikuwa katika kipindi kigumu sana cha ukosefu wa umeme…..”
Nina wasiwasi kwamba baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa na wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM ama wamesahau kauli hii ya Dr. Harrison Mwakyembe, ama kwa makusudi wanataka kupotosha watanzania. Akina Nape Nauye na John Chiligati wanamjumuisha Edward Lowassa kwenye kundi la mafisadi kutokana na suala la Richmond. Lakini Chiligati alikuwa Bungeni wakati Mwakyembe akihitimisha hoja ya Kamati yake Teule, na alimsikia Mwakyembe akimsafisha Lowassa kwamba makosa yake hayakuangukia kwenye sura ya kwanza ya uwajibika, ya kiongozi kuwajibika kwa makosa yake mwenyewe. Sura hii ndiyo unayoweza hata kumwita mtu fisadi. Lakini Lowassa aliwajibika kwa makosa ya watendaji walio chini yake, hata kwa mujibu wa Dr. Mwakyembe. Anayewajibika kwa aina hii ya pili huwezi kumwita fisadi. Akisifu aina hii ya Edward Lowassa kuwajibika, Dr. Mwakyembe anasema, “…Kitendo cha kuwajibika kwa aina hii, kunaijengea Serikali au taasisi heshima na imani ya pekee katika jamii, kunatoa picha ya kwamba, uongozi unajali, unalielewa tatizo kwa kubeba lawama wao wenyewe”. (Makofi). Mwakyembe anakwenda mbali na kuhusisha uwajibikaji huu wa Lowassa na ule wa Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akiwasilisha utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu suala hilo tarehe 28 Agosti 2008 alisema yafuatayo kuhusu azimio na. 16 la Waziri Mkuu kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi huo, “Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zilizochukuliwa ni kwamba, Azimio hili lilitekelezwa mwezi Februari, 2008 kwa kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu aliamua kujiuzulu kwa kuwajibika kisiasa kwa maslahi ya Taifa.” Hivyo ni wazi hata Serikali inakubaliana na Kamati Teule kwamba Mhe. Lowassa aliwajibika, siyo kama fisadi bali aliwajibika kisiasa kwa maslahi ya Taifa. Ndiyo maana Azimio na. 16 linalomhusu Waziri Mkuu halikuendelea kujadiliwa Bungeni. Hata wanaodai kwamba baadaye Spika aliondoa hoja hii Bungeni kabla halijakamilika, wajue kwamba suala la Waziri Mkuu kuwajibika (Azimio na. 16) halikuwemo tena, na kwa hiyo hata hoja ingeendelea kuwa Bungeni Lowassa asingeguswa tena.
Sudi Mnete 

No comments:

Post a Comment