Pages

Friday, April 8, 2011

KATIBA MPYA CHINI YA SAA 100!


Ndugu Zangu,


TUMEONA na kusikia kwenye taarifa ya habari TBC1 jana usiku, Waziri wa Sheria Na Katiba Bibi Celina Kombani akitamka; kuwa utaratibu wa kukusanya mawazo ya wadau juu ya mapendekezo ya Muswaada wa Sheria itakayosimamia mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya utachukua siku tatu!


Na ulianza jana, Dodoma na Dar es Salaam. Leo zimekuja taarifa, imeongezwa siku moja zaidi. Utachukua siku nne, saa 96. Naam. Chini ya saa 100! Ina maana , kuwa baada ya saa 96 za kukusanya maoni ya wadau Muswaada utarudi tena bungeni na kujadiliwa na waheshimiwa wabunge.



Na ukipitishwa, basi, mchakato unaendelea ukimruhusu Rais kuanzisha mchakato kwa kuwateua wajumbe wa Kamati itakayoratibu mchakato na mengineyo. Na tafsiri kuu hapa ni hii; Watanzania tutakuwa tumepewa Katiba Mpya tunayoililia chini ya saa 100. Na lifuatalo nina hakika nalo, kuwa Watanzania HATUTARIDHIKA nayo. Kwanini? Fuatilia ninachoandika, utanielewa.


Ni juzi tu nimeandika kupitia safu yangu kwenye Raia Mwema, kuwa; ” Nauona, mwelekeo mbaya wa upepo wa kisiasa nchini mwetu. Nina shaka kubwa. Naamini, tuko wengi wenye mashaka na mwelekeo wa nchi yetu tunayoipenda.” ( Mraba Wa Maggid, Raia Mwema, Aprili 6, 2011 )


Kwenye makala yangu ile niliweka wazi, kuwa katika hili la mchakato wa kupata Katiba Mpya tumeanza na mguu mbaya. Tumeyaona Dodoma na Dar es Salaam jana. Sikuhitaji kuwa na Elimu ya Unajimu kubaini hilo. Tulishaziona ishara.


Hakika, ikitaka, Serikali inaweza kurudi nyuma na kuanza upya. Wahenga walitwambia, ni heri nusu shari kuliko shari kamili. Katiba ni ya Watanzania, kwanini usiwepo ’ Mchakato Kivuli’- Shadow process utakayojumuisha makundi mbali mbali ya kijamii. Wajadili kwa uhuru kabisa, yote. Kisha nao waje na mapendekezo yao. Ingeepusha shari kamili.


Haiyumkini suala nyeti kama la Muswaada wa Mapendekezo ya Sheria itakayosimamia mchakato wa Katiba likajadiliwa na wadau kwa siku nne tu. Ndio, chini ya saa 100. Maana, Katiba ya nchi ni kitabu nyeti chenye kuhusu maisha ya kila siku ya Mtanzania. Hauingii akilini, utaratibu wa wadau kujadili Muswaada huu kwenye kumbi za Msekwa Dodoma na Karimjee Dar. Halafu ikawa basi, imetosha. Urudishwe kwa Wabunge, waujadili, kisha waupigie kura, na zaidi kuupitisha.


Watanzania tuko zaidi ya milioni 42. Ni vema na ni busara kukawepo na wigo mpana zaidi wa kuwafikia Watanzania wengi zaidi kadri inavyowezekana. Hivi, inatoka wapi, ’ghafla’ na ’dharura’ hii ya wadau kutakiwa kutoa maoni yao ndani ya saa 96? Maana, hili ni suala nyeti kwa Watanzania na lenye kuhusu mustakabali wa nchi. Kwa nini tusipewe muda zaidi wa kutafakari?


Na wahusika wana nafasi ya kujisahihisha na kuokoa sura zao. Maana, tukubali, kuwa mchakato unaoendelea hautasaidia kupata Katiba itakayowapa imani Watanzania kuwa italinda maslahi ya taifa lao na yenye kukidhi matakwa ya wakati tulionao. Hayo ni mashaka ya kweli ya Watanzania walio wengi, yasipuuzwe. Na Watanzania wanajua, kuwa wanachokitafuta sasa walikuwa nacho, walikipoteza, kwa bahati mbaya.


Na kuna kisa kutoka Uganda. Milton Obote, mbali ya mambo mengine, anakumbukwa na Waganda kwa tukio la kihistoria la ’ Kuchakachua’ Katiba ya nchi hiyo kwa kuifanyia mabadiliko kinyemela. Ilikuwa Aprili 15, 1966. Ilikuwa aubuhi moja. Wabunge wa Uganda, kabla ya kikao, walielekezwa kwenye masanduku yao ya makabrasha bungeni wakachukue ’ Muswaada wa dharura’ wa Marekebisho ya Katiba.



Muswaada ule wa Marekebisho ya Katiba ukajadiliwa ’ kishabiki’ na kupitishwa ndani ya saa moja. Unakumbukwa kwa jina maarufu la ’ Pigeon-hole’ Constitution- Katiba ya Sanduku la Makabrasha. Ni kitendo kile cha Obote, ndicho kilichopelekea Uganda kupitia wakati mgumu kwa miaka miaka mingi zaidi baadae.


Si tunajua, kuwa Obote alikuwa na ugomvi na chama cha KY- Kabaka Yekka. Hivyo basi, alikuwa na ugomvi na Mfalme Fredrick Kabaka na WaBaganda. Katiba mpya ikampa nguvu nyingi Obote na UPC yake- Chama chake. Kabaka na WaBaganda walimtambua haswa Obote. Aliwanyanyasa kwa kuwafunga na hata kuwaua. Ndio, aliwanyamazisha, kwa muda.


Lakini naye, Obote, hakubaki salama. Idi Amin akaja akampindua na kushangiliwa sana na WaBaganda wa Kampala na kwengineko. Kosa alilofanya Obote ni hili; kubadilisha Katiba kukidhi mahitaji yake na ya Chama chake katika wakati uliokuwepo. Obote hakuiangalia Uganda ya miaka 50 hadi 100 iliyofuata. Na hilo ndilo tatizo la viongozi wetu wengi Afrika.


Tukirudi hapa kwetu, kwa kuusoma Muswaada ule wa sheria inatoa tafsiri hii; kuwa ndani ya saa 96 zilizopangwa za kupokea maoni ya wadau zitakuwa zimeweka msingi wa Watanzania kupatiwa Katiba Mpya wasiyoitaka, lakini, itakuwa imehalalishwa, kwa taratibu za Kibunge.



Kwani, haitarajiwi Wabunge wa CCM walio wengi kuukwamisha Muswaada huo. Na ikitokea wakafanya hivyo, kwa maana ya Wabunge hao wa CCM wakaukwamisha Muswaada huo wa sheria, basi, Wabunge hao wa CCM watakuwa wameanza kazi ya ’ Chama kujivua magamba’ na baadhi yao kunusurika na adhabu ya wapiga kura ifikapo 2015.


Ni ukweli, kuwa Nchi yetu iko njia panda. Mbele yetu kuna njia mbili; moja inaelekea tunakopita sasa. Kwenye hali ya ’ kujifunga’ na kubaki tulipo bila kupiga hatua za haraka za maendeleo huku baadhi, wakiwamo viongozi, wakiwa na udhibiti mkubwa wa hali ya mambo. Njia nyingine inaelekea kwenye uhuru zaidi wa wananchi na uwezo wa kuwadhibiti na kuwawajibisha viongozi wao. Ni njia inayoelekea kwenye ustawi wa nchi.

Watanzania tuna kiu kubwa ya kuianza safari ya kuipita njia ya pili. Njia yenye uhuru zaidi na matumaini ya ustawi wa taifa. Njia itakayotufanya tuondokane kabisa na njia ya kwanza, njia inayotufunga na kutubakisha hapa tulipo.
Kwa viongozi watakaochangia kutupitisha kwenye njia ya kwanza, nahofia, kuwa hao watakumbukwa kwa dhamira yao hiyo mbaya kwa Watanzania.


Kwa wale viongozi watakaochangia katika kutupitisha kwenye njia ya pili, basi, hao hawatasahaulika mioyoni mwa Watanzania. Watakuwa ni wanadamu walioamua kuachana na ubinafsi na kutanguliza maslahi ya taifa. Ni imani yetu, kuwa hata Wabunge wengi wa CCM wanaweza kuingia katika kundi la viongozi hao. Kutupitisha kwenye njia ya pili.


Na kama Bunge letu litabariki azma ya Serikali kuendelea kutupitisha katika njia hii ya kwanza kwenye mchakato huu wa Katiba, basi, ni dhahiri, kuwa tuendako kuna giza zaidi kulipo hapa tulipoanzia. Kuna watakaoikumbuka Katiba yetu ya sasa.


Na hiki ni kipindi kigumu sana Nchi yetu inakipitia tangu tupate Uhuru wetu.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.


Maggid,
Dar es Salaam
Ijumaa, Aprili 8, 2011

No comments:

Post a Comment