Wednesday, June 29, 2011
SIMBA YAIFUNGA OCEAN VIEW 1-0
SIMBA imezinduka na kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Zanzibar Ocean View katika mechi ya michuano ya Kombe la Kagame iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Amir Maftah aliipatia Simba bao hilo la ushindi katika dakika ya 22 kwa shuti kali la umbali wa mita 28 na mpira kujaa wavuni moja kwa moja.
Bao hilo la Maftah lilikuwa ni kama kusawazisha makosa yake baada ya kukosa bao la
penati katika dakika ya nane ya mchezo huo.
Penati ilitolewa na mwamuzi Sylvester Kirwa wa Kenya baada ya Mussa Hassan Mgosi kuangushwa eneo la hatari na mlinzi mmoja wa Ocean View.
Ushindi huo kwa Simba ni ahueni kwao na mashabiki wao baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika mechi ya kwanza dhidi ya Vital ‘O’.
Katika mechi hiyo ya jana, Simba ilitawala zaidi kipindi cha kwanza, ambapo Athumani Iddi
‘Chuji’ anayeichezea Simba kwa mara ya kwanza tangu ajiunge nayo akitokea Yanga kutokana na kuzomewa na mashabiki wa Yanga.
Chuji alibadilishwa dakika ya 58 na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Banka. Kipindi cha pili Simba ilianza mchezo kwa kasi na kukosa mabao kadhaa.
Katika dakika ya 45, Haruna Moshi Boban alichelewa kuunganisha krosi ya Mgosi na kukosa bao la wazi.
Ocean View pamoja na kushindwa kuhimili mikikimikiki ya Simba, walipata nafasi chache za kufunga, dakika ya 20, mabeki wa Simba walijichanganya lakini Walulya Derrick alirekebisha makosa na kuokoa.
Matokeo hayo yameifanya Simba ifikishe pointi nne nyuma ya Ocean View inayoongoza
kundi kwa kuwa na pointi sita.
Simba sasa inahitaji ushindi katika mechi zilizosalia ili ifike hatua ya robo fainali.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa Ocean View, Abdulfatah Abbas alimlalamikia mwamuzi
kuwa aliipendelea Simba.
Michuano hiyo inaendelea tena leo ambapo mabingwa soka Tanzania Bara, Yanga watashuka
dimbani kumenyana na Elman ya Somalia.
Yanga inahitaji ushindi katika mechi hiyo ili kufufua matumaini ya kucheza robo fainali baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na El Merreikh ya Sudan katika mechi ya kwanza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment