WAMILIKI wa vyombo vya usafiri vya moto kuanzia keshokutwa watajisikia afueni baada ya utekelezaji wa mabadiliko ya bei ya nishati ya mafuta kuanza.
Hatua hiyo inatokana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Ewura) jana kutangaza kushuka kwa bei ya mafuta jamii ya petroli na dizeli.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, kuanzia siku hiyo, bei ya dizeli itapungua kwa Sh 215 kwa lita huku ya petroli ikisubiri nayo kushuka kwa kiwango ambacho hakikutangazwa jana.
Lakini wakati hali ni hiyo kwa mafuta hayo,ya taa yatapanda kwa Sh 385, ambapo Masebu aliongeza kuwa, ifikapo Agosti Mosi bei ya mafuta hayo inatarajiwa kushuka zaidi ili kutoa nafuu kwa mtumiaji.
Masebu, alisema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano wa wadau wa mafuta na kutaka bei hizo mpya zifuatwe na kuheshimiwa.
Alisema, pia bei ya petroli itapungua na kiwango chake kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa baada ya kukamilika ukokotoaji wa tozo zilizopunguzwa, huku akionya kuchukua hatua za kisheria kwa watakaokiuka agizo hilo la kushusha bei.
“Lengo la mkutano wa leo (jana) ni kuwaeleza wadau wa mafuta kuhusu mambo yaliyotokea Dodoma, ambayo yamesababisha sisi Ewura kama wadhibiti, kuwatangazia kuwa kutokana na punguzo la kodi katika mafuta na nyongeza katika mafuta ya taa, bei mpya ya bidhaa hizo itaanza rasmi Julai mosi,” alisema Masebu.
Alisema, kwa sasa kinachosubiriwa ni kusainiwa kwa Sheria ya Fedha yenye makubaliano hayo yaliyopitishwa na Bunge.
Kutokana na mabadiliko hayo, Masebu alisema, tofauti ya bei ya dizeli na mafuta ya taa itakuwa Sh. 15 kwa lita, kwa maana ya mafuta ya taa kuuzwa kwa bei ya chini ya dizeli kwa kiwango hicho ili kuzuia uchakachuaji.
Bei ya zamani ya bidhaa hizo mbili kwa mujibu wa Masebu, mafuta ya taa yaliuzwa kwa bei nafuu pungufu ya Sh. 400 ikilinganishwa na ya dizeli na kusababisha baadhi ya mafuta yaliyokuwa yakiuzwa nchini kuchakachuliwa.
Alisema, pia upo mchakato wa kukokotoa tozo zingine kwa ajili ya kuzipunguza, ili kuifanya bei ya mafuta hayo jamii ya petroli kuwa nafuu zaidi na Agosti mosi, punguzo kubwa linatarajiwa kuanza rasmi kutumika.
Akizungumzia mfumo wa kuweka vinasaba katika mafuta, Masebu alisema, umepitishwa rasmi kutekelezwa nchini ili kudhibiti wafanyabiashara wadanganyifu wanaosingizia kusafirisha mafuta nje ya nchi na baadaye kuyauza nchini ili kukwepa kodi.
“Tumeamua kuwataarifu kuwa mfumo huu wa ‘fuel marking’ tunaendelea nao na tangu uanze, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeongeza mapato yake kutokana na magari mengi kukamatwa, yakifanya udanganyifu na kupigwa faini,” alisema.
Pia mfumo huo umesaidia TRA kupata mapato yaliyokuwa yakivujishwa kwa kukwepa kodi.
Kuhusu mfumo wa uingizaji mafuta kwa pamoja, Masebu alisema, Serikali imekamilisha michakato yote ikiwa ni pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kusaini kanuni za mfumo huo na kuzichapisha katika Gazeti la Serikali toleo namba GN 164 la Juni 3.
Kanuni hizo kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, zimetoa wajibu mkubwa kwa wadau wa mafuta zikiwamo taasisi na kampuni za mafuta, ambazo zimetakiwa kuunda Kamati ya Uratibu na Bodi ya Wakurugenzi, katika miezi mitatu ijayo, ili mfumo huo uanze kutekelezwa.
Alisema, vyombo hivyo viwili pamoja na Ewura kuwa msimamizi na mdhibiti, vitasimamia masuala ya zabuni.
“Mfumo huu tunatarajia utasaidia kupunguza gharama kubwa za mafuta, kwa kuwa utashindanisha kampuni za mafuta na hivyo bei itapungua, suala hili sasa si hadithi, bali ndiyo ukweli wenyewe,” alisema.
Wakati akiwasilisha Bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, alisema, katika jitihada za Serikali za kupunguzia mzigo wa gharama za maisha wananchi, imeamua kupunguza baadhi ya kodi za mafuta ili bei ya bidhaa hiyo ipungue.
Akiwasilisha muswada wa Sheria ya Fedha kwa mwaka 2011, Naibu Waziri wa Fedha, Pereira Silima, alisema Serikali imeongeza ushuru wa bidhaa kwa mafuta ya taa kutoka Sh. 52 hadi Sh 400.30 pamoja na mambo mengine, lengo ni kudhibiti uchakachuaji wa mafuta nchini.
Upunguzaji huo wa bei za mafuta, pia una lengo la kudhibiti mfumuko wa bei, ambao umekuwa ukisababishwa na bidhaa hizo kutokana na umuhimu wake katika bidhaa na huduma za kijamii.
No comments:
Post a Comment