Mbunge wa Kawe Halima Mdee, CHADEMA, aliyeuliza leo Bungeni swali la msingi kuhusu Development Entrepreneurship for Community Initiative, DECI, na maswali ya nyongeza, amempa wakati mgumu Naibu Waziri wa Fedha, Gregory Teu, wakati alipotakiwa aeleze hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu maofisa wa DECI walioshindwa kutekeleza wajibu wao hadi DECI ikafanya shughuli zake kinyume cha sheria.
Katika maswalic yla nyongeza, Mdee alisema, DECI ilifanya shughuli zake kwa miaka mitatu za kuchukua amana za wananchi bila kuwa na kibali cha kufanya hivyo, je, “Serikali inatoa kauli gani juu ya maafisa wake ambao walikuwa wanajua suala hilo lakini hawakuchukua hatua zozote?" na "kwa kuwa fedha zinazoshikiliwa ni za wanachama na waliofanya uhalifu huo ni watu watano, na kwa vile thamani ya fedha inashuka kwa nini wanachama ambao hawakuwahi kuvuna hata mara moja wasikabidhiwe fedha hizo?"
Ndipo Teu aliposema, “Fedha zinazodaiwa na wanachama ni nyingi wakati fedha zilizoko kwenye akaunti za wakurugenzi ni kidogo.”
Baada ya kujibu hivyo alienda kukaa, ndipo Spika akamkumbusha kuwa hajajibu sehemu nyingine ya swali kuwa maofisa wa Serikali ambao walizembea hadi DECI wakaendesha shughuli zao kinyume cha sheria wamechukuliwa hatua gani?
Teu akarudi kwenye eneo la kujibia mwaswali na kusema “Nafikiri walikuwa bado hawajaandikishwa,” kauli iliyosababisha Wabunge wengine kuangua kicheko.
Awali akijibu swali la msingi la Mdee, Teu alisema Serikali haijachukua fedha za DECI bali fedha hizo, Shilingi bilioni 14.81 zimezuiliwa katika akaunti zilizomilikiwa na wakurugenzi wa DECI katika benki mbalimbali nchini.
Katika swali lake, Mdee alitaka kufahamu hatma ya fedha za wananchi. Alisema fedha hizo ni asilimia 37.77 ya ambazo zinadaiwa na wanachama wa DECI ambazo ni Shilingi bilioni 39.3/=, na uamuzi wa kuzizuia uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiwa ni hatua mojawapo ya uchunguzi dhidi ya Deci ambayo ilikuwa inaendesha mchezo wa upatu.
“Napenda kuliarifu Bunge lako kuwa kesi ya DECI iliyofunguliwa mwaka juzi katika mahakama ya Kisutu inaendelea kusikilizwa,” alisema Teu na kuongeza, “Hivyo hatma ya fedha hizo za wananchi itategemea hatma ya kesi hiyo kwani Deci ilikuwa na matawi 40 katika mikoa 18 ya Tanzania Bara”.
Alisema, usikilizwaji wa mashahidi wa Dar es Salaam umekamilika na hatua za kuwapata mashahidi kutoka mikoa mingine zimeanza. Alisema, DECI ilikuwa na wanachama 649,859 na sehemu ya wanachama hao watahitajika kutoa ushahidi mahakamani.
No comments:
Post a Comment