Pages

Wednesday, June 29, 2011

Anayetuhumiwa kutapeli mil. 218/- za magari anatafutwa

POLISI Mkoa wa Temeke, inamtafuta Mtanzania anayeishi nchini Japan, Hassan Omary (30) kwa tuhuma za utapeli wa zaidi ya Sh. milioni 218 na kutoroka mara baada ya kuachiwa kwa dhamana.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, David Misime aliliambia gazeti hili jana kuwa, Omary anayejishughulisha na biashara nchini Japan, anatuhumiwa kuwatapeli Watanzania baada ya kuwaahidi kuwa angewaletea magari.

Kwa mujibu wa Misime, awali Omary alikamatwa Juni 23, mwaka huu Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam wakati akijiandaa kurudi Japan.

Kamanda Misime amesema, Omary alipelekwa katika kituo kidogo cha Polisi uwanjani hapo na baadaye alihamishiwa kituo cha Polisi Chang’ombe wilayani Temeke.

“Usiku huo alishikiliwa hapa na kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo na aliachiwa kwa dhamana kwa masharti ya kutakiwa kurudi siku inayofuata kuendelea na mahojiano na utaratibu mwingine wa kisheria,” amesema Misime.

Kamanda Misime amesema, cha kushangaza siku iliyofuata, mshitakiwa huyo hakufika kituoni hapo na baadaye walipata taarifa kuwa ametoroka nchini.

Hata hivyo Kamanda huyo amesema, suala la kutoroka nchini halina ukweli wowote na ana uhakika kuwa mtuhumiwa huyo bado yupo nchini.

“Tunaendelea kumtafuta na hata kama kweli atakuwa ametoroka, tutatumia njia zingine kumpata ikiwemo askari wa Interpol (Shirika la Kimataifa la Polisi), ili aje kujibu tuhuma za utapeli zinazomkabili na za kutoroka dhamana yake,” ameongeza Misime.

Omary anatuhumiwa kutapeli kiasi hicho cha fedha kwa walalamikaji wawili waliotambulika kwa jina moja moja la Titus na Philemon kwa kuwadanganya kwamba angewaletea magari na matrekta.

Kamanda Misime amesema, mshitakiwa atakapokamatwa, wataangalia afunguliwe kesi ya aina gani; ya madai au jinai na kuongeza kuwa tayari wameweka mitego sehemu mbalimbali ili kumkamata.
habari leo

No comments:

Post a Comment