Wahenga hawakukosea waliponena kuwa kabla hujafa hujaumbika, mwanaume huyu wa nchini Vietnam, anaomba msaada toka kwa wasamaria wema ili aweze kufanyiwa operesheni ya kuuondoa uvimbe kwenye mguu wake wenye uzito wa kilo 80 na urefu wa mita moja.
Kijana Nguyen Duy Hai wa nchini Vietnam, hawezi kufanya kitu chochote zaidi ya kukaa chini au kujilaza kwani uvimbe kwenye mguu wake umekuwa mzito sana kiasi cha kufikia uzito wa kilo 80 hivyo kuunyanyua mguu wake ni sawa na kuzinyanyua kilo 80 toka chini.Uvimbe huo ambao hautokani na kansa uliopo kwenye mguu wake wa kulia, unachukua nafasi yenye urefu wa mita moja kiasi cha kuingia kwenye rekodi ya uvimbe mkubwa kuliko yote iliyowahi kurekodiwa nchini Vietnam.
Uvimbe kwenye mguu wa Nguyen ulianza alipokuwa na umri wa miaka 14, ambapo ulipozidi kuwa mkubwa ulipelekea kukatwa kwa mguu wake lakini umeendelea kukua kila miaka ilivyoenda na hivi sasa Nguyen akiwa na umri wa miaka 31 hawezi tena kufanya chochote zaidi ya kulala au kukaa.
Umaskini wa familia yake ndio sababu ya Nguyen kushindwa kwenda hospitali kufanyiwa operesheni ya kuondolewa uvimbe huo.
Kilio chake cha kuomba msaada toka kwa wasamaria wema duniani kimepelekea habari kuhusiana na uvimbe wake kusambaa haraka kwenye vyombo vya habari duniani.
Nguyen anatumaini kuna mtu atajitokeza kulipia gharama za matibabu yake hivyo kumuondolea mzigo mama yake mwenye umri wa miaka 61 ambaye hivi sasa ndiye anayemuuguza wakati wote.
No comments:
Post a Comment