SERIKALI imesema, uchunguzi wa awali umebainisha kuwa watu 24 waliopoteza maisha na wengine kubabuka ngozi baada ya kuoga kwenye Mto Tigithe wilayani Tarime, hawakuathirika kutokana na kemikali kutoka Mgodi wa North Mara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa wakati akihitimisha mjadala wa ofisi yake, alisema uchunguzi umebanisha kuwa watu hao walipata madhara kutokana na kemikali ya Zebaki ambayo haitumiwi na mgodi huo.
"Mgodi wa North Mara hautumii Zebaki lakini watu wa pale kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia Zebaki kwenye uchimbaji wa dhahabu. Hata hivyo uchunguzi unaendelea na taarifa yake tutaiwasilisha hapa," alisema.
Waziri huyo alisema, wamekuwa wakishindwa kusimamia ipasavyo sheria kwenye migodi inayoharibu mazingira kutokana na kuwa na wataalamu wachache, vifaa vichache na fedha wanazopewa kutotosha.
Akizungumzia maji machafu yanayotoka kwenye Hosteli za Mabibo jijini Dar es Salaam na kuharibu mazingira na kutoa harufu kali, alikiri kuwepo tatizo hilo na kubainisha kuwa suala hilo wameshaitaarifu NSSF kwa hatua zaidi.
Awali akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) aliitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya waliojenga majengo ya Shoppers na Mayfair Plaza jijini Dar es Salaam, majengo ambayo yamezuia mkondo wa maji na matokeo yake wakazi wa bonde la Mpunga, Msasani wanapata taabu mvua zinaponyesha.
Mbunge huyo alilieleza Bunge kuwa, Kawe darajani kwenye mto kuna mtu aliyemtaja Robert Mugisha ameanza ujenzi wa nyumba na analindwa na kigogo wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwani ameonesha kiburi cha kuendelea na ujenzi licha ya kupewa zuio la kisheria.
Imeandikwa na Maulid Ahmed,Habari leo
No comments:
Post a Comment