Gazeti moja la Urusi limesema leo kuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi yuko tayari kuacha madaraka , lakini anataka kupatiwa uhakika wa usalama wake likiwanukuu maafisa wa juu wa Urusi.
Ripoti hiyo katika gazeti linalosomwa na watu wengi nchini Urusi la Kommersant, ambalo hata hivyo halikutaja vyanzo vya vyake hivyo, inakuja siku moja baada ya harakati za utafutaji wa njia za kumaliza vita nchini Libya zikichukua nafasi kubwa katika mazungumzo baina ya Urusi na katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen pamoja na rais wa Afrika kusini Jacob Zuma.
Kanali Muammar Gaddafi anatoa ishara kuwa yuko tayari kuachia madaraka lakini kwanza anataka apate uhakikisho wa usalama wake, gazeti la Kommersant limenukuu kile ilichokiita duru za ngazi ya juu katika uongozi wa Urusi.
Duru hizo zimeeleza katika ripoti kuwa mataifa mengine, hususan ikiwa ni pamoja na Ufaransa , ziko tayari kutoa uhakika huo.
Ripoti hiyo ya gazeti la Kommersant , pia imesema kuwa Gaddafi anataka mtoto wake Saif al-Islam aruhusiwe kugombea iwapo yeye atajiondoa kutoka madarakani , sharti ambalo waasi huenda wasilikubali.
Serikali ya Libya imesema jana Jumatatu kuwa ilikuwa katika mazungumzo na viongozi wa upinzani, lakini upande huo umeshikilia msimamo wake juu ya hatima ya Gaddafi.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika kusini Maite Nkoana-Mashabane alipokutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle jana amesisitiza kuwa suluhisho la kisiasa ni muhimu katika mzozo wa Libya.Bildunterschrift: Mtoto wa kanali Gaddafi , Saif al-Islam ambaye baba yake anataka aruhusiwe kugombea urais.
"Wote tunakubaliana kuwa kile kitakachoisaidia Libya ni suluhisho la kisiasa na sio kijeshi.Wakati nikuzungumza nanyi hivi sasa rais Zuma amepewa mamlaka na umoja wa Afrika kujiunga na rais Medvedev katika mkutano mjini Sochi ambao pia unaendelea kuliangalia suala hili."
Kiongozi wa upinzani nchini Libya anatarajiwa wakati huo huo kufanya mazungumzo mjini Ankara Uturuki leo, muda mfupi baada ya nchi hiyo kulitambua baraza la taifa la mpito lililoundwa na waasi likipambana na utawala wa kanali Muammar Gaddafi, ameeleza afisa wa ngazi ya juu wa Uturuki.
Mwenyekiti wa baraza la taifa la mpito nchini Libya Mahmud Jibril alipokutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle
Mahmud Jibril , ambaye anahusika na masuala ya mambo ya kigeni katika baraza hilo la taifa ,TCN, lililo na makao yake katika ngome ya waasi mjini Benghazi, anatarajiwa kuwa na mazungumzo ya pande tatu na waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Ahmet Davotoglo na mwenzake kutoka umoja wa falme za Kiarabu UAE, Sheikh Abdullah bin Zayed al-Nahayan.
Mazungumzo hayo yana lenga katika kutayarisha mkutano wa kile kinachojulikana kama kundi la kimataifa linaloshughulikia Libya, unaotarajiwa kufanyika Julai 15 hadi 16 mjini Istanbul.
Wakati huo huo waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague jana alimsisitizia rais wa halmashauri ya umoja wa Afrika Jean Ping kuwa kundi hilo la mataifa linajukumu muhimu katika kutatua mzozo wa Libya wakati walipokutana kwa mazungumzo mjini London.
Uingereza ni moja kati ya nchi zilizo mstari wa mbele katika kampeni ya mashambulizi ya NATO dhidi ya kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, lakini operesheni hizo hazijaweza kuvuta uungwaji mkono mkubwa kutoka mataifa yanayoizunguka nchi hiyo ya Afrika kaskazini.
Dw.
No comments:
Post a Comment