MBUNGE wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi (CCM), ameitaka Serikali kutoa sehemu ya faida ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni Kisangi aliitaka Serikali kutoa sehemu ya faida za aonesho hayo, ili zitumike angalau kununua madawati kwa shule za Manispaa hiyo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu alisema Serikali itayaendeleza maonesho hayo, lakini haina mpango wa kutoa gawio hilo.
Naibu Waziri huyo alisema pamoja na kwamba Serikali haina mkakati wa kutoa gawio hilo, lakini maonesho hayo yamekuwa yakisaidia kutoa ajira kwa wakazi wa Dar es Salaam wakiwamo wa Manispaa ya Temeke.
Alifafanua kuwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade), hupata fedha za maonesho hayo kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo kiingilio cha magari na watu mbalimbali wakati wa maonesho.
Mapato yote kwa mujibu wa Nyalando, hukatwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Majengo ambazo huchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya nchi ikiwemo Wilaya ya Temeke.
Alitoa takwimu za mapato hayo zilizoonesha kuwa mwaka 2005/2006 mapato yalikuwa Sh bilioni 1.02 na matumizi yalikuwa Sh milioni 461 na ziada ilikuwa Sh milioni 560.
Takwimu hizo zilionesha kuwa katika maonesho ya mwaka jana, mapato yaliongezeka na kufikia Sh bilioni 1.8 na matumizi yakaongezeka na kufikia Sh bilioni 1.3, lakini ziada ikapungua na kuwa Sh milioni 547.
No comments:
Post a Comment