Pages

Monday, May 2, 2011

Tafakuri Yangu ya Leo; Popote Ulimwenguni Ambapo Masikini Waliowengi Hawakusikilizwa Basi Imesikika Milio Ya Risasi Na Mabomu!

   “A Hungry Man Is Always An Angry Man”….Bob Marley(1945-1983)

  Haya ni maneno ya kifalsafa yaliyowahi kutamkwa na gwiji wa muziki wa Reaggae hayati Robert Nestar Marley maarufu kama Bob Marley nayaita maneno ya kifalsafa kwasababu yalilenga kwenye Ulimwengu halisi aishio mwanadamu , kwa maana ya Kiswahili kauli hii yaweza kusemwa kuwa “mtu mwenye njaa mara zote huwa na hasira”
   Hili halina ubishi hata kidogo ingawaje ukweli ni kuwa mara nyingi kauli za kifalsafa huwa hazina maana moja hivyo najua wapo baadhi ya watu watanipinga kwenye hili nakuibua tafsiri zao nasema hewala na natanguliza shukrani zangu kwao kwa maana binadamu tumeumbwa tofauti hivyo wanatimiza haki yao ya msingi ya kufikiri lakini kwangu mimi naungana na maana iliyotolewa na legend huyu wa reaggae.
    Jana asubuhi nimemsikia Bw Gracian Mukoba ambaye ni mwenyekiti wa chama cha walimu Tanzania akizungumza kupitia kituo kimoja cha redio jijini Dar es salaam Bw Mukoba alinukuliwa akisema “hata hela ya chakula bado haijatosha kwa walimu, mwalimu anatoka nyumbani hajanywa chai kisha mtoto wake karudishwa nyumbani anadaiwa ada na duka la jirani mwalimu anadaiwa kwasababu alikopa ili mwisho wa mwezi alipe hata hivyo mshahara wake bado mdogo sana kukidhi haya yote, halafu mwalimu huyu anenda darasani kufundisha, hivi tutegemee ni nini kutoka kwa mwalimu huyu?”
    Naam! Hizi ni zama za kuambiana ukweli , hivi mara ngapi walimu wamelilia nyongeza za mishahara? Nani anawasikiliza? Kwanini hawasikilizwi? Viongozi wahusika na serikali naomba wajibu maswali yafuatayo ambayo yanawahusu watanzania masikini walio wengi kwenye nchi hii;
1.      Hivi serikali inafaidika nini wananchi wake wanapoishi kwenye lindi la ufukara na umasikini wa kutisha?
2.      Hivi watoto wetu kwenye shule za kata wataendelea kufeli mitihani mpaka lini?
3.      Hivi serikali inaona sawa jinsi wazungu wanavyoendelea kupora maliasili zetu kama madini huku mtanzania anazidi kudidimia kwenye umasikini wa kutisha?
4.      Hivi viongozi wetu wanafaidika nini na kuharibika kwa maadili miongoni mwa vijana? Wengi wakiwa wasikilizaji wa bongo flava hawapendi kujifunza mambo wala utamaduni wao, serikali kwanini haina program maalumu ya malezi ya vijana?
5.      Hivi serikali ya rais Kikwete kwanini bado haijatimiza yale yote iliyoahidi walau robo yake tu? hivi Mheshimiwa rais Kikwete anajisikia furaha gani wananchi wake wanapoulizia mambo aliyowaahidi?
6.      Hivi serikali inafaidika nini matabaka yanapoongezeka kila uchao? Tabaka la walionacho na wasio nacho yana faida gani kwa serikali? Kwanini masikini ndiyo wengi?
7.      Viongozi wa serikali wanafaidika nini na mgao wa umeme? Kwanini mpaka leo tatizo la umeme linaendelea? Au Mheshimiwa rais Kikwete alivyoahidi kujenga barabara za juu(fly-overs) halafu mpaka leo msongamano wa magari unaendelea jijini Dar rais alimaanisha nini kuahidi jambo hili?
8.      Serikali inafaidika nini na malumbano yanayotengenezwa kwa makusudi? Mfano hii rasimu mbovu ya mapendekezo ya katiba mpya ambayo watu hawaitaki kwanini serikali inang’ang’ania? Kwa faida ya nani? Au kwanini swala la muungano kujadiliwa linazuiwa kwa faida ya nani? Na litazuiwa mpaka lini? wananchi wanautaka muungano ila wanataka kuujadili serikali inapopiga chenga ina maanisha nini?
9.      Hivi uwekezaji usio nufaisha wananchi utaendelea mpaka lini? mpaka lini mapigano ya kugombea ardhi kama ya Mbarali yataendelea? Na haya yanamfaidisha nani?
10.  Lini serikali itajifunza kusikiliza wananchi wake? Lini serikali itawalinda wanahabari wa nchi hii ambao wanayumbishwa kwa rushwa na ubabe kila uchao kiasi kwamba wanashindwa kusema ukweli, je wao wasiposema kwa niaba ya wananchi nani atasema? Au lini basi viongozi wa dini wa nchi hii hawatakaripiwa bila aibu na wanasiasa uchwara pale viongozi hao wa dini wanapokosoa ubabaishaji wa serikali?

Naam! Nauliza hivi kwasababu naona viongozi wamelala usingizi wa pono, wao hawashtuki kwanini watanzania masikini wanamlilia Nyerere kila uchao? Hawajui kuwa hii si dalili njema hata kidogo, kwa maana nyingine wananchi wamekata tamaa kwasababu hawasikilizwi ndiyo maana kilasiku wanamkumbuka Nyerere.
   Lakini katika mkanganyiko huu kuna ukweli wa kihistoria kuwa popote ulimwenguni masikini walio wengi wasiposikilizwa basi hapo milio ya mabomu na risasi husikika, ndiyo hata Tunisia wanyonge hawakusikilizwa sihitaji kusema nini kilitokea? Pia Misri wanyonge walipuuzwa na sisi wote ni mashahidi ya kilichotokea kule, hofu yangu mimi si huu ukweli wa kihistoria HAPANA hofu yangu kubwa ni tabia ya historia kujirudia, hii ndiyo hofu yangu kubwa na hii ni kanuni haiwezi kupingwa na kwa bahati mbaya si kanuni yangu mimi Nova Kambota bali ya kihistoria!  Naam! Iwe usiku au mchana siku ya wafanyakazi au wakulima serikali ijihoji itaendelea kupuuza wananchi mpaka lini? lakini isiishie hapo bali pia ijiulize kwa kiasi gani imejipanga kukabiliana na ukweli huu wa kihistoria?

Kitendawili si deni ukishindwa nipe mji,
Kwa wanataaluma kutofautiana kimawazo si kosa bali ni dalili ya jamii iliyo hai,
Nova Kambota Mwanaharakati,
Nipigie; 0717-709618(Tanzania) au +255717-709618(Nje ya Tanzania)
Kwa maoni na ushauri niandikie;
Kwa habari zaidi za kitafiti na uchambuzi tembelea Blog yangu;
Tanzania, East Africa,
Jumatatu, Mei 2,  2011.

No comments:

Post a Comment