Monday, May 23, 2011
HUKUMU YA EPA
Habari zinasema imetangazwa katika taarifa ya habari mchana huu, Radio One Stereo kuwa watuhumiwa wawili wa kesi ya kwanza ya wizi wa fedha kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ndugu wawili, Rajabu Maranda na Farijala Hussein imetolewa na wamehukumiwa kwenda jela miaka 5 na kuilipa Serikali fedha iliyoibwa la sivyo, mali zao zitafilisiwa kwa mujibu wa sheria.
Jopo la mahakimu watatu ndilo lililotoa hukumu hiyo ambayo awali ilikuwa na jumla ya miaka 21 lakini kwa kuwa watatumikia adhabu hizo kwa wakati mmoja, basi ikaamriwa kuwa watatumikia miaka 5 kila mmoja.
Mahakimu hao ni Ilvin Mgeta, Saul Kinemela na Focus Bambikye na waliitoa hukumu hiyo katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, baada ya watuhumiwa kupatikana na hatia.
Awali, watuhumiwa walikuwa wakikabiliwa na mashitaka 8 lakini walikutwa na hatia katika mashitaka 6 miongoni mwao yakiwemo ya kughushi na kuwasilisha hatia za uongo ambazo ziliwapatia ingizo la shilingi bilioni 1.8 mali ya BoT kwa njia ya udanganyifu wakonyesha kuwa, Kampuni ya Kiloloma and Brothers imepewa idhini ya kukusanya deni la kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai, India.
Mojawapo ya makosa yaliyofutwa ni lile la kula njama kwa nia ya kutenda kosa na wizi.
Wakili Mkuu wa Serikali Boniface Stanslaus aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa kwa kuzingatia kiasi kikubwa cha fedha kilichochukuliwa na madhara yaliyotokea kwa wananchi.
Wakili wa watuhumiwa, Majura Magafu, amesema wateja wake wanakata rufaa.
Maranda na Hussein wanakabiliwa na kesi nyingine tatu za EPA, zikiwa ni miongoni mwa kesi kadhaa za EPA zilizofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu. Kesi hizo zinawakabili wafanyabiashara maarufu na waliokuwa watumishi wa BoT.
Farijala Hussein na Rajabu Maranda
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment