Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Temeke,
Joseph Yona (32), ametekwa nyara na kujeruhiwa vibaya kwa kipigo kisha kutupwa
katika vichaka eneo la Tegeta Ununio, wilayani Kinondoni a watu wasiojulikana.
Yona ambaye alitekwa juzi akiwa katika eneo la Mtoni kwa Aziz
Ali, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Yona ambaye pia ni Mjumbe
wa Baraza Kuu la Chadema alisema jana kwamba alitekwa yapata saa 5.00 usiku wa
kuamkia jana na watu ambao awali, walijitambulisha kuwa ni polisi.
“Tulikuwa tumekaa na vijana wanne wa Tawi la Ukombozi, Chadema
la Temeke, ndipo ghafla wakajitokeza watu kama sita hivi wakaja moja kwa moja
na kuninyanyua huku wakiniambia twende kituo cha polisi,” alisema.
Alisema baada ya kuingia ndani ya gari ambalo lilikuwa
linafanana na yale ya polisi alivuliwa fulana na kufungwa macho na mikono.
Alisema baada ya mwendo uliochukua kitambo kidogo, gari hilo
lilisimamishwa na watu hao wakamshusha chini na kumpeleka sehemu iliyokuwa na
bonde huku wakiendelea kumpiga kabla ya kumtelekeza na kutoweka.
“Njiani nilijaribu kuwasihi wasiniue kwa kuwa nina watoto wadogo
wawili ambao wananihitaji, niliwasisitiza watambue na kwamba nao wana watoto
wafikirie, wakaniuliza kwa nini naivuruga Chadema kwa tamko nililolitoa hivi
karibuni kutokana na mgogoro unaoendelea,” alisema.
Alisema kuwa alijitetea kwa kuwataka wakasome vizuri tamko lake,
lakini waliendelea kumpiga na kumtaka aombe msamaha kwa kuishambulia Kamati Kuu
ya chama hicho, jambo ambalo hakuwa tayari kulifanya kwa kuwa hakuona kama kuna
kosa alilolifanya.
“Walinitupa na kutimua mbio wakiniacha nikiwa na maumivu makali.
Nilitulia kwa muda na kujitahidi kuinuka na kupiga hatua kwenda nyumba
zilizokuwa jirani kuomba msaada, hapo sikuwa na simu wala nauli,” alisema.
Alisema kuwa alipata msaada wa fulana na kuwasiliana na ndugu
zake na polisi ambao baada ya muda walifika na kumpeleka Muhimbili kwa
matibabu.
Hivi karibuni, Yona alitoa tamko la kupinga hatua ya Zitto
kuvuliwa nyadhifa zake na Kamati Kuu ya chama hicho.
Kova aunda jopo la uchunguzi
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
alisema jana kuwa ameunda jopo la wapelelezi wanane watakaoongozwa na Mkuu wa
Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP),
Jaffari Mohamed kuchunguza tukio hilo.