HERIETH MAKWETTA
HISTORIA ya makundi ya muziki wa kizazi kipya ya Wanaume Halisi na Wanaume Family, si rahisi kusahaulika kirahisi akilini mwa wapenzi wa muziki huo Afrika Mashariki.
Ni kwasababu yaliyokana na kundi moja lililokuwa na nguvu kubwa, hata lililipomeguka bado kila upande ulishika chati.
Mgawanyiko wao ulitokea mwaka 2009 baada ya Juma Kassim 'Sir Nature' kujiondoa katika kundi la TMK Wanaume Family na kuunda TMK Wanaume Halisi, alijiengua na wengine kadhaa.
Kundi hilo lilijipatia sifa na umaarufu baada ya kuibuka na albamu yake ya kwanza, inayoitwa �Tatu Bila�. Lakini kabla ya mwaka kuisha kundi la Wanaume Halisi lilivunjika tena baada ya uongozi wake kuwatema wasanii saba na kubaki na watano.
Nature anasema uamuzi huo ulitokana na matakwa ya wadhamini wapya ambapo waliingia nao mkataba, nao ni kampuni ya DLC inayofanya kazi zake katika nchi za Tanzania na China.
Kampuni hiyo ilikuwa ikisimamia kazi zote za kundi hilo, ikiwa ni pamoja na kulitangaza ndani na nje ya nchi na kuliandalia maonyesho.
�Tulipata wakati mgumu sana katika kuchuja vichwa 12 vilivyomo ndani ya kundi ili kubaki na vitano," anasema Sir Nature.
Mbali na yeye wengine wanne waliobaki kundini ni Dolo, Baba Levo, JB wa Mabaga Fresh na KG Son.
Waliochujwa nao wakaamua kuanzisha kundi lao lililofahamika kwa jina la Wanaume.
Wanaume wao walibadili sera. Wakati awali TMK ilikuwa kwa ajili ya wasanii wa Temeke tu, Wanaume wao wakafungua milango kwa yeyote hata awe anatoka Bagamoyo, ili mradi awe mtu wa kazi.
Wanaume wanaundwa na Richard Shauri Rich One, Karim Kazumari Kaka Man, Abdul Ally Mzimu, David Mpangile Daz P, Athuman Yahaya A Man na Juma Mbelwa Juma Jazz.
Wakati hayo yakitokea Inspector Haruni na wenzake wengine walikuwa wameshajiengua awali na kurudia kundi lao la asili, Gangwe Mob.
Hata hivyo kundi la Wanaume Family lililobaki chini ya Fela nalo liliingia doa, Jebi, YP na Y Dash nao wakajiengua na kuunda kundi lao lililoitwa TMK Unity.
Lakini miaka ya hivi karibuni makundi haya mawili maarufu yaani Wanaume Halisi na Wanaume Family yamepunguza kasi na pengine kufunikwa na baadhi ya wasanii wapya waliochipukia
Mwakilishi wa Wanaume Family, Amani Temba 'Mh Temba' anaeleza sababu zilizowafanya kupunguza kasi.
"Ni kweli tumekuwa kimya kwa kiasi fulani, lakini si kimya kirefu kwani hivi karibuni tumetoa kazi. Ni 'Kichwa Kinauma, naamini hii ni kazi iliyokubalika vema tu na mashabiki. Bado tupo," anasema huku akitabasamu.
Anasema mfano upo kwake, kwani ana takribani miaka miwili hajatoa wimbo binafsi, lakini tayari ameshamaliza kazi ya kuandaa wimbo anaotarajia kuuachia hivi punde.
Katika wimbo huo anaoutaja kwa jina la 'Maryoo' anatoboa siri kuwa amemshirikisha Bibi Cheka, kikongwe aliyegukia muziki wa kizazi kipya.
Temba, mkongwe wa Wanaume Family aliyekuwapo tangu awali, anasema kuanzishwa kwa Kituo cha Mkubwa na Wanawe, ndiyo sababu kubwa ya kufifia kwa kundi lao.
"Huu ni mpango maalum, si kwamba Wanaume Family imekufa ila ni mkakati wa kukitangaza kituo cha Mkubwa na Wanawe, kundi letu bado lipo pale pale," anasema.
"Unajua Temba hawezi kutoa wimbo na Aslay akatoa wimbo kwa wakati mmoja, hivyo tumeamua kuwapa sapoti hawa kwanza ili wakue na baadaye tutaendelea."
Katika kupeana nafasi huko, Mh. Temba ameshirikishwa katika wimbo wa Aslay 'Niwe Nawe' na ule wa Bibi Cheka Ni Wewe.
Anasema mfumo wanaoutumia ni kuwafanya vijana wao wajitegemee kwanza ndipo Wanaume Family iweze kurudi upya.
"Kundi bado lina mengi ya kufanya tupo wengi tu na wote tuna nia moja, hivyo tunajitolea kwa hali na mali kuhakikisha tunazalisha vipaji vingi kupitia kundi letu," anasema Temba aliyewahi kutamba na kibao cha Mkono Mmoja alichomshirikisha Chegge.
No comments:
Post a Comment