Wakati Bw Aziz Bouallouchen akiingia katika jumba la sinema katika mji wa Marrakesh nchini Morocco, tofauti na ilivyo katika majumba mengi ya sinema siku hizi ambapo wateja wanapewa miwani maalum za picha ya 3D, yeye anapewa vipokea sauti vinavyobanwa kichwani (headphones).
Bw Bouallouchen, ambaye umri wake ni kama miaka 20 hivi, si mwendaji sinema wa kawaida, na hili sio jumba la sinema la kawaida. Kila kiti ndani ya jumba la sinema kina vifaa maalum vya kusaidia wapenda filamu wasioona.
Filamu inayoonesha hapa inaitwa Lalla Hoby, filamu maarufu ya vichekesho nchini Morocco kuhusu mtu ambaye anavuka bahari ya Gibraltar ili kumsaka mke wake aliyemkimbia na kwenda kuishi na mwanaume mwingine nchini Ubelgiji.
Mwelekeo wa filamu
Filamu hiyo ilitoka mwaka 1996, na ni filamu pekee kutoka Afrika kaskazini kuwekewa maelezo ya maneno ndani yake.Akiwa amevaa vipokea sauti ambavyo vimeunganishwa katika vinasa sauti katika vishikio vya kiti, Bw Bouallouchen anasikiliza sauti inayoelezea mfululizo wa matukio, ishara za watu na matukio ambayo usiposikia unapoteza mwelekeo wa filamu.
"Ni wazo zuri sana," anasema Bw Bouallouchen. "Sijaweza 'kutazama' filamu tangu nilipopatwa na maradhi yaliyosababisha kupoteza uwezo wa kuona."
Miaka saba baadaye, amejikuta akiwa amekaa sambamba na watu wanaoona, "wakitazama" filamu pamoja.
Na hiyo ni kutokana na maelezo ya maneno, kila mmoja anacheka wakati muafaka katika vichekesho vya Lalla Hoby, akionekana kuanguka katika boti ndogo katika bahari ya Gibraltar.
Morocco inaongoza njia barani Afrika katika matumizi ya teknolojia hii mpya. Sauti inazungumza "sambamba" na matendo katika filamu na hutoa taswira njema zaidi kwa watu ambao hawawezi kuona.
Viwango
"Sisi ni nchi pekee barani Afrika na katika mataifa ya Kiarabu ambao tunatoa huduma hii kwa wasioona," anasema Nadia el-Hansali wa Wakfu wa Tamasha la Filamu la Marrakesh.Wakfu huo, ambao unaandaa matamasha mengi makubwa ya filamu, ambapo filamu zenye maelezo ya sauti kwa wasioona zimekuwa zikioneshwa kwa miaka miwili, unatenga fedha kwa ajili ya filamu zote ziwe na viwango vya kuonekana na watu wasioona.
Filamu nane mpaka sasa zina maelezo ya sauti, ikiwemo L'Atlante ya mwaka 1934, The African Queen (1951) na East of Eden (1955).
Katika kipindi cha miezi 18 ijayo, filamu nyingine sita zitawekewa huduma hiyo ya maelezo ya sauti.
"Tumetazama kuona kiasi gani cha kusema na kipi ni muhimu kwa ajili ya filamu nzima kueleweka"
Nadia el-Hansali
Iko kamilifu kabisa, na sauti huingia katikati ya mapengo kati ya mazungumzo ya wacheza sinema.
"Tumetazama kuona kiasi gani cha kusema na kipi ni muhimu kwa ajili ya filamu nzima kueleweka," amesema Bi el-Hansali.
"Naepuka kutoa taarifa nyingi kupita kiasi ambazo zitawachanganya wale wasio na uwezo wa kuona skrini."
Lengo ni kuondokana na mtindo wa zamani wa kutumia watu kutoa maelezo ndani ya sinema, huku wakiwa wamesimama, wakijaribu kuelezea kinachoendelea, lakini mara nyingi hutoa maelezo hayo wakati mazungumzo muhimu katika filamu yakiendelea.
Sinema
Mohamed Doukkali, mhadhiri asiyeona wa falsafa katika chuo kikuu cha Rabat nchini Morocco, ni mshabiki mkubwa wa teknolojia na yeye hutumia kompyuta maalum katika kazi zake za kila siku."Moja ya mambo muhimu ya teknolojia mpya ni kuwa huondoa vikwazo vinavyokukabili," Anasema Bw Doukkali.
Anajielezea kama mtu "mpenda filamu", lakini mara nyingi hutazama DVD akiwa nyumbani pamoja na mtu anayemuelezea kinachoendelea.
Amefurahishwa sana sasa kuwa hatimaye anaweza kwenda sinema.
"Pongezi kwa sauti ambayo inatoa maelezo ya kinachoendelea na tunaweza kufiatilia filamu katika njia ambayo hatukuweza kufuatilia zamani," amesema.
"Unafurahia zaidi kutazama filamu ukiwa umejumuika na watu wengine wengi, kitu ambacho ndio hasa lengo la sinema."
BBC.
No comments:
Post a Comment