Upo msemo mmoja ulivuma siku chache zilizopita, unasema, "ukiona manyoya, basi ujue keshaliwa" Kwa hivyo, ujumbe huu unaweza ukawa umetufungua macho wengine tuliokuwa tukikuna vichwa kujiluliza kulikoni? Vipi "kutiririka" kwenda India kwa matibabu kwa viongozi wetu kunashamiri na kushika kasi hivi? Mimi kwa mfano nilijiuliza: Je! Hii inatokana na wagonjwa hao kukosa imani na tiba toka kwa wataalamu wetu? Kwamba, wanahisi wanapewa tiba isiyo na kiwango? Au ni imani ya kasumba ya kujitakia au kufuata mkumbo tu kwamba matibabu ya "mzungu" au "mhindi" ama "mchina" yanaponesha vyema na haraka zaidi kuliko yale ya "mbantu" mwenzetu? Hatuamini wala kuuthamini utaalamu wa wataalamu wetu? Ikiwa madai yao kwamba wanakwepa huduma hafifu na mbovu, je, hawa viongozi wanaokuwa wepesi kutaka matibabu nje ya nchi, wanakosaje akili ya kuwawezesha wataalamu wetu kwa vifaa na mazingira bora ya kazi kwa kutumia fedha hizo hizo wanazozipeleka "India" ili nasi Watanzania tujivunie Watalaalamu wetu, wananchi wa kipato cha chini nao wasioweza kwenda "India" nao wapate nafuu ya tiba nzuri? Mbona tunadharauliana hivi? Umewahi kujiuliza ni kwa nini Watanzania wengi wanaohama nchi na kuajiriwa nchi nyingine wanasifika kwa uchapa kazi wao lakini wakiwa Tanzania walidharauliwa hata pale waliposhauri yaliyo ya haki? Ama ndiyo "Nabii hakubaliki kwao?" Fedha wanazolipwa viongozi wetu hawa si zinatokana na kodi za wananchi na rasilimali za mumu humu ndani jamani? Sasa badala ya kuzizungusha humu ndani, ni kwa nini zinapelekwa kunufaisha mataifa ya nje? Ama yote hayo hayana maana kwa kuwa fedha zenyewe, haziendi "nje" kweli bali zinazunguka na kurudi mifukoni mwao? Hii nchi hii, ukisikia "pa" ujue ndiyo hivyo tena...! | chanzo www.wavuti.com | w |
Thursday, February 2, 2012
Je wajua: Kwenda kutibiwa India inawezekana ni "biashara" ya watu fulani?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment