Pages

Friday, January 13, 2012

CCM Keko Machungwa waomba mgogoro wao kutatuliwa

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), tawi la Keko Machungwa B wilayani Temeke, kimeuomba uongozi wa chama hicho mkoa kuingilia kati mgogoro uliopo baina ya uongozi wa tawi hilo na wilaya unaoweza kuwapoteza zaidi ya wanachama 444 waliopo katika tawi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa tawi hilo, Andrew Kisalu alisema kwa muda mrefu uongozi wa pande hizo mbili umekuwa na mgogoro wa chini chini aliodai ni hatari na unaweza kuwasarambatisha wanachama wakati wowote.


Alisema mgogoro huo kimsingi hauna maslahi kwa chama hicho na sasa umefikia hatua ya kukwamisha ununuzi wa jengo linalotumiwa kama ofisi ambalo mmiliki wake alishatangaza kuliuza tangu mwishoni mwa mwaka jana huku akitoa kipaumbele kwa chama hicho.


Kisalu alisema baada ya uongozi wa chama hicho tawi kuwasiliana na mwenye jengo hilo, walikubaliana kumpatia fedha anazohitaji kiasi cha Sh milioni 15 ambazo waliziomba kutoka makao makuu ya chama kupitia ngazi ya Kata na Wilaya.


“Matokeo yake hadi hivi sasa bado hakuna dalili zozote za kupata fedha hizo na kila tulipojaribu kufuatilia tulibaini kuwapo kwa ukwamishaji katika ngazi ya chama wilaya, suala linaloweza kusababisha tulikose jengo hili tunalolihitaji kwa nguvu zote,” alisema Kisalu.


Alisema kwa taarifa zilizopo jengo hilo pia linatakiwa na chama kimoja cha siasa kwa gharama ya Sh milioni 18 ili walitumie kama ofisi, jambo alilodai kuwa bado halijakubaliwa na mmiliki wake kwa vile pia ni mkereketwa wa CCM hivyo kipaumbele chake anatoa kwa chama chake.


Aidha alisema tangu waanze kulitumia jengo hilo kama ofisi mwaka 2008, mbali na kupata mafanikio ya kuongeza idadi ya wanachama.


Aliwaomba viongozi wa juu wa chama hicho kulitafutia ufumbuzi suala hilo haraka ili kukinusuru chama hicho na wanachama wake kwani tayari kimeweza kujijenga vizuri huku kukiwa na maombi mengi kutoka kwa wanachama wengine wanaotaka kujiunga.

No comments:

Post a Comment