Pages

Tuesday, October 11, 2011

MAITI YA MWANACHAMA CHADEMA YAKUTWA PORINI

MAITI ya mkazi wa Dar es Salaam, Mbwana Masudi Mbwana anayedaiwa kuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imepatikana katika pori la Magereza katika Barabara ya Mwanzugi wilayani Igunga, mkoani Tabora ikiwa imeharibika.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Anthony Lutta, kwa sasa Polisi wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa daktari itakayobainisha sababu ya kifo cha mtu huyo.


Chadema wametoa taarifa kwa vyombo vya habari wakitaka Polisi ifanye uchunguzi wa kifo cha mwanachama wao huyo ambaye wanadai alipotea, kwa kuwa taarifa za awali za uchunguzi zinaonesha kuwa mwili wa marehemu una majeraha, macho yametobolewa na kichwa kimepasuliwa kutokana na kipigo.


“Ni kweli Polisi tulipokea Oktoba 2, mwaka huu siku ya uchaguzi Igunga, taarifa kutoka kwa Chadema juu ya kupotea kwa mwanachama wao ila mpaka sasa uchunguzi kuhusu suala hilo unaendelea,” amesema Kamanda Lutta.


Amesema, askari walioenda kuichukua maiti hiyo katika eneo ilikopatikana, waliikuta ikiwa katika hali mbaya hivyo suala la macho kutoboka au kichwa kupasuliwa hawakuliona. “Na ndio maana kwa sasa tunasubiri kwanza ripoti ya daktari,” alifafanua Kamanda huyo.


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika taarifa yake leo kwa vyombo vya habari, alisema chama hicho kinalaani ilichokiita mauaji na uharamia aliofanyiwa mwanachama wao huyo aliyewasili Igunga Septemba 30, mwaka huu kushiriki katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge akiwa wakala wa chama hicho.


“Hata hivyo, tangu awasili hakuonekana tena hadi Oktoba 9, mwaka huu maiti yake ilipopatikana katika pori hilo la Magereza,” alisema Mbowe na kuvitaka vyombo vya dola kuchunguza haraka na kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo na kuwataka wananchi wenye taarifa yoyote kuiwasilisha kwenye vyombo vya usalama ili sheria ichukue mkondo wake.


Amesema, kwa kuwa mwili wa marehemu umeharibika vibaya, chama hicho kimeshauriana na ndugu wa marehemu na kukubaliana azikwe leo Igunga kwa heshima zote za chama na baadaye maombi na sala kwa marehemu vitafanyika Dar es Salaam.

Habari leo. 

No comments:

Post a Comment