MSOMAJI hili ni tukio la kusikitisha, kuhuzunisha na pengine laweza kukutoa machozi kama ilivyonitokea, lakini nakuomba uwe mvumilivu ili kuviachia vyombo vya usalama na sheria vifanye kazi yake.
Matukio ya kikatili, kudhalilisha utu wa mwanadamu na ambayo yanahitaji kukomeshwa kwa gharama yoyote ile ya kukata sehemu za miili ya walemavu wa ngozi, yaani Albino, yalikoma kwa muda, pengine ni kutokana na harakati zilizoanzishwa na Rais Jakaya Kikwete za kuwasaka na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria.
Lakini yaonekana juhudi hizo, hazijazaa matunda. Tatizo hilo ambalo limesababisha wanadamu na Watanzania wenzetu kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa viungo wa kudumu, limerejea tena Kanda ya Ziwa.
Mmoja wa waliofikwa hayo ni kijana Adam Robert (14), ambaye alijitahidi kutetea maisha yake dhidi ya wauaji wenye tamaa ya ya pesa kwa nguvu ya ushirikina.
Robert ni mlemavu wa ngozi (albino), mkazi wa kijiji cha Nyaruguguna Kata ya Nyijundu wilayani Geita katika mkoa mpya wa Geita.
Kwa sasa, kijana huyo amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, akipatiwa matibabu, baada ya kukatwa mkono wa kushoto na kisha kunyofolewa vidole vitatu vya mkono wa kulia.
Tukio hili limetokea usiku wa kuamkia Jumamosi ya Oktoba 15 mwaka huu, nyumbani kwao na mlemavu huyo. Siku hiyo alivamiwa na mtu mmoja ambaye bado hajatambulika wala kutiwa mbaroni na polisi, ingawa upelelezi mkali unaendelea wilayani Geita juu ya tukio hilo.
Siku hiyo ya tukio majira ya saa 7 na dakika kadhaa usiku, napigiwa simu na moja ya vyanzo vyangu vya habari wilayani Geita na kujulishwan juu ya kuwepo kwa tukio hilo.
Chanzo hicho kilinisisitizia kwamba hali ya majeruhi ni mbaya sana, ambapo gari la polisi limeamua kuachana na msako wa mtu anayetuhumiwa kujihusisha na kitendo hicho ili kumkimbiza hospitalini kujaribu kuokoa maisha ya mlemavu huyo.
‘’Wewe rafiki yangu unalala sasa hivi wakati huku kuna tukio kubwa limetokea? Nyanyuka uende hospitalini kuna mlemavu wa ngozi au albino amejeruhiwa vibaya kwa kukatwa mkono na kunyofolewa vidole vitatu, hali yake ni mbaya, tuko njiani tunamleta hospitali hapo Geita…..’’ kilisema chanzo hicho cha habari kupitia simu ya mkononi kikinipa taarifa za tukio hilo.
Nikanyanyuka kutoka kitandani. Nilipoangalia saa yangu nilibaini kuwa ni saa 7 :30 usiku, nikajiuliza umbali alipo mtu huyo ni kilomita zaidi ya 90, hivyo mpaka atakapofika hospitalini itakuwa saa 10 alfajiri, nikasema hapana ni bora nilale ili asubuhi niwahi hospitalini.
Kesho yake niliamka mapema na kwenda hospitalini majira ya saa 1:30, nilipofika katika hospitali hiyo, nikaenda moja kwa moja wodi ya wanaume namba 8, kwa sababu usiku wake nilikuwa nimeelezwa kwamba majeruhi ni mwanamume, hivyo nilijua kwamba kwa vyovyote atakuwa katika wodi hiyo.
Nilipoingia tu, macho yangu yaligota kwa mlemavu huyo, ambaye amelazwa kitanda namba 5 katika wodi hiyo. Nilimtambua mapema ikizingatiwa kwamba siku hiyo hakukuwa na wagonjwa wengi waliolazwa katika wodi hiyo.
Nilipofika kwa mtoto huyo, nilimkuta mtu mmoja ambaye baada ya kujitambulisha kwake, aliniambiwa kwamba yeye ni baba wa mlemavu huyo. Wakati huo mtoto huyo alikuwa akihema juu juu huku akiwa na dripu ya kumuongezea damu mkononi mwake. Hakika hali ile ilinisikitisha sana na kujikuta nikitokwa na machozi .
Siyo mara yangu ya kwanza kushuhudia tukio kama hilo la kujeruhiwa kwa albino. Nimewahi kushudia matukio makubwa, ikiwemo kushuhudia mwili wa albino aliyeuawa vibaya baada ya kukatwa miguu yote miwili. Huyo wauaji walimkata miguu yote miwili kwenye mapaja na kubakiza usawa wa makalio tu!.
Baada ya hapo, nikaanza kumhoji baba wa mlemavu huyu ambaye alijitambulisha kwangu kwa jina la Robert Tangawizi (36). Alinisimulia kwa kina juu ya tukio hilo. Hata hivyo, muda wote alionekana kama mtu mwenye wasiwasi na alikuwa akitetemeka. Wakati mwingine alikuwa akitetemeka mno hadi kushindwa kuongea.
Akisimulia zaidi mkasa huo, baba huyo anasema siku ya tukio alifika nyumbani majira ya saa moja kasoro na alimkuta mwanae nyumbani akitengeneza kuni kwa ajili ya moto wa kuota, maarufu kwa jina la Kikome. Wakasalimiana kisha yeye akaenda ndani na kuhifadhi jembe lake, ambalo alikuwa ametoka nalo shambani.
Baadaye alitoka nje na kukuta mwanae akiwa amekwishawasha moto, akaenda kuketi naye huku wakiota moto. Muda mfupi baadaye alimuona mtu amesimama umbali wa mita 20 hivi shambani. Alimuita na kutaka kujua shida yake.
Mtu huyo alipofika, alimwambia kwamba anatafuta ng’ombe wake, aliodai kuwa walikuwa wamepotea tangu asubuhi. Alimkaribisha na kumpatia kiti. Alipoketi walianza kuota moto huku wakiendelea na mazungumzo yao juu ya upotevu wa ng’ombe wake.
Ghafla mtoto wake huyo (majeruhi) akamwambia kwamba mtu siyo mzuri, kwani tangu mchana alikuwa anamfuatafuata alipokuwa malishoni akiwa na ng’ombe, ambako alikuwa akimdanganya kuwa angempatia kofia.
Baada ya kusikia mwanae akimueleza hivyo juu ya mtu ambaye wameketi naye, aliamua kumvuta pembeni na kumtaka amueleze vizuri, ambapo huko alisisitiza kuwa mtu huyo alikuwa akimdanganyia kofia kwamba akaichukue, lakini yeye alikataa. Baadaye, alimtaka warejee kwenye kikome na wakafanya hivyo.
“Tukarejea na tukaketi, lakini kabla sijaanza kumuuliza zaidi mtu huyo, chakula kikaletwa mbele yetu, tukanawa na kuanza kula. Ghafla mvua ikaanza kunyesha hivyo ikabidi nichukue ugali na mwanangu huyu akachukua mboga ili twende kula ndani. Nikatangulia kuelekea ndani, lakini nilipoingia tu ndani, nikasikia kishindo na kelele za huyu mwanangu akilia, nikatoka nje nikasimama mlangoni. Nilipoangalia niliona mtu huyo aking’ang’ana kuukata mkono wa kulia wa mwanangu. Nilishikwa na butwaa na kushindwa la kufanya pamoja na kwamba kitendo hicho kilichukua zaidi ya dakika 10. Baada ya mtuhumiwa huyo kumaliza kutenda unyama huo, aliondoka na kutokomea gizani na ndipo nilipoamua kuanza kuwaita majirani ili waje kusaidia”, anasema.
Habari leo
No comments:
Post a Comment