MWAJABU Juma kutoka Temeke ndiye mrembo wa kwanza kuingia nusu fainali za shindano la Vodacom Miss Tanzania 2011 linalotarajiwa kufanyika Septemba 10.
Mwajabu ambaye alishika nafasi ya tatu kwenye shindano la Miss Temeke na kupata tiketi ya kushiriki Vodacom Miss Tanzania, ameingia nusu fainali baada ya kuibuka kinara katika shindano la mrembo mwanamitindo ‘Miss Top Model’.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency ambayo ndio waratibu wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga alisema Mwajabu alichaguliwa na majaji watatu walioongozwa na Asia Idorus.
Warembo wengine walioingia tano bora katika kinyang’anyiro hicho ni Jenifa Kakolaki, Silvia Kimasha, Alexia William na Zeronia Manoko.
“Mashindano ya Miss Tanzania safari hii yamebadilika, kwanza nusu fainali kutakuwa na warembo 15 badala ya 10 kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,” alisema.
Lundega alisema warembo watano kati ya hao 15 watapatikana katika mashindano madogo madogo yatakayofanyika wakati warembo wakiwa kambini.
“Miss Top Model tumeshampata, bado Sports Woman, Miss Talent, Miss Personality na Miss Photogenic, kila wiki tutakuwa na shindano la kumtafuta mshindi wa kipengele kimoja,” alisema.
habarileo
No comments:
Post a Comment