NAZI ni moja ya zao linalotumika sana na wakazi waishio maeneo ya pwani katika mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.
Hapa nchini zao hili limekuwa la asili, enzi na enzi na limesaidia katika matumizi mbalimbali hasa katika kuongeza ladha ya chakula, ikiwekwa kama kiungo, mafuta ya kujipaka kama aina ya kipodozi katika kulainisha ngozi kwa watoto na watu wazima,
nywele na dawa ya magonjwa mbalimbali ya binadamu.
Viinilishe vilivyomo katika nazi daima hubaki hai ndiyo maana ni tiba kwa magonjwa mengi na pia ina kiinilishe kiitwacho Lauric ambacho mtu akikinywa mwilini kinakuwa mono lauric.
Mtafiti wa Mafuta Mwali ya Nazi (virgin oil) wa Kituo cha Utafiti cha Mikocheni Dar es Salaam, Dk. Ruth Minja, anasema kiini lishe hicho kinapatikana katika maziwa ya mama kwa asilimia 50 hadi 55 ya kiini lishe hicho.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili kwenye Maonesho ya Nanenane ya Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Morogoro mwaka huu, Dk. Minja anasema matumizi ya mafuta hayo ni mengi kuliko yaliyobainika mpaka sasa.
“Tukishakuna nazi ili kupata mafuta mwali, tunaianika kwa saa nne na kisha kuichuja kwa kitambaa safi cheupe, vipo vifaa maalumu vya kazi hiyo lakini ni rahisi kusema kitambaa cheupe kisafi, matumizi na kazi za mafuta ni nyingi zaidi ya zinazofahamika hivi sasa hivyo tunaendelea kuzitafiti,” anasema Dk. Minja.
Kuhusu mafuta mwali kama dawa, Dk. Minja anabainisha kuwa, mafuta hayo yakitumiwa kwa kunywa na watu wenye virusi vya Ukimwi, husaidia kupandisha kinga ya mwili (CD4), kwa kuwa mafuta hayo yana nguvu kiasi ya kuzingira kirusi ili kisijibadilishe na kuzaana na hivyo kuongeza kinga.
Anasema pia mafuta hayo yakitumika kwa maelekezo ya daktari, yanaleta tija zaidi ya mtu akitumia bila utaalamu na kwamba pia ni dawa ya mafua, kwa kiasi inasaidia wagonjwa wa kisukari kwa kuwa inachochea uzalishaji wa Insulin mwilini.
Dk. Minja anasema utafiti kuhusu mafuta mwali ya nazi na zao kwa ujumla ulianza mwaka 1979, ambapo watafiti walitumia mashine kukamua mafuta na teknolojia ya kuanika nazi ilitumika kuwafundisha wakulima kutokana na uhaba wa vifaa jambo linalokikabili kituo cha Mikocheni hadi sasa.
“Kuna mambo mengi ya kuzungumza na wakulima na kushirikiana kuyafanya ili kuongeza tija ya zao la nazi lakini mafungu ya fedha yanayokuja ni madogo kiasi kwamba tunashindwa kufika katika maeneo mengi kwa wakati mmoja,” anasema Dk. Minja.
Hata hivyo, kituo hicho kilichoanza kuhamasisha matumizi ya mafuta mwali mwaka 2006 kwa kutoa semina na mafunzo mbalimbali, kinafanyakazi na vikundi vya wajasiriamali ambavyo huwawezesha kiteknolojia kikiwemo kikundi cha Bagamoyo- Chambezi wanakozalisha minazi kwa ajili ya kutengeneza mafuta hayo huku kituo hicho kikisimamia ubora.
Kwa mujibu wa Dk. Minja, soko la uhakika la mafuta mwali lipo kuanzia la ndani hadi nje ya nchi na kutokana na ubora wa mafuta hayo, chupa ya ujazo wa miligramu 250 iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh 3,000 miaka michache iliyopita sasa ni Sh 7,500 hivyo ni zao la kibiashara kwa wakazi wa pwani.
Changamoto: Pamoja na faida hizo za nazi hasa mafuta mwali, magonjwa ya nazi hasa ugonjwa sugu wa Kunyong’onyea kwa kitaalamu Lethal Yellowing, ni tatizo kubwa na umeenea kwa madaraja tofauti katika pwani yote ya Tanzania Bara kama ifuatavyo: Kwa mujibu wa Mtafiti wa Kituo cha Mikocheni, Gideon Nyalusi, ushambuliaji wa kiwango cha juu upo katika maeneo ya pwani ya Mkuranga na Rufiji, kiwango cha wastani ni pwani ya Lindi na Mtwara na kiwango cha chini maeneo ya pwani ya Dar es Salaam na Tanga.
Nyalusi anasema utafiti rasmi kuhusu magonjwa ya nazi ulianza mwaka 1978, mwaka mmoja kabla kuanza uzalishaji wa mafuta mwali ya nazi, utafiti huo ulifanyika chini ya mradi wa uzalishaji wa zao la nazi wa NCDP.
Anasema mwaka 1980 upandaji wa eneo la mashamba ya minazi Bagamoyo-Chambezi, Kifumangao na Sotere-Mkuranga pamoja na Magawa, Rufiji-Mbwera, Lindi-Ng’apa na Tanga-Pongwe na Maramba.
Mtafiti Nyalusi anasema mwaka 1996, minazi mirefu, mifupi na chotara kutoka nje ya nchi, ililetwa nchini kwa ajili ya majaribio kama itahimili vishindo vya magonjwa na kuonesha haiwezi, na kuamuliwa kuletwa aina 28 za minazi mirefu kutoka Afrika Mashariki maarufu kama EATall.
“Hii ilipandwa mikoa ya Mtwara na Tanga kwa majaribio ambapo kati ya hizo, aina tano zilionesha kuhimili magonjwa kwa asilimia 65 hadi 70, baada ya kuzipata hizo aina tano, tulizipanda kwa kuzipa majina kutokana na eneo,” anafafanua Nyalusi.
Kwa mujibu wa Nyalusi, Tanga ilipandwa eneo la Vuo na kupewa jina EATallxVuo, nyingine EATallxLBS na EATallx Mwambani na eneo la Kilwa Mtoni iliitwa EATallxMtoni huku eneo la Songosongo ikaitwa EATallxSongosongo.
Mtafiti huyo anasema hatua hiyo ya utafiti ilizaa matunda kwa sehemu na kwa kuwa mimea hiyo ya nazi haikuwa na uwezo wa kukabiliana na magonjwa kwa asilimia 100, wakulima walifunzwa namna ya kuizoea minazi kuishi na ugonjwa bila kudhurika kwa kiasi kikubwa kwa kupanda mazao mbadala.
Pili walibainishiwa mazao hayo mbadala ambayo ni maembe, michungwa na kuongezewa teknolojia ya sasa kwa kuchanganya na mazao ya muda mfupi ya chakula kama vile mahindi, kunde, mbaazi, viazi, muhogo na mengineyo ili mkulima asikose kuvuna kabisa pindi nazi zikigoma kumpa kipato.
Elimu imewafikia wakulima? Kuhusu elimu zaidi kwa wakulima, Nyalusi anasema wanaendelea kutoa elimu huko Bagamoyo ambako wakulima tayari wanaona faida ya nazi na pia mkazo zaidi umewekwa kwa wakulima wa Rufiji na maeneo yote ya Kusini, Mkuranga na Tanga kwa mfumo wa mashamba darasa.
Anasema mashamba darasa hayo ni ya wakulima 15 ambao hupewa miche 24 ya minazi kwa ajili ya shamba darasa na pia huwapa bila malipo mbegu bora za mazao mbadala ya chakula kama mahindi, kunde kulingana na mafunzo ya shamba darasa.
Nyalusi anabainisha kuwa kwa Wilaya hizo tatu (Rufiji, Mkuranga na Tanga) wamewafikia wakulima 45 mwaka huu kwa mfumo wa shamba darasa ambao wanapaswa kuwafikia wakulima wenzao mara tatu yao na tayari wamepeleka miche na mbegu hizo ili mwezi ujao (wa tisa), wataalamu waanze mafunzo ya mashamba darasa kwa wilaya hizo.
Mfanyabiashara wa nazi katika Soko la Kariakoo, Dar es Salaam, Mustafa Khamis anakiri kuwa nazi ina faida nyingi kuacha mafuta mwali, lakini anasikitishwa kwa kile alichodai haoni mchango wa Serikali kuwasaidia wakulima wa nazi nchini kwa kuwa wamekuwa wakihangaika wenyewe hivyo kusababisha kuyumba kwa bei ya nazi sokoni mara kwa mara.
“Unaweza kuja leo ukakuta nazi Sh 500 nyingine Sh 800 hadi 1000 hii ni kwa sababu ya msimu wenye wa Mfungo wa Ramadhani, lakini ikiisha, utaona nazi hadi Sh 200, hakuna bei ya wastani ya soko, hivyo huwezi kusema hili ni zao la biashara kwa kuwa bado halipo kibiashara japo linasifika na kufahamika duniani kote,” analalama Khamis.
Vipi kuhusu Zanzibar? Nyalusi anasema miongoni mwa mambo waliofanikiwa Zanzibar ni kudhibiti magonjwa kwa kuzuia uingizwaji wa miche ya nazi ovyo visiwani humo.
habari leo.
Anaongeza kuwa “hivyo tangu awali, Zanzibar hawana tatizo la magonjwa kutokana na udhibiti huo lakini huku Bara, usimamizi wa mipaka na ukaguzi wa kitaalamu ulisuasua awali na kusababisha hali hiyo.
No comments:
Post a Comment