Pages

Monday, April 11, 2011

Gbagbo akamatwa baada ya purukushani

Laurent Gbagbo akionyeshwa kwenye televisheni muda mfupi baada ya kukamatwa

Kiongozi wa Ivory Coast Laurent Gbagbo ametiwa kizuizini mjini Abidjan na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi wa Umoja wa Mataifa.

Alikamatwa wakati majeshi ya kiongozi anayetambulika kimataifa kuwa Rais wa nchi hiyo Alassane Ouattara na vifaru vya Ufaransa kuingia kwenye makazi yake.

Bw Gbagbo alikuwa akikataa kukabidhi madaraka, akisema alishinda uchaguzi wa Rais wa mwezi Novemba.
Ufaransa ilisema majeshi yanayomwuunga mkono Ouattara yalimkamata, lakini washirika wa Bw Gbagbo walisema ni majeshi maalum ya Ufaransa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alisema kukamatwa kwa Bw Gbagbo kumemaliza miezi kadhaa ya ghasia zisizo na sababu, na Umoja wa Mataifa utaunga mkono serikali mpya.
Majeshi ya kutunza amani ya umoja huo yaliyashutumu majeshi yanayomwuunga mkono Bw Gbagbo kwa kuhatarisha maisha ya raia na kuiomba Ufaransa, ambalo lilikuwa koloni lake, kuondosha silaha nzito za kiongozi huyo.

Kumekuwa na madai ya ukatili kufanywa na wote wafuasi wa Gbagbo na Ouattara, na umoja huo una taarifa ya zaidi ya watu 1,000 kuuawa na takriban 100,000 kukimbia nchi hiyo.
Wawakilishi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa wa Ivory Coast, Youssoufou Bamba, walisema Bw Gbagbo atashtakiwa.

Mjini London, Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague alisema kama atafunguliwa mashtaka, basi ashtakiwe kwa kuzingatia njia zinazostahili.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Hillary Clinton alisema mjini Washington kwamba kukamatwa kwa Bw Gbagbo kumepeleka ujumbe kwa "madikteta" ambao "hawatopuuza sauti za watu wao katika uchaguzi wa haki na huru."

No comments:

Post a Comment