MKURUGENZI wa Manispaa ya Temeke, Magreth Nyalile amelipongeza shirika lisilo la kiserikali la Kukabiliana na Umasikini na Kutunza Mazingira (APEC), kwa kupunguza matukio ya uporaji na mauaji ya waendesha pikipiki na baiskeli ya magurudumu matatu maarufu bodaboda katika Wilaya ya Temeke.
Akifunga mafunzo ya usalama kwa waendesha pikipiki Kata ya Yombo Vituka, Buza na Makangarawe iliyosoma kwa niaba yake na Ofisa Afya Usafishaji Manispaa ya Temeke, Ernest Mamuya, Mkurugezi huyo alisema kazi inayofanywa na APEC ni ya kupongezwa.
“Tunawashukuru APEC kwa kupunguza mauaji ya waendesha pikipiki kutoka watu watano mwaka 2009 hadi watatu mwaka 2011,” alisema.
Pia alipongeza kazi nzuri ya kufundisha Polisi Jamii na uanzishwaji wa vikundi vya Ulinzi Shirikishi ilivyosaidia kupatikana kwa bunduki 18 Wilaya ya Temeke na risasi 1,309 kwa Kanda maalumu ya Dar es Salaam zote zikitumika katika uhalifu.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa APEC, Respicius Timanywa alisema tangu kuanza mafunzo ya ulinzi shirikishi mwaka 2010 mauaji na matukio ya uhalifu wa uporaji wa pikipiki yamepungua kwa kiasi kikubwa Timanywa aliomba Polisi kusaidia kufunga vituo vya pikipiki ambavyo vinaongoza kwa vitendo viovu kama uchomaji wa magari ya watu na kubeba mshikaki.
Alisema mwaka 2009 pekee takwimu zinaonesha watu 120 walifariki dunia na wengine 1,073 kupata ajali mbaya na baadhi kukatwa viungo vyao wengi wao wakiwa waendesha pikipiki. Na mpaka sasa kwa kushirikiana na polisi wameshafundisha vijana 1,000.
No comments:
Post a Comment