Pages

Thursday, December 15, 2011

Kampuni tano zaomba kujenga daraja Kigamboni

KAMPUNI tano zimejitokeza kuomba zabuni ya ujenzi wa daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambazo moja kati ya hizo ndiyo itakayopewa dhamana ya ujenzi huo mara mchakato huo utakapokuwa umekamilika.

Akizungumza wakati wa kufungua zabuni hiyo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ludovick Mrosso, alisema awali kampuni saba zilijitokeza kuomba, lakini mbili kati ya hizo, zilishindwa kuwasilisha mchanganuo wake.


“Tunashukuru kuwa mwitikio umekuwa mzuri, hivyo kinachohitajika kwa sasa ni kumpata mshindi mmoja kutoka katika kampuni hizi tano ili tuweze kumkabidhi jukumu la ujenzi wa daraja hilo linalotarajiwa kuwa chachu ya uchumi katika sekta ya usafirishaji,” alisema Mrosso.


Alizitaja kuwa ni Long Jian Road and Bridge, Sichuan Road and Bridge Group, China Communication Construction, China Railway Contract Eng Group ikishirikiana na China Major Bridge Eng, zote za China.


Mrosso alisema hatua iliyofikiwa ni ya kwanza kuelekea nyingine na kwamba kinachosubiriwa kwa sasa ni mchujo kwa makandarasi hao ili kumpata mmoja atakayekabidhiwa jukumu la ujenzi huo.


Alisema wanatarajia kuwa mkandarasi atakayepatikana, atajenga daraja hilo kwa ufanisi na hivyo kumaliza kiu ya muda mrefu ya kuwepo kwa daraja hilo linalotarajiwa kuwa kiunganishi kizuri kwa wakazi wa Kigamboni.


Aidha, alisema ujenzi wa Daraja la Kigamboni ni mradi mkubwa kwa NSSF kusimamia katika kutoa huduma bora kwa jamii.

No comments:

Post a Comment