Saturday, May 17, 2014
Truvada yatumika kuzuia Ukimwi badala ya kondomu
Dar es Salaam. Wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili na wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja sasa wanatumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi aina ya Truvada kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo badala ya kutumia mipira ya kondomu.
Mwananchi lilizungumza na baadhi ya wafanyabiashara ya ngono jijini katika maeneo ya Mwananyamala Hospitali, Komakoma na Vingunguti ambao walisema kuwa wanatumia dawa hizo kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya VVU ili kuwaridhisha wateja wasiopendelea mipira hiyo.
Baadhi ya wafanyabiashara hao walidai kuwa wanatumia Truvada kuzuia maambukizi pindi wanapokutana na wanaume wakware ambao huwabaka au kuwalazimisha kufanya mapenzi bila kinga.
“Hizi dawa tunazipata katika hospitali na wakati mwingine katika maduka makubwa ya dawa. Kwa sababu zinazuia maambukizi ya Ukimwi na sisi ni watu ambao tunafanya kazi katika mazingira hatarishi,” anasema Leyla Musa, mmoja wa wanawake hao.
Si hivyo tu, kwa kuwa hii ni biashara baadhi yao hukubali kufanya mapenzi bila mipira ili kupata fedha nyingi kutoka kwa wanaume.
Wengine hukimbilia huduma ya PEP
Baadhi ya wanawake hao wanasema kuwa baada ya kufanya mapenzi na wanaume kadhaa asubuhi huenda katika kliniki zinazotoa huduma za ARV na kudanganya kuwa wamebakwa na kisha hupewa huduma za dharura za ARV zinazoitwa kwa kitaalamu Post-exposure prophylaxis.
Kwa kawaida mtu aliyebakwa au kujikata hupewa dawa aina ya Lamivudine, Zerophidine au Truvada kulingana na uzito wa tatizo.
“Tunatumia hizi dawa mara kwa mara lakini tunafanya hivyo katika kliniki tofauti ili tusigundulike,” alisema mmoja wao, mkazi wa Mwananyamala, Mariam Leshaniki.
Kwa maelezo ya Dk Rachel Baggaley, mtaalamu wa masuala ya Ukimwi wa Shirika la Afya Duniani anasema dawa za PEP zipo maeneo mengi duniani kwa sasa na zinafanya kazi kwa ufanisi pia hazina madhara kwa mwanamke.
“Dawa hizi siyo sumu mwilini, zinaingia kwenye mfumo wako wa damu kabla virusi havijajizatiti na inavizuia ili mradi uzitumie ndani ya saa 72,” anasema Dk Baggaley.
Dawa ya Truvada, ambayo ina mchanganyiko wa dawa aina ya Tenovofir na Emtricitabine, imethibitishwa kuwa salama kwa kupunguza makali ya VVU pia kuzuia maambukizi mapya. Dawa hizi zinazotengenezwa nchini India, zimekuwa msaada mkubwa wa tiba kwenye nchi zinazoendelea.
Mkurugenzi wa Sera, Mpango na Utafiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk Raphael Kalinga alisema Tume hiyo inakemea kwa nguvu zote tabia inayofanywa na watu hao, kwani hakuna tofauti na kuvaa chuma kisha kujitumbukiza kwenye moto uwakao.
“Wanachofanya siyo sahihi. Ina maana kama una kinga ya malaria basi unatakiwa ukae karibu na mbu wakuume. Si unawakimbia… huo siyo uamuzi sahihi kabisa na ninawataka waondokane na tabia hiyo,” alisema.
Hata hivyo, Dk Kalinga alikiri kuwa ni kweli dawa hizo zinazuia maambukizi, lakini bado inategemea wingi wa virusi alivyonavyo mgonjwa pia mtu anaweza kuambukizwa magonjwa mengine ya zinaa kama kisonono, kaswende na pangusa.
“Kwa kweli tunakemea kwa nguvu zote na tunawashauri kwa usalama wao waondokane na mawazo hayo na wala wasijaribu hata mara moja kuacha kutumia kondom kuzuia maambukizi,” alisema.
Kama njia hii ya kuzuia maambukizi ya VVU itaendelea kufuatwa basi itabadilisha mfumo mzima wa kupambana na virusi hivyo ambao unahimiza matumizi ya kondomu kama kinga. Tangu mwaka 2010, tafiti tatu tofauti kuhusu dawa ya Truvada zimefanyika na kuonyesha uwezo mkubwa wa kuzuia maambukizi ya VVU iwapo zitanywewa kila siku. Wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsi moja waliotumia dawa hizo kila siku, walipopimwa damu walionekana kuwa salama kwa asilimia 99.
Wakati Dk Kalinga akipinga matumizi ya Truvada kama kinga ya VVU, Daktari wa magonjwa ya kuambukiza wa New York, Anthony Fauci, alisema ni vyema dunia nzima ikakubaliana na mpango wa kuanza kutumia dawa hizo ili kuokoa mamia ya watu walio katika hatari ya maambukizi.
“Kaswende, kisonono kinaweza kutibiwa na dawa za viua sumu (antibiotics), lakini Ukimwi ukiupata ni wa maisha yote hauwezi kutibiwa,” alisema Dk Fauci.
Kituo cha Kuzuia Magonjwa cha Marekani, kinaeleza kuwa hata kama itakubaliwa Truvada zitumike kama kinga, basi zitatolewa kwa wale ambao bado hawajaambukizwa. Pia, watatakiwa kupimwa kila baada ya miezi mitatu kuhakikisha kuwa hawajapata maambukizo na kupimwa ili kujua kama hawapati madhara yoyote yanayosababishwa na dawa hizo pia kama hawana magonjwa ya zinaa.
Watafiti waliogundua Truvada wanaeleza kuwa dawa hiyo kwa sehemu kubwa inakinga VVU na upande mwingine inasaidia kuua virusi vya Ukimwi kwa mtu ambaye tayari ameshaathirika. Hata hivyo, FDA na watafiti hao hawajaeleza kama Truvada inatibu moja kwa moja, isipokuwa wanasisitiza: “Inamkinga mtu kupata maambukizi mapya, inamsaidia mwathirika kwa kuua VVU pamoja na kumkinga dhidi ya magonjwa nyemelezi.”
Mtafiti wa Masuala ya Ukimwi, Dk Edward Maswanya anakana kuwa Truvada inazuia maambukizi na kusema siyo sahihi kutumia dawa hizo kama kinga.
“Kinga inayoaminika na kukubalika kuzuia maambukizi ni kondomu pekee hiyo Truvada haizuii kabisa,” alisema.
Alisema wanaofanya biashara ya ukahaba wanajiweka hatarini kupata maambukizi ya VVU pia wapo hatarini kuambukiza wengine.
Baadhi ya wanawake wanaofanya biashara ya ngono wa eneo la Temeke, Tandika na Mbagala Zakhem walipohojiwa walidai kuwa mipira ya kiume imekuwa siyo salama kwao tena, kwani kuna wakati wanaume huitoboa kwenye chuchu na mara nyingine huzama ukeni kiasi cha kusababisha wafanyiwe upasuaji.
“Kondomu zinasaidia, lakini kwa wanaume wastaarabu, lakini ninapomeza hizi dawa hata nikibakwa zinazuia maambukizi na zinasaidia kama ninao nisiwaambukize,” alisema mmoja wa wanawake hao.
Mashoga nao
Mwanamume anayeshiriki mapenzi ya jinsi moja, Aly maarufu kama Aunt Aly, mkazi wa Kinondoni anasema ingawa anaishi na VVU, lakini yeye huzitumia dawa hizo kuepuka kupata maambukizi mapya na kuzuia asiwaambukize wengine, kwani hubakwa mara kwa mara na vibaka.
“Mara kwa mara sisi tunaingiliwa kwa nguvu na wakati mwingine wabakaji hawavai mipira sasa, tunakunywa hizi kama sehemu ya kinga, ingawa mimi nazinywa kama ARV za kawaida,” alisema.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
BAADHI YALIYOJILI MWEZI WA NNE
Shobigo style Mtanzania pekee aliyeiwakilisha nchi yake katika mashindano ya dance ya red bull huko Afrika Kusini na kushika nafasi tatu za juu
Mafuriko yakaikukmbuka jiji la Dar es Salaam
Samaki wa ajabu aliyevuliwa katika mashamba ya mpunga huko Morogoro
Yanga kupoteza wachezaji wawili Didier Kavumbagu na Domayo ambao wote wamesajiliwa na Azam kwa msimu unaokuja.
Wawakilishi katika bunge la katiba Ukawa walivyolisusia Bunge
Mafuriko yakaikukmbuka jiji la Dar es Salaam
Samaki wa ajabu aliyevuliwa katika mashamba ya mpunga huko Morogoro
Yanga kupoteza wachezaji wawili Didier Kavumbagu na Domayo ambao wote wamesajiliwa na Azam kwa msimu unaokuja.
Wawakilishi katika bunge la katiba Ukawa walivyolisusia Bunge
NAINGIA MZIGONI TENA
Baada ya blog yetu ya temeke pamoja kukaa kimya kwa kipindi cha mwezi hivi tutaanza kuwa tena hewani tusubiri ubunifu mpya ambao utafanya kila mda uwe una hamu ya kufungua blog yetu
Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitikeza
Subscribe to:
Posts (Atom)