Licha ya Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, kutokuwa na jina kubwa katika ulingo wa siasa na wengi kumwona mgeni, ndiye aliyekuwa 'kichwa' (think tank) wa Ukawa, imefahamika.
Juzi, Chadema ilimteua Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu mpya kushika nafasi ya Dk. Willibrod Slaa, aliyejiuzulu nafasi hiyo Julai 30, mwaka jana, kwa kile akichokieleza kuwa ni utaratibu kutofuatwa wa kumkaribisha Edward Lowassa, aliyehamia katika chama hicho kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, uteuzi wake umepokelewa kwa mtazamo tofauti kutokana na kutokuwa na jina kubwa katika ulingo wa siasa, lakini imefahamika kuwa ni mmoja wa watu waliofanikisha mipango mikakati ya Ukawa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kupata mafanikio makubwa, baada ya kuwa na wabunge 113 bungeni ikiwa ni wale wakuchaguliwa na viti maalumu.
Idadi hiyo ni kubwa zaidi kupatikana tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kwanza unaojumuisha vyama vingi mwaka 1995.
Katika mafanikio hayo, Dk. Mashinji alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sera na Wanataaluma wa Ukawa na ndio walioandaa Ilani ya Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Akielezea uwezo wake na anavyomfahamu, Mwenyekiti wa Kamati ya Sera na Wanataaluma wa Ukawa, Dk. Rodrick Kabangira, ambaye amefanya kazi kwa karibu na Dk. Mashinji, alisema ni mtendaji mwenye malengo ya kimkakati na kufuatilia kwa karibu anayoyatenda.
"Nilifahamiana naye mwaka 2011 tulipokuwa tunaandika majarida mbalimbali ambayo tuliyawasilisha Chadema kama la namna ya kuboresha sekta ya afya na baadaye kuandika ilani, lakini katika Kamati ya Ufundi ya Ukawa, tumefanya kazi pamoja. Namfahamu vizuri ni mtu sahihi kwa Chadema katika kuelekea mwaka 2020," alisema.
Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi, alikuwa mzungumzaji wa namna Sera na Ilani ya Chadema inavyoweza kutekelezwa kwa kuwa anaijua kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho na kwamba kwa mwonekano ni mpole na anayezungumza taratibu, lakini anatoa neno zito.
AMWAGA SERA FURAHISHA
Akihutubia mamia ya wananchi wa Mwanza katika viwanja vya Furahisha jana, Dk. Mashinji alisema ataongoza kimkakati zaidi kwa kuwa na mabadiliko ya kimfumo ndani na nje ya chama kwa kujenga matawi ya chama katika kila eneo.
"Naagiza kila kata kuwe na kamati za ufuatiliaji palipo na diwani na ambako hakuna ili kuhakikisha masuala ya wananchi yanafuatiliwa kwa karibu katika sekta mbalimbali kama elimu, maji na mengine. Madiwani wafanye kazi, hatukuwapeleka kuuza sura bali kusimamia kwa karibu maslahi ya wananchi," alisema
Aidha, aliagiza wabunge wote wa Ukawa kugeuza suala la Katiba Mpya ni agenda ya kudumu kwa kila dakika wanazopata ndani ya Bunge na kwamba kikosi cha kimkakati ndani ya chama kitaimarishwa katika utekelezaji wa shughuli zinazolenga kutetea maslahi ya wananchi.
Dk. Mashinji alisema ni lazima maeneo yanayoongozwa na Ukawa, ustawi wa wananchi uonekane na kwamba mambo yatakayosimamiwa ni mabadiliko ya wananchi ili washike hatamu ya chama na viongozi washirikiane nao.
Lingine ni kujiandaa kwenda kwa kasi kwani kwenda pole pole jua litazama na giza kuingia na kushindwa kusonga mbele kufikia malengo ya kuchukua dola m,waka 2020.
ATAJA VIPAUMBELE VYAKE
Dk. Mashinji ameweka wazi vipaumbele vitano ambavyo ataanza navyo baada ya kuingia ofisini katika kuhakikisha Chadema inafanikiwa kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ikiwamo kukipeleka chama hadi kwa wananchi wa kawaida.
Akizungumza jana na Nipashe, aliwashukuru wajumbe wa Baraza Kuu waliompigia kura za ndiyo kwa asilimia 100 huku alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni utekelezaji wa ilani ya Chadema katika halmashauri wanazoongoza, kupinga rushwa na makundi yanayotaka kumea, Katiba Mpya na kusimamia mabadiliko ndani na nje ya chama.
Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu kaulimbiu kubwa ya chama hicho ilikuwa mabadiliko ambayo hayajahitimishwa kwa kushindwa uchaguzi bali yametajwa katika ilani na yatatekelezwa kwa vitendo.
"Baraza Kuu na wengine bado tuna jukumu la kuwasimamia na kuwatetea Watanzania. Tusiogope licha ya watu kunakili mambo yetu na kutaka kuyatekeleza, hawawezi kutufikia sisi ambao ndio tunajua utekelezaji wake, twendeni katika kiini cha tatizo," alisema.
Dk. Mashinji ambaye aliambiwa uteuzi wake na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, wakiwa hotelini, alitaja kingine ni kukisogeza chama kwa wananchi zaidi kwani kufanya operesheni mbalimbali na mikakati ya kichama kwa kuwa mtaji mkubwa wa chama ni watu.
"Msingi wa chama uko chini, mtaji wa chama ni watu na siyo vipeperushi, magari. Hezekiah Wenje akishinda kesi si yeye ni Wananyamagana wameshinda, hivyo ni lazima tuwafikie wannachi huko waliko ili 2020 tuweze kushinda uchaguzi,"alisisitiza.
Alisema kazi iliyoko mbele yake si nyepesi, lakini watafikaje Ikulu itajulikana baada ya kufika mtoni, na kuwataka wanachama na viongozi kutoogopa polisi na vyombo vingine vya dola vinavyotumika kuwanyanyasa.
Kipaumbele kingine ni kusimamia mabadiliko ya Katiba Mpya ambayo yalianza kwa kuhakikisha mifumo iliyopo inabadilika kwa kuwa imekuwa chanzo kikubwa cha kuwanyima haki za msingi na ukuaji wa uchumi wa Watanzania.
"Hatuwezi kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa katiba tuliyonayo au iliyopendekezwa na Bunge Maalumu. Tuna matatizo nyeti ya kitaifa ambayo chanzo chake kikubwa ni mfumo. Ukiangalia suala la rushwa utabaini shida ni mfumo uliopo na ambao tunahitaji kuubadili kwa kutumia Katiba Mpya, hivyo nikiiingia ofisini litakuwa kipaumbele," alisema.
Aliongeza kuwa: "Lengo letu ni nguvu ya umma, tuiwezeshe kutambua haki zao mfano mgogoro mkubwa baina ya wenyeviti na mameya wa halmashauri ni wakuu wa wilaya na mkoa kuingilia utendaji wa halmashauri kwa kuwa kuna mifumo ya kikoloni kwa Katiba Mpya tutaiondoa."
Dk. Mashinji alisema lingine ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chadema 2015, ambayo alishiriki kuiandaa tangu mwanzo na anajua inavyoweza kutekelezwa kivitendo katika halmashauri zinazoongozwa na Chadema katika kuleta maendeleo endelevu ya wananchi.
Katibu huyo ambaye ni Daktari wa Binadamu, alisema pia ni lazima kuwa pamoja katika ujenzi wa chama na kushika hatamu, huku akitumia mfano wa maji ambayo huenda pamoja na yanapofika kwenye maporomoko hushuka pamoja.
Jambo lingine ni kupinga rushwa na makundi ambayo yameanza kumea ndani ya chama, ili kuendelea kukitofautisha chama hicho na kingine na kudhihirishia umma kuwa wamejipanga kushuka dola ifikapo 2020.
WABUNGE CHADEMA WAMZUNGUMZIA
Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffary Michael, alisema chama kimepata mtu sahihi kwa wakati sahihi kwa kuwa moja kwa moja inakwenda kuvunja propaganda zilizopandikizwa kuwa ni chama cha Kaskazini.
Alisema ataleta mawazo mapya ndani ya chama kuliko kuendelea na watu wale wale wenye mawazo yale yale na akipewa ushirikiano ataweza kuvaa viatu vya Dk. Slaa, kwa kusimamia maono yake ambayo alitumia muda wake mwingi katika ujenzi wa chama imara.
Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema uwezo wa mwenyekiti wa taifa kuficha siri ni ushahidi tosha kuwa chama kinasiri na intelejensia ya hali ya juu na kina sifa za kushika dola kwa mwaka 2020.
Alisema Dk. Mashinji si mgeni katika utendaji serikalini na harakati mbalimbali ikiwamo kutetea maslahi ya madaktari na sekta ya afya ambayo inakabiliwa na matatizo mengi hadi sasa, hivyo kwa kumtumia wataweza kunyonya ujuzi na kuupeleka katika halmashauri zinazoongzwa na Chadema.
Naye Mwalimu alisema siku zote duniani hakuna mbadala wa mtu kwa kuwa kila mmoja ana uwezo, uimara na udhaifu wake, kinachotakiwa ni kutekeleza majukumu kwa viwango vinavyotakiwa.
"Nimeshika nafasi ya kaimu katibu, haikuwa kazi rahisi kwa kuwa nafadi hii ni nyeti sana, kila mtu anakuangalia wewe, lakini naamini bosi mpya tuliyempata ni mtu imara, anaijua Chadema siyo kwa kuisoma, bali kushiriki ikiwamo kuandika ilani na machapisho mbalimbali," alibainisha.
Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kiwelu, alisema kwa kiongozi huyo anaiona Chadema mpya kwa kuwa ni mtu mwenye uwezo na anafahamu anachokitenda.
Awali, akizungumza wakati wa kumuombea kura kwa Baraza Kuu, Mbowe, alisema ameona Dk. Mashinji anastahili kuendeleza guruduma la chama hicho kwa kuwa ni mtu makini, mwenye maono na anayejua atendalo.
Mjumbe wa Kamati Kuu, Lowassa, alisema Mbowe amedhihirishia umma kuwa uamuzi wake ulikuwa makini sana kwa kuwa ameleta mtu kijana na shupavu hasa katika nyakati za mabadiliko.
"Tumekupa imani kubwa, chama kinachofuata kuongoza nchi ni Chadema, lengo letu ni kukamata dola na rafiki yetu wa kweli ni kutuwezesha kufika Ikulu 2020," alisema.
WADAU WAPONGEZA
Uteuzi wa Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu wa Chadema umepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wanasiasa na wasomi nchini.
Baadhi ya makundi hayo, wameeleza kuwa Chadema imemteua mtu ambaye alikuwa hafahamiki kwa wananchi, hivyo imekuwa ‘surprise’ kwa wanachama wao, kwa kuwa walikuwa wanatarajia kusikia jina kubwa.
Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulhakim Atiki, alisema pamoja na kuwa Mashinji hafahamiki kwa wananchi, lakini alikuwa ni mmojawapo wa wanachama walioshiriki katika kutengeneza Ilani ya Ukawa wakati wa uchaguzi mkuu.
Alisema ni kijana mwenye uwezo wa kuongoza Chadema kama makatibu wakuu wengine waliotangulia.
Alisema tangu kuondoka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Aman Kabourou, aliyetokea Kanda ya Ziwa, hakukuwa na katibu mkuu mwingine aliyetokea upande huo, hadi alipoteuliwa Mashinji.
“Nadhani Chadema wamezingatia ukanda zaidi, tena ukizingatia wakati wa uchaguzi mkuu maeneo ya Kanda ya Ziwa hawakufanya vizuri, hivyo wamemteua Mashinji ili kujiimarisha zaidi,” alisema.
Naye mwanazuoni kutoka Chuo cha Diplomasia, Israel Sosthenes, alisema hamfahamu Dk. Mashinji vizuri, lakini Chadema hadi kumteua kushika nafasi hiyo ya juu watakuwa wako sahihi na uhakikia na mtu huyo.
Alisema katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu katika usimamizi wa chama, na kwamba ni mapema kumzungumzia kama ataweza au la.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Anna Mghwira, alisema hakuwa anamfahamu Dk. Mashinji, na kwamba amemfahamu mara baada ya kuteuliwa.
Alisema Chadema ni chama kikubwa nchini, hivyo hakiwezi kumtemteua mtu kushika nafasi hiyo kubwa ndani ya chama kama uwezo wake ni mdogo.
Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Siasa ya Sayansi, Dk. Bashiru Ally, alisema hamfahamu Dk. Mashinji utendaji wake kiundani, kwa kuwa ni mara ya kwanza kumsikia.
Alisema anawafahamu viongozi wakuu wote wa Chadema, alisema Dk. Mashinji hakuwahi kumwona kumwona wala kumsikia akishiriki katika masuala ya chama, alisema kama aliwahi kushiriki itakuwa ngazi za chini.
Alisema uteuzi wake unaweza kuwa na faida ndani ya Chadema, kwa kuwa ni mtu ambaye hana mambo mengi kama walivyo viongozi wengine wakubwa ndani ya chama hicho.
Aliongeza kuwa, Dk. Mashinji ni jina jipya pia, ni kijana ambaye anaweza kumudu kazi ya ukatibu mkuu wa chama.
Chanzo. Nipashe