Pages

Saturday, February 22, 2014

Kinega: Kijana ‘muuza unga’aliyepitia misukosuko mingi katika maisha

 Baada ya kufika kwenye nyumba wanayoishi wale vijana watatu, aliwakabidhi zile barua na papo hapo wakaelewa nini anachotaka kwao.  Wao wakamwonyesha mzigo, ambao ulikuwa ni bangi inayolimwa wilayani humo.  Kisha, wakamwambia bei ya mzigo ambapo alitoa kiasi cha Sh 40,000. Walimuuzia kila kifurushi kwa Sh 12,000. Kwa mzigo alionunua angepata kiasi cha Sh 300,000 atakapouza jijini Dar es Salaam.

Na Florence Majani, Gazeti la Mwananchi

Dar es Salaam. Safari yangu ya kukutana na Wilfred Joseph, (Kinega) inaanza saa 4:30 asubuhi.
Ninaelekea Keko Machungwa, wilayani Temeke, ambako anaishi Kinega. Kwa mwendo wa daladala, nafika nyumbani kwake saa 6:15 mchana.
Namkuta akiwa kwenye shughuli zake, karibu na Deluxe Bar na hapo anaanza simulizi  ya safari ya maisha yake, kutoka uanafunzi wake, hadi muuza dawa za kulevya na mtumiaji nguli aliyepitia misukosuko mingi kimaisha.
Anasema baada ya kumaliza darasa la saba, wazazi wake walimtafutia shule ya sekondari mkoani Lindi.
Akiwa kidato cha tatu, ulitokea ugomvi baina yake na mwenzake ambaye alizimia, jambo ambalo unaweza kusema ndiyo mwanzo wa historia ndefu ya maisha yake.
“Nilipigana naye, akazimia. Kwa hiyo, uongozi wa shule ukaamua kunisimamisha masomo na kuniamuru nirudi nyumbani,” anasema Kinega.
 Anaongeza kuwa baada ya kurudi nyumbani wazazi wake waliketi naye kujadili ni jambo gani atalifanya baada ya kusimamishwa masomo. Hata hivyo, hakuwa na chochote cha kufanya kwa kipindi hicho.
Sh40,000 za godoro
Anasema siku moja, mama yake alimpa fedha kiasi cha Sh40,000 ili akanunue godoro Kariakoo, alipofika  huko, akakutana na rafiki wa kaka yake, ambaye baada ya kumweleza kuwa ametumwa godoro na ana kiasi fulani cha fedha, alimpa ushauri wa kuanzisha biashara. “Yule rafiki wa kaka aliniambia, kama nina hela kiasi hicho na shule nimesimamishwa kwa nini nisifanye biashara? Akaniambia tuanze kuuza bangi,” anasema.
“Yule kijana aliniambia kuwa mzigo unapatikana Kyela,  Mbeya na hiyo biashara ina hela nzuri, kisha akanipa barua tatu na kuniagiza mtaa maalumu huko Kyela, kituo cha mabasi ambako nitawakuta wenyeji wangu.
Aliporudi nyumbani alikuwa akiwaza kwa kina atawaambiaje wazazi wake kuhusu ulipo mzigo alioagizwa.
Kwa bahati nzuri, hakuwakuta kwa hiyo akachukua nguo zake na kurudi kwa rafiki yake na siku iliyofuata, saa 11:00 alfajiri, akaondoka na kupanda basi kuelekea Kyela.
“Nilianza safari nikiwa na barua zangu tatu, nilishuka nikaelekea nilipoelekezwa na kaka, nilipata ugumu kidogo wa ramani, lakini nilielekezwa na nikafika salama, ” anasema.
 Alipofika akapokewa na vijana watatu  alioagizwa kwao, ambao walimpokea baada ya kujitambulisha kuwa ni ndugu wa mtu fulani (kaka yake) na kuanza safari ya kwenda kwenye nyumba wanayoishi.
Wakati wanapita kuelekea wanakoishi vijana hao, wakasimamishwa na wasichana waliokuwa wameketi nje ya nyumba moja, wasichana hao walilalamika kwa nini hawajatambulishwa mgeni.
“Wale wasichana walipotambulishwa kuwa mimi ni mdogo wake Chedi,  basi walilaumu sana kwa nini wenyeji wangu hawakunitambulisha ili wanisalimie wakati Chedi alikuwa ana mchumba hapa? Nikawapa mikate niliyonunua njiani na tukaendelea na hamsini zetu,” anasimulia Kinega.
Baada ya kufika kwenye nyumba wanayoishi wale vijana watatu, aliwakabidhi zile barua na papohapo wakaelewa nini anachotaka kwao.  Wao wakamwonyesha mzigo, ambao ulikuwa ni bangi inayolimwa wilayani humo.  Kisha, wakamwambia bei ya mzigo ambapo alitoa kiasi cha Sh40,000. Walimuuzia kila kifurushi kwa Sh12,000. Kwa mzigo alionunua angepata kiasi cha Sh300,000 atakapouza jijini Dar es Salaam.
Kinega anasema akiwa hapo alibaini kuwa mzigo mwingine unalimwa hapo Kyela na mwingine unatoka Malawi.
“Sikutaka kukawia, niliwaambia wenyeji wangu ninataka kuondoka siku inayofuata kwa hiyo wakanifungia mzigo, wakaupaki vizuri na kweli uliingia mzigo wa maana kwenye mabegi, kisha wakanisindikiza kwenda kituoni,” anasema.
 Wakati wanaelekea kituoni wakapita katika nyumba ile ile ambayo kuna wale wanawake aliokutana nao siku iliyopita. Hata siku hiyo waliwakuta wanawake hao ambao walitaka kumsindikiza.
Mbele ya polisi Kyela
Wanawake hao walibeba mabegi na safari ya kuelekea kituo cha mabasi ikaanza. Ghafla, wakati wakiendelea na mazungumzo, likatokea kundi la polisi, hali ambayo ilisababisha wale vijana watatu kutawanyika.
 “Wale vijana walipotawanyika, tukabaki mimi na wanawake watatu wakiwa wamebeba mabegi yangu, hata hivyo wale polisi hawakufanya chochote zaidi ya kusema ‘nyinyi  kina Mjuba, kina Amos kila siku mnauza mawese halafu mnakaa kimya eeh?” anasimulia.
“Wale polisi wale hawakufanya chochote nami na wenzangu tuliendelea na safari yatu hadi kituo cha mabasi.”
Walipofika kwenye gari walipakia mizigo na ilipotimu saa 8:00 usiku safari ilianza kuelekea Dar es Salaam. Ikumbukwe kuwa, miaka ya 1990 mabasi karibu yote yalikuwa yakiruhusiwa kutembea usiku.
 “Nilifika Dar es Salaam asubuhi na nilipokewa na rafiki mwenye gari aina ya Land Rover, ambaye nilimwambia anishushe kwa rafiki yangu mwingine. Nikatua mizigo yangu na kwenda nyumbani, ” anasema Kinega huku tukiwa tumeketi kwenye kibaraza nje ya nyumba yao.
Siku iliyofuata, anasema alikwenda kwa rafiki yake ambako aliacha mizigo yake na kumweleza ni kipi kilicho ndani ya mabegi yale. Kwa bahati mbaya au nzuri, rafiki yake alikuwa akifahamu ubora wa bangi ndipo alipoijaribu na kuisifia kuwa ni bangi bora.
“Cha ajabu, rafiki yangu akasema anataka kuununua mzigo wote, akaniuliza bei, nikamwambia na hapohapo akanipa Sh150,000 za kwanza,” anasema.
Baada ya Kinega kupata fedha kiasi kikubwa kwa wakati ule  hakutaka kulaza damu, aliamua kutopoteza muda na akaamua kupumzika siku moja kabla ya kurudi tena Kyela kuchukua mzigo mwingine.
 “Niliona daah, haya si ndiyo maisha. Nikasema  acha nirudi tena Kyela nikachukue mzigo mwingine, nikageuza baada ya siku moja,” anasema.
 Kweli, Kinega aligeuza na kwenda tena Kyela akitumia kiasi cha fedha aliyopata ya faida yake ya kwanza kuchukua mzigo mkubwa zaidi.
Balaa la kwanza
Aliweza kuondoa harufu ya bangi kwa kupulizia marashi ya blue lady na one wish, yenye harufu kali.
 Alifanya hivyo mara tano au  sita  hivi lakini siku moja, kama balaa lisivyoweza kutabirika, Kinega alikamatwa.
Alikamatwa akiwa tayari amefika jijini, eneo la Keko Mwanga  kwani siku hiyo, rafiki yake mwenye gari hakuja kumpokea kama kawaida.
“Basi, ile nashuka tu, tayari nimeshaita teksi, nimepakia mzigo, nikashangaa watu watatu wananifuata  ambao wamevaa kiraia. Wakaipekua mizigo yangu na kweli wakaikuta bangi,” anasema.
Polisi wale wakamwamuru Kinega kuingia ndani ya teksi aliyoikodi, kisha wakamwambia dereva aelekee kituo cha polisi Chang’ombe.
“Nilichokuwa nikijaribu licha ya kuwa sikuwa na uzoefu, ni kutafuta njia ya kuwapoza. Basi, nikamwambia dereva apite njia ya mbali ili safari iwe ndefu nizungumze nao,” anasema.
Itaendelea

MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA MAULIDI MSIKITI WA CHANGANI-TEMEKE


 Baadhi ya waumini wa dini ya kiislam wakifurahia maadhimisho ya maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W yaliyofanyika msikiti wa qadiriyah Temeke







Wednesday, February 12, 2014

MAZISHI YA SEIF MTAMBO (ODERA)

 Baadhi ya waombolezaji wakibeba jeneza la aliyekuwa kipa wa zamani wa Mtibwa Seif Mtambo ODERA ambaye alizikiwa katika makaburi ya Mtoni kwa kindande
 Mbunge wa Temeke Mh.Abbas Mtemvu alikuwa mmoja wa wahudhuriaji katika msiba huo